November 28, 2016Na Saleh Ally
TANGU dirisha dogo la usajili la Ligi Kuu Bara lifunguliwe Novemba 15, mwaka huu kumekuwa na maneno mengi kuhusiana na masuala ya usajili kwa karibu kila klabu.

Dirisha hilo litafungwa Desemba 15, mwaka huu na inawezekana kabisa si vibaya kusema kwa kila timu inayotaka kufanya mabadiliko katika kikosi chake ina nafasi kubwa ya kufanya namna hiyo kwa kuwa muda unatosha.
Maana wakati ligi inaendelea, mfano hivi; zinapofikia mechi kumi za mzunguko wa kwanza, timu kupitia benchi la ufundi inaweza kujua inahitaji kufanya mabadiliko katika sehemu ipi.

Katika mechi tano za mwisho kwa kuwa kila mzunguko una mechi 15, klabu itakuwa imejua kuwa kweli hasa inahitaji kufanya mabadiliko wapi na kwa sababu zipi ili kuhakikisha inamaliza kwa uhakika ngwe ya pili yenye mechi 15 pia ambazo huongezeka ugumu zaidi ya ile ya kwanza.

Ngwe ya pili inaongezeka ugumu kwa kuwa kunagawanyika makundi matatu marazote. Kunakuwa na kundi la kwanza lenye timu kuanzia tano hadi saba ambazo zinapambana kuepuka kuporomoka daraja. Timu nne hadi tano zinazowania kubaki ligi kuu na nyingine tatu hadi nne zinazowania kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Hivyo malengo huwa mbele kwa kila kikosi na hapo ndipo ugumu huongezeka kwa kuwa kila upande unakuwa umejua upo kundi gani na unataka nini, hivyo hakuna anayekubali kupoteza kirahisi.

Washambuliaji wawili wa Simba, Laudit Mavugo raia wa Burundi na Frederic Blagnon kutoka Ivory Coast wamefunga mabao matano tu kwa ujumla katika zaidi ya mechi 15 walizocheza kama utazijumlisha kwa wote.

Wachezaji hawa iko hivi; Mavugo amefunga mabao manne, Blagnon amefunga moja. Baada ya hapo, mambo yakawa magumu kwao na wakati mwingine wakaonekana wana presha kubwa sana.

Wakati tumeingia kwenye usajili, kumekuwa na tetesi za kila aina kuhusiana na usajili wa Simba ingawa Kocha Joseph Omog amesema anataka kipa, beki wa kati na mshambuliaji. Sasa sijajua kwa nini ni mshambuliaji?

Ukiangalia bado inaonekana hivi, hawa wawili, kila mmoja amekuwa mfungaji bora katika ligi ya kwao. Kama Burundi si ligi ngumu, mmoja wa washambuliaji wake Amissi Tambwe sasa anasumbua kwa misimu mitatu mfululizo.

Ligi ya Ivory Coast hakuna ubishi ni ngumu kuliko ya hapa nyumbani. Na utakubaliana nami kwamba hawa wawili hakuna ambaye amepata nafasi ya kutosha na kuaminika angalau kumaliza dakika 90 mara saba ili kumuongezea hali ya kujiamini.

Bado kila mmoja hana uhakika wa kuanza kwa kuwa Omog ambaye ni kocha mgeni naye yuko bizeanajenga kikosi chake. Hivyo leo huyu na kesho yule, ukichanganya na kutozoea mazingira kwa kuwa wanatokea nchi tofauti katika mazingira ya Francophone (nchi zinazozungumza Kifaransa) na kufanya kazi katika Anglophone (nchini zinazotumia Kingereza), tena hapa ni Kiswahili zaidi, basi utajua kuna mengi wanatakiwa kuyazoea na ndani ya mechi 15 pekee, si rahisi.

Hii inaweza kutokea kwa mchezaji mmojammoja kama vile Tambwe ambaye alipata bahati ya kuanza vizuri na kusonga mbele. Lakini si rahisi kumtokea kila mmoja.

Ukimuangalia Mavugo, mimi niko tayari kuweka shilingi yangu, kwamba Simba wakimuamini, anaweza kuja kuwa mchezaji hatari zaidi kuliko wote Ligi Kuu Bara.

Lakini kwa aina ya mshambuliaji wa kati anayekuwa kama Didier Drogba. Yule Blagnon, siku itafika kama Simba watamuamini. Simba watajidanganya na kujichanganya kama watasajili mshambuliaji mwingine wa nje.

Kusajili mshambuliaji mwingine wanje ni kujichanganya kwa kuwa bora Mavugo au Blagnon ambao wameozea kwa mechi 15 za mwanzo, wakirejea watakuwa wamejifunza jambo na kujipanga.

Akiletwa mwingine mpya kutoka nje, naye atakuwa na mechi 15 za kujifunza za Ligi Kuu Bara mzunguko wa pili na haitakuwa faida yenye afya kwa Simba.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV