November 26, 2016



Kocha Hans van der Pluijm, amesema suala la nani bosi haliwezi kuwa kitu muhimu, badala yake ushirikiano wake yeye na George Lwandamina ndiyo jambo bora zaidi.

Pluijm amepanda cheo na kuwa mkurugenzi wa ufundi wa Yanga, wakati Lwandamina anachukua nafasi yake kama kocha mkuu.

"Lengo ni mafanikio ambayo yatazaliwa na ushrikiano, nani bosi nani mkubwa haliwezi kuwa suala la msingi sana. Mwisho wa msimu, tunatakiwa kuwa na mafanikio," alisema.


Jana, rasmi Yanga ilimtambulisha Lwandamina kuwa kocha wake mkuu pia ikamtambulisha Pluijm kuwa mkurugenzi wa ufundi, klabu hiyo imesema Pluijm ni bosi wa Lwandamina.

Awali kulikuwa na sintofahamu kuhusu nafasi ya Pluijm raia wa Uholanzi kwamba labda angekuwa chini ya Lwandamina raia wa Zambia aliyejiunga na Yanga akitokea Zesco ya nchini kwao.

Akimtambulisha kwa waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, alisema Lwandamina ni kocha mkuu atakayekuwa chini ya Pluijm ambaye yeye atakuwa akizitazama timu zote za Yanga.

“Pluijm yeye ni bosi wa timu zote za Yanga kuanzia hii ya wakubwa hadi ile ya vijana na nyingine zitakazoanzishwa, ila majukumu ya Pluijm kwa Lwandamina yataishia nje ya uwanja.

“Ndani ya uwanja kwa timu ya wakubwa bosi atakuwa Lwandamina na hataingiliwa na Pluijm labda kushauriwa tu, hivyo ndivyo watakavyofanya kazi,” alisema Sanga.

Akizungumza baada ya kutambulishwa, Pluijm alisema atahakikisha anafanya kazi bega kwa bega na Lwandamina ili kuipa mafanikio Yanga kuanzia pale alipoachia yeye.

“Nitafanya naye kazi kwa karibu kwa manufaa ya Yanga na Tanzania, naamini tutakuwa na matokeo mazuri ya pamoja hivyo mashabiki wasiwe na wasiwasi,” alisema Pluijm.


Kwa upande wake, Lwandamina alisema: “Nitajitahidi kufanya kazi pamoja na Pluijm kuhakikisha Yanga inapiga hatua zaidi kutoka mahali ilipo sasa.” 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic