November 26, 2016Hatma ya Malimi Busungu kubaki Yanga inasubiri majaliwa ya Kocha George Lwandamina ambaye ameomba CD za mechi zote za timu hiyo ili kuangalia kiwango cha kila mchezaji kisha aamue kama atambakisha ama la.

Busungu alishakubali kuondoka Yanga katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo na baadhi ya timu zilipanga kumsajili kwa mkopo baada ya kuona hana nafasi katika kikosi cha kwanza.

Hata hivyo, Lwandamina, raia ya Zambia, aliyejiunga na Yanga akitokea Zesco ya nchini kwao, ameagiza kutofanyika jambo lolote la usajili kwa sasa hadi atakapoona viwango vya wachezaji wake.

Meneja wa Busungu, Yahya Tostao, alisema awali kulikuwa na mchakato wa kumtoa kwa mkopo Busungu na timu nne zilionyesha nia ya kumhitaji.

“Mambo yote yamesimama kwanza kwani Lwandamina anataka kwanza kupitia CD za mechi zote ili kufahamu kama atamhitaji (Busungu) kwa ajili ya kufanya naye kazi ama la.


“Iwapo hatamhitaji, itabidi tuendelee na mpango wa kumpeleka kwa mkopo katika timu nyingine, kwa sasa bado tunaendelea na mazungumzo na timu zinazomhitaji Busungu,” alisema Tostao.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV