December 19, 2016


Na Saleh Ally
NILIKUWA nina hamu kubwa kutaka kuona kile ambacho Yanga wanaweza kubadilisha baada ya benchi la ufundi la Kocha George Lwandamina kuingia kazini.

Lwandamina, raia wa Zambia, amechukua nafasi ya kocha Hans van Der Pluijm, raia wa Uholanzi ambaye msimu uliopita alikuwa na mafanikio makubwa kweli baada ya kubeba ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo, pia akachukua Kombe la FA lililokuwa limerejeshwa.

Pluijm anaondoka, Lwandamina anaingia na Yanga ina hamu ya mafanikio. Kumbuka imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa katika nafasi ya pili, ikiwa ni tofauti ya pointi mbili badala ya zile nane hadi mechi ya 13 kwa kila timu.

Kwa kawaida, hesabu zote zilionyesha Lwandamina ndiye kocha mwenye mtihani mgumu zaidi kuliko mwingine Ligi Kuu Bara kwa kuwa amechukua kikosi ambacho kinaonyesha hakikuhitaji kocha mpya kutokana na kazi nzuri iliyokuwa inaendelea.

Mechi ya kwanza dhidi ya JKT Ruvu ambayo inakuwa ni ya 16 kwa Yanga msimu wa 2016-17, Lwandamina ameonyesha kama atakwenda na muunganiko ambao anautengeneza na wachezaji wakamuelewa kweli, basi Yanga inaweza kuwa bora maradufu kuliko ilivyowahi kuwa au kudhaniwa.

Lwandamina akifanikiwa, kila kitu kikaenda alivyopanga, Yanga hawatakuwa wanashikika. Lakini kama watashindwa kumuelewa, basi huenda mambo yakawa magumu zaidi Yanga.
Uchezaji wa mechi dhidi ya JKT unaonekana wachezaji Yanga wameanza kumuelewa vizuri na “Chemistry” imeanza kukubali na ikikaa sawa, basi watatisha na kuwa hatari.


Kikosi:
Unagundua Lwandamina amepanga kikosi ambacho si kigeni kabisa, lakini anafanya kile ambacho Pluijm hakukitaka kitokee mwanzo. Kuanza kumpanga kiungo Thabani Kamusoko namba sita. Alifanya hivyo mara chache, lakini kwa Mzambia huyo akijua Justice Zulu yuko jukwaani, anaonyesha ana mtaji mkubwa akianza na Kamusoko.

Wakati Kamusoko akiwa dimba la chini, Haruna Niyonzima anamrudisha ‘nyumbani’, namba nane. Kiungo cha ugavi, naye kwa kuonyesha furaha yake kuu, anaitendea haki nafasi hiyo. 
Anawazima mdomo tena wote waliokuwa wakilalamika eti anakaa sana na mpira, anaendelea kufanya yake tena kwa ufasaha akihusika na mabao yote matatu waliyopata Yanga.

JKT walikuwa vizuri, utaona waliwazuia Yanga katika kipindi cha kwanza licha ya kujifunga. Baada ya Lwandamina kuona kuna ugumu, hiki sasa ndiyo kilichonionyesha naye ana mambo yake, kama yakiendelea, makocha wajiandae.

Mabadiliko:
Wapenda soka wanaita sub, kifupi cha neno la Kiingereza substitution, yaani mabadiliko. Yale mabadiliko matatu aliyoyafanya Lwandamina, yanaonyesha ni mmoja wa makocha wajanja na wenye uwezo mkubwa wa kuusoma mchezo.
Baada ya Yanga kwenda na uongozi wa bao moja alilojifunga Michael Aidan wakati akijaribu kuokoa, kipindi cha pili, kiligeuka kuwa mali ya Yanga na wachezaji wangetulia wangeweza kufunga mabao mengi zaidi.


Amissi Tambwe (NJE), Juma Said (NDANI)-Dk ya 56:
Unaona kocha huyu alichokifanya, hautegemei kocha yeyote afanye katika wakati wa mwanzo wa kipindi cha pili. Anamtoa mfungaji bora wa msimu uliopita aliyekuwa anaongoza kwa mabao Yanga kwani alishafunga saba katika mechi 15 zilizopita.

Halafu anamuingiza kiungo mkabaji, Juma Said ‘Makapu’, kumbuka ndani yumo Kamusoko pia Niyonzima. Maana yake ametoa mshambuliaji, kaingiza kiungo. Katika hali ya kawaida unajiuliza, anakwenda kulinda katika dakika ya 56? Kama ni kweli ungekuwa ni wazimu. Jibu, hapana!

Lwandamina aliona unyumbulikaji wa Niyonzima, namna alivyo vizuri katika mchezo huo. Maana yake, Makapu anashuka chini, Kamusoko anapanda juu, Niyonzima anasogea juu kushoto lakini sasa anakuwa kama ‘free role’, mchezaji ambaye hana majukumu mengi ya kukaba badala yake kuchezesha timu.

Sub hii ilichangia Niyonzima kumiliki kiungo pale akisaidiana na Kamusoko ambaye tayari alisogea juu na hii inawafanya JKT wapunguze mashambulizi langoni mwa Yanga kwa kuwa wanatakiwa zaidi kulinda maana Niyonzima na Kamusoko, wamesogezwa mlangoni kwao. Hapa hakuna ubishi, ilikuwa ni lazima JKT wafungwe.



Thabani Kamusoko (NJE), Geofrey Mashiuya (NDANI)-Dk 85
Mabadiliko haya yanaonyesha yana maana mbili, kwanza ni kumpumzisha Kamusoko ambaye alianza namba sita akamalizia namba nane. Lakini kuzidi kuwabakiza JKT langoni kwao kwa kuwa Mwashiuya ana kasi, atawalazimisha kubaki chini. Hapa Yanga inakuwa inalinda ushindi wake.
Lakini kumbuka ni mabadiliko mengine dakika za mwisho, kiungo anatoka anaingia mshambuliaji. Huenda ulitarajia kuona anatoka mshambuliaji, anaingia kiungo kuongeza ulinzi. Hili ni somo jingine.

Donald Ngoma (NJE), Obey Chirwa (NDANI)-Dk 90
Haya ni mabadiliko ya kawaida kwa kuwa sub ipo na Yanga imepata uhakika wa ushindi lakini ni ujumbe kwa Chirwa aliyebaki mwishoni kabisa baada ya Yanga kutaka kumtoa kwa mkopo. Kwamba si sawa yeye kuingia muda huo, pia vizuri ajitahidi.
Lwandamina anaonyesha ni kocha mwenye uwezo mkubwa wa kucheza na saikolojia ya wachezaji na anajua afanye nini kwa maandalizi ya mechi ijayo akitumia mechi ya sasa. Ana mechi mbili za ligi Desemba hii, acha tuendelee kujifunza kuona “maujuzi” haya ni yake au ndiyo “aliotea” tu.

 KIKOSI:
Deogratius Munishi
Juma Abdul
Mwinyi Haji
Kelvin Yondani
Vincent Bossou
Thabani Kamusoko/ Mwashiuya Dk 85
Simon Msuva
Haruna Niyonzima
Donald Ngoma/ Obrey Chirwa Dk 90
Amissi Tambwe/ Said Juma Makapu Dk 56
Deus Kaseke

Sub
Ally Mustapha
Hassan Kessy
Obrey Chirwa
Vicent Andrew
Said Juma Makapu
Juma Mahadhi
Geofrey Mwashiuya

MECHI 2 ZIJAZO ZA YANGA:
DESEMBA 23   
Vs African Lyon       
DESEMBA 28   
Vs Ndanda FC 



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic