October 1, 2016


Licha ya kuwa na matumaini makubwa ya ushindi kwenye mechi ya leo dhidi ya Yanga, Simba imeingia hofu na kuwawekea ulinzi mkali wachezaji wake wakiwemo Ibrahim Ajibu na Laudit Mavugo.

Simba inacheza na Yanga mechi namba 43 ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo timu hizo zilikuwa katika maandalizi makali ili kukabiliana.

Yanga wenyewe waliweka kambi Pemba huku Simba ikiwa Morogoro. Sasa kuelekea mchezo huo, Simba iliamua kuwawekea ulinzi nyota wake na kutotaka mtu yeyote kutazama mazoezi yao jana Ijumaa.

Simba chini ya Kocha Joseph Omog raia wa Cameroon, jana ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana uliopo Posta jijini Dar es Salaam huku ikiwa imeimarisha ulinzi.

Salehjembe ambayo ililishuhudia ulinzi mkubwa uliowekwa na uongozi wa timu hiyo.

Meneja wa Simba, Mussa Mgosi ndiye aliyeongoza ulinzi huo kuzunguka uwanja wote kwa kuhofia hujuma za watani zao Yanga.

Wakati mazoezi hayo yakiendelea, Mgosi alionekana akiwafukuza baadhi ya watu waliokuwepo nje ya uzio wa uwanja huo waliokuwa wakirekodi mazoezi hayo kwa simu zao za mkononi.

Meneja huyo, mara baada ya kufanikiwa kuliondoa kundi hilo la watu, haraka aliwafuata waandishi wa gazeti hili na kuwazuia kupiga picha na kufuatilia programu za timu hiyo zilizokuwa zinaendelea uwanjani.

“Mpiga picha eheee! Inatosha hizo picha ulizozipiga, ujue tupo vitani na hatutaki mambo yetu yaonekane kwa uwazi, tulipanga kufanya kwa siri.

“Naomba muondoke eneo hili, halafu mbona mnatufuatilia, basi nendeni na Pemba kwenye mazoezi ya Yanga,” alisikika Mgosi akilalamika.


Katika hatua nyingine, Omog alifanya kikao na wachezaji wake kabla ya kuanza programu zake katika mazoezi hayo akitumia dakika 20 kuanzia saa 3:10 hadi 3:30 asubuhi wakijadili masuala mbalimbali.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV