Na Saleh Ally
KUNA wakati fulani nilifanya mahojiano na bondia mmoja, akakubali kwamba wamekuwa wakifanya makosa mengi kutokana na kitu alichokiita “njaa”.
Njaa kamwe huwa haiishi, tena ni ya ajabu sana, hata ukila asubuhi, mchana inarudi, ukila tena usiku inarudi na itakupumzisha unapokwenda kulala. Utakapoamka tu, unaamka nayo!
Najua njaa aliyomaanisha ni ukosefu wa fedha, lakini ukipata fedha ndiyo hiyo inahusisha kuendesha maisha ikiwa ni pamoja na kuitibu njaa.
Njaa haiishi, ukilainisha mambo kwa kukiuka utaratibu au usahihi wa mambo kwa lengo kwa kutaka kuitibu, ndiyo unajikuta unaanza kufeli mambo mengi sana ya msingi ambayo ungeweza kuyaweka sawa taratibu lakini ukaenda katika njia sahihi.
Francis Cheka ni kati ya mabondia bora kabisa nimewahi kuwaona hapa nyumbani. Lakini kwa mwendo anaokwenda huenda pia ni mwendesho wa hiyo ‘njaa’, kuna dalili zote kwamba mwisho wake kama bondia mahiri umekaribia na hii inanisikitisha sana.
Nianze na hayo masikitiko kwa kuwa nilishiriki kwa ukaribu wakati Cheka akianza kuinuka na wakati fulani nilitaka kuzichapa na promota wake ambaye alimdhulumu fedha zake halafu nilipoandika habari, eti akatishia kunitwanga ngumi maana nimefichua siri.
Lengo langu lilikuwa ni kumsaidia Cheka ambaye wakati huo ndiyo alikuwa anatoka katika ngumi za ridhaa na kuingia kwenye ngumi za kulipwa ambazo zilihitaji msaada wa mtu makini na si yule promota ambaye alionyesha wazi alitaka kumtumia ili kuchuma zaidi.
Cheka ambaye sasa ni mkomavu akiwa na rekodi ya kuwahi kuwapiga karibu mabondia wote maarufu wa Tanzania anashindwa kuelewa anachokifanya na kuiacha ‘njaa’ iwe mwongozo wa maisha yake kwa kuwa ameingia mkataba wa kucheza mapambano mawili makubwa na tofauti ya siku za kucheza ni wiki moja tu.
Pamoja la kwanza amecheza nchini India juzi na kuchapwa kwa Technical Knockout (TKO) na bondia Mhindi, Vijenger Singh! Raundi ya tatu, Cheka aliomba ‘Po’ akionyesha mambo hayakuwa mazuri na hakuweza tena kuendelea na pambano.
Lakini baada ya pambano hilo, Cheka ameugeuza mchezo wa ngumi kama Ligi Kuu Bara kwa kuwa anacheza mechi mbili za ngumi ndani ya siku nane. Haya ni maajabu ya dunia.
Cheka sasa ana pambano jingine aliloingia mkataba na anatakiwa kucheza na Dulla Mbabe, mechi inachezwa Desemba 25, ikiwa ni ndani ya siku nane tu tangu apigane India.
Kumbuka safari ya kutoka India kuja Tanzania, ukijumlisha saa za ndani ya ndege na kusubiri uwanja wa ndege ‘Transit’, haiwezi kuwa chini ya saa nane.
Bondia ambaye ameshindwa kumaliza raundi hata tano akionekana kabisa hakuwa anajiweza. Leo anarejea kupigana na bondia ambaye anachipukia kwa kasi kubwa, ambaye ameonyesha uwezo mkubwa.
Kwanza kwangu naona kweli mapromota si watu wanaowajali mabondia tena hata kidogo. Lakini pia naingiwa hofu kuu na wale waliopewa kusimamia ngumi na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kwamba hawana meno, kama wapo wamelala na kama hawajalala basi hawaoni na hawajui wanalolifanya.
Huyu Cheka anauwawa na hawa mapromota wawili ambao wanamuandalia mapambano mawili magumu kabisa ndani ya siku nane, wote mmekaa kimya mkimuangalia anakwenda kwisha kabisa.
Pambano na bondia Singh, Cheka alipigwa kama mtoto, wote tuliona na mwisho tukafanya ujinga, akatangazwa kuwa mshindi. Tumeona pambano la India, Cheka hajarudi tena katika kiwango chake tunachokijua, ajabu kabisa, vyombo vinavyosimamia ngumi, vipo na vimepitisha amalizwe kabisa.
Kama cheka atapigwa na Dulla, basi safari ya bondia bora wa Tanzania imemkuta na hatakuwa na nafasi ya kurejea. Kwanza kiwango chake kimeshuka, lakini akiwa hajajiweka vizuri, anapigana mapambano mawili ndani ya siku nane. Hata ni maajabu na kweli kama atapoteza dhidi ya Dulla, itakuwa ni safari yake na mwisho atabaki bondia wa kawaida. Salama au ukombozi wake, labda afanye maajabu na kushinda pambano hilo. Tusubiri.









0 COMMENTS:
Post a Comment