Na Saleh Ally
TANGU mwanzoni mwa miaka ya 2000 alipotua Yanga akitokea kwao Zanzibar, beki Nadir Haroub, maarufu kama Cannavaro, amekuwa msaada mkubwa katika kikosi cha Yanga.
Lakini katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara msimu huu, Cannavaro amepotea kwa kasi kubwa huku akionekana si beki mwenye nafasi tena ya kuitumikia Yanga kwa uhakika.
Cannavaro, nahodha wa Yanga, nahodha wa timu ya taifa ya Zanzibar na wa zamani wa Taifa Stars, anaonekana si mchezaji mwenye nafasi tena hata ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Yanga.
Kama utakuwa mfuatiliaji, unagundua Cannavaro alianza kuyumba mwishoni mwa msimu uliopita, kwani pamoja na Yanga kubeba ubingwa msimu wa pili mfululizo, yeye aliumia akiwa anaitumikia timu ya taifa katika mechi dhidi ya Algeria.
Wakati akiwa anauguza majeraha yake, kocha Charles Boniface Mkwasa alimtangaza Mbwana Samatta kuwa nahodha mpya wa kikosi chake, tena bila ya kufanya mawasiliano yoyote na Cannavaro ambaye alikuwa akiuguza majeraha aliyoyapata wakati akiitumikia Stars au akilitumikia taifa la Tanzania.
Baada ya uamuzi huo wa Mkwasa kwa kuwa Samatta alifanikiwa kuwa Mwanasoka Bora Afrika kwa wale wanaocheza nyumbani, beki huyo kisiki aliamua kujiondoa katika timu ya taifa, tena akilaumu, kudharauliwa, kuonewa na kutopewa heshima hata kidogo.
Hata alipoitwa katika kikosi cha Stars kwa mara nyingine, alitangaza kutokwenda na kusema hakuona kama angefanya hivyo. Kweli hakwenda na kama unakumbuka, Mkwasa alisema kuna wengi wa kuitumikia Stars, akafanya uchaguzi mwingine na mambo yakaendelea.
Unaweza kuanza kujiuliza, Kocha Hans van Der Pluijm alichukizwa na hilo, kwa kuwa Mkwasa ni rafiki yake, akaamua kutompa nafasi ya kutosha?
Je, Cannavaro mwenyewe, alijivuruga kisaikolojia wakati akilalamika kuhusiana na Mkwasa ambaye si walikutana Taifa Stars tu? Badala yake alikuwa kocha wake Yanga, pia ni mchezaji gwiji wa zamani wa Yanga?
Kulalamika sana, kulimponza Cannavaro na kujikuta akijiondoa mchezoni kisaikolojia na mwisho ameshindwa kurejea katika hali yake? Kuna mengi sana ya kujiuliza na huenda majibu yakawa na mgongano wa mambo mengi sana.
Ukweli, Cannavaro hawezi kuwa sawa na kama litakuwa ni suala la majeraha, linaweza kuwa na asilimia zake. Suala la umri pia linaweza kuwa na asilimia zake za mchango kuhusiana na hali yake ya sasa.
Bado unaweza kusema haitoshi, angalia mechi anazocheza Cannavaro, utaona hayuko katika kiwango bora kilichozoeleka na inawezekana kabisa hali ya kisaikolojia haijakaa vizuri. Tukubaliane, mwili unaongozwa na kichwa na inaonekana Cannavaro hayuko vizuri ‘kichwani’.
Kuna kila sababu ya Cannavaro kutengeneza kichwa chake kwa kuwa akiendelea hivyo, hakutakuwa na ujanja kwake zaidi ya kuomba kuandaliwa mechi ya kuagwa ili aondoke zake Yanga kwa heshima, ikiwezekana aende akacheze kwingine au kuendelea na mambo mengine kulingana na atakavyoamua.
Kisaikolojia Cannavaro hawezi kuwa vizuri. Huenda suala la kuondolewa unahodha kwa mfumo ambao hakupenda, tena na mtu kutoka Yanga, lilikuwa jambo lililomuumiza kichwa na wataalamu wa saikolojia wanasema “Etiology”.
Mtu anayefikia katika kiwango hicho huwa na maumivu ya kimawazo yanayosababisha ashindwe kufanya mambo fulanifulani kama alivyokuwa akifanya zamani.
Mwenyewe anakuwa hajui kama hivyo ni sahihi au la na huenda akawa anafikiria mambo mengine bila ya kujua aliumia kimawazo.
Anaweza kupona na kuondokana na “Etiology”, hali au dalili hizo za kuumwa, kwanza kwa kung’amua au kukubali kuna kitu kilimuumiza na anatakiwa kukifanyia kazi ili kukiondoa au kuondokana nacho. Kama asipofanya hivyo, maana yake atakuwa hajakubaliana nacho na kitaendelea kumuumiza na “kumuangamiza”, mwisho ataonekana ameshindwa kufanya kila alichoweza kwa ufasaha.
Kama Cannavaro ana maumivu ya suala la Mkwasa, au anaona kuna jambo hakulifurahia, sasa anataka kulikubali na kulimaliza. Kama tatizo la umri litakuwa linamkabili, lakini akiwa vizuri kisaikolojia, bado ataweza kujisimamia tena na kucheza vizuri kwa kuwa hauwezi kusema ndani ya miezi sita, Cannavaro ameisha sababu ya umri tu.
Kwangu Cannavaro ni kati ya mabeki bora kabisa waliowahi kutokea nchini na amefanya mengi mazuri ambayo hayapaswi kubezwa, mengi yatawezekana kama Cannavaro atakubali na kuamua kubadili mambo ingawa chaguo litabaki kuwa lake, kurejea au kukubali aandaliwe mechi ya kumuaga.








Kiswahili kigumu sana kuagwa au kuangwa?
ReplyDelete