Na Saleh Ally
HIVI
karibuni, timu kadhaa zinazoshiriki Ligi ya Mpira wa Kikapu nchini Marekani
(NBA), zilianza kuonyesha nia ya kumuwania Mtanzania Hasheem Thabeet Manka.
Timu
hizo zilionyesha nia kutokana na maendeleo mazuri ya Hasheem katika timu yake
ya Grand Rapid ambako ameendelea kuonyesha ubora wakati ikipambana katika
D-League ya NBA.
Wachezaji
wengi ambao wanakuwa hawajafanya vizuri, hushiriki katika ligi hiyo. Hasheem,
aligoma kusaini kuzitumikia timu kubwa za mpira wa kikapu barani Ulaya katika
nchi za Hispania, Ugiriki na kwingineko, akaamua kubaki D-League.
Angekubali
kwenda Ulaya, pamoja na donge nono angekuwa gumzo barani humo. Lakini imani
yake, ilikuwa ni anaweza kurudi NBA na sasa timu zimeanza kuonyesha nia kwake,
jambo ambalo linathibitisha kweli inawezekana kwake.
Hasheem
amekodi kocha maalum ambaye ni maarufu na ana uwezo mkubwa na hutumiwa na
wachezaji wengine nyota wa NBA. Malipo ya kocha huyo yanaonyesha ni hadi dola
20,000 (zaidi ya Sh milioni 42.4) kwa mwezi kwa wanaomkodisha. Lengo la Hasheem
ni kujiweka sawa, awe fiti na mwisho arejee NBA.
Hasheem
ni binadamu, Mtanzania wa kwanza kucheza NBA akitokea kwenye nafasi ya draft
katika kundi ambalo wako wanaoendelea kufanya vizuri kama DeMar DeRozan na Stephen
Curry.
Inawezekana
kama binadamu aliteleza, lakini utaona kwa kiasi gani wengi wameishia kumsema,
hakuna aliyeonyesha sapoti.
Angalia,
hukuwahi kusikia kiongozi hata wa serikali au yule wa mpira wa kikapu akimpa
moyo kwamba siku moja atarejea na kipi cha kufanya.
Hasheem
anarudi kwenye historia tena, kama ambavyo alifikia hapo, ameanza mwanzo kwa
kufanya mazoezi makali, juhudi ya juu na kama kuna sehemu alikosea amepaona na
anapafanyia kazi.
Wakati
anachipukia, hakukuwa na kiongozi wa serikali wala vyama vya mpira wa kikapu
aliyemsaidia, maana wote waliamini hana uwezo. Akapambana sana, mwisho akawa
gumzo la taifa, nyota ya taifa, mwanamichezo ghali zaidi kuwahi kutokea
Tanzania. Akageuka furaha na faraja ya wote.
Alipoonekana
kuyumba, akawa gumzo na sehemu ya watu kuweka maneno ya kila aina. Sasa ameamua
kukaa kimya, peke yake tena anapambana tena na inawezekana siku nyingine
akarejea tena.
Ana
nafasi ya kurejea kwa kuwa rekodi zake za mwisho kwenye D League akiwa na Grand
Rapid zinaonyesha ana nafasi.
Lazima
tukubali, Hasheem hakubahatisha na anaweza kuwa mtu wa mfano kama utatulia na
kujiuliza umbali wa NBA na yeye alifikaje maana kufika hapo, kuanza kupambana
na watu kama Kobe Bryant wakati wakicheza na wengine, si kazi ndogo.
Rekodi
zake za mwisho na Grand Rapids Drive, zinaonyesha alicheza mechi 23 akiwa na
wastani wa pointi 1.2 , rebaundi 1.7, blocks 4, hii ni katika kila dakika 8.3
za mchezo.
Katika
msimu uliopita wa D League, wastani wake ulikuwa bora zaidi hadi kufikia pointi
8.6, reboundi akapata 6.2, blocks ikawa pointi 2.4, hii ni ndani ya kila dakika
22.2.
Lakini
katika wachezaji wote wa D League, alishika namba tatu kwa kuwa na blocks 117,
namba nne kwa kuwa na ubora wa ulinzi akipata pointi 101.3, na namba tano
kwenye blocks baada ya kupata asilimia 8.7.
Hasheem
mwenye umri wa miaka 29, ni Mtanzania wa aina yake, alijiinua peke yake,
kaanguka anaweza kujiinua tena. Jambo ambalo bado tunaweza kujifunza ni kwamba
unaweza kupambana ukiwa na watu wachache na ukashinda.
0 COMMENTS:
Post a Comment