October 3, 2016Imeelezwa kuwa maamuzi ya mwamuzi, Martin Saanya ambayo hayakuwa yakikubalika kwa mashabiki wengi wa Simba juzi Jumamosi, yamesababisha kifo cha shabiki na mwanachama wa klabu hiyo, Haji Mkelo kilichotokea asubuhi ya jana Jumapili mkoani Morogoro.

Katika mchezo huo ambao Yanga na Simba zilitoka sare ya bao 1-1, Saanya alikuwa akilalamikiwa zaidi na mashabiki wa Simba kutokana na kile kilichoonekana kuibeba zaidi Yanga.

Kifo cha mwanachama huyo wa Simba kutoka Tawi la Dumila Morogoro, kilitokea nyumbani kwake baada ya kurudi salama na wenzake kutoka Uwanja wa Taifa, Dar ambapo mechi hiyo ilipopigwa.

Imeelezwa kuwa, mwanachama huyo akiwa na wenzake wa tawi hilo, walisafiri kutoka Morogoro mpaka Dar kuushuhudia mchezo huo, lakini mara kwa mara alikuwa akipandwa na presha kutokana na kutokubali maamuzi ya Saanya.

Wakati wakiwa uwanjani, presha ilimpanda Mkelo, baada ya kupatiwa huduma ya kwanza, akarudi kwenye hali yake na kuendelea kuushuhudia mchezo huo.

Wakiwa njiani kurejea mkoani Morogoro, mwanachama huyo mara kwa mara alikuwa akilaumu uamuzi wa Saanya ambapo walifika Morogoro saa saba usiku na kwenda kupumzika nyumbani kwake, lakini asubuhi presha ikampanda zaidi, akaaga dunia.

Ally Omary Buruani ambaye ni mwanachama wa tawi hilo, amelieleza gazeti hili: “Tumesikitishwa na kifo cha mwanachama mwenzetu na leo (jana) jioni tunaenda Turiani katika Kijiji cha Kibati kwa ajili ya mazishi yatakayofanyika kesho (leo) Jumatatu.”0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV