October 31, 2016



Simba na Yanga, zimekutakana juzi Jumamosi lakini hazijafikia mwafaka kuhusiana na suala la beki Hassan Kessy ambaye Simba inamtuhumu kusaini kuichezea Yanga huku akiwa bado ana mkataba na Msimbazi.

Mjumbe wa Shirikisho la Soka Tanzania  (TFF) ambaye pia ni  Mjumbe wa Heshima wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Said El Maamry, aliyepewa jukumu la kuzisuluhisha timu hizo baada ya viongozi wa Yanga na Simba kwa kushirikiana na wale wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF, kumpendekeza kuwa msuluhishi wao, amesema kwamba kilichosababisha lisipatiwe ufumbuzi hiyo juzi ni kutofika kwa mjumbe muhimu wa Yanga.

Alisema mjumbe huyo ni Wakili wa Yanga, Alex Mgongolwa ambaye alishindwa kufika katika mkutano huo kutokana na kuwa na matatizo ya kifamilia yaliyomfanya asafiri kwenda mkoani Iringa.

“Tulikutana jana (juzi) kwa ajili ya kulipatia ufumbuzi suala hilo lakini bahati mbaya hatukuweza kufanya chochote baada ya viongozi wa upande wa Yanga kutotimia ambapo wakali wao, Alex Mgongolwa hakuweza kutokea kutokana na kuwa na matatizo ya kifamilia.

“Alipata msiba hivyo akasafiri kwenda Iringa kwa ajili ya suala hilo ndipo viongozi wa Yanga waliofika katika mkutano huo wakaniomba tuahirishe mpaka hapo atakapokuwa amerudi.

“Kutokana na hali hiyo ilibidi nikubali ombi hilo, hivyo tutakutana tena siku ya Alhamisi baada ya Mgongolwa kurudi kwani anatarajia kurudi Jumanne (kesho),” alisema El Maamry.

Timu hizo mbili zipo katika mvutano mkubwa ambapo Simba inataka ilipwe na Yanga dola 600,000 (zaidi ya Sh bilioni tatu) kama fidia kwa kile kinachodaiwa kuwa ilimsainisha Kessy mkataba wa ajira wakati akiwa bado yupo na mkataba na klabu hiyo.

Simba ambao walifika kwenye kikao hicho kwa ajili ya kulimaliza suala hilo, ndiyo walalamikaji kwamba Kessy alisaini mkataba na Yanga wakati bado akiwa na mkataba nao.

Kamati ya TFF ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji tayari ilikaa na kufikia uamuzi lakini haiikuutangaza na badala yake ikataka pande hizo mbili kukutana na kulisuruhisha.

Taarifa za ndani zinaeleza, Yanga imepigwa kumbo katika kesi hiyo kwa kuonekana ilimsainisha Kessy akiwa na mkataba lakini kamati hiyo imetoa nafasi hiyo ya kiungwana kama pande hizo mbili zinaweza kumalizana.

Iwapo Yanga ambao ni walalamikiwa na Simba ambao ni walalamikaji watashindwana katika hilo, kamati hiyo itatangaza adhabu hiyo ambayo itakuwa na athari kubwa zaidi kwa Yanga.



1 COMMENTS:

  1. Yanga imepigwa kumbo kivipi wakati hakuna taarifa rasmi ya TFF?

    Umeanza tena mambo yako? Wakati wa sakata la Okwi nilifika mahali nikaamini kufuatia nakala zako kwamba Ismail Aden Rage alikula hela ya uhamisho wa mwisho.

    Mwishowe uliumbuka baada ya Simba kupokea malipo toka Ttoile du Sahel. Sasa umeanza kutengeneza uongo mwingine kuhusu sakata la Kessy. Utakua lini?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic