January 20, 2017Mtanzania,Thomas Ulimwengu alikulia katika klabu ya AFC ya nchini Sweden ambako sasa ameamua kurejea na kucheza Ligi kuu ya nchini humo.

Habari za uhakika zinasema Ulimwengu amefikia makubaliano na AFC inayoshiriki ligi hiyo ya Sweden maarufu kama Allsvenskan.

“Kweli makubaliano yamekuwa mazuri na Jumapili (kesho) Ulimwengu anaweza kuwasili hapa na kujiunga na AFC. Nafikiri akija hapa litakuwa ni suala la kumalizana,” kilieleza chanzo cha uhakika kutoka Sweden.

Juhudi za kumpata meneja wake, Jamal Kisongo zilifanikiwa lakini hakutoa majibu ya moja kwa moja.

“Ulimwengu anaweza kwenda Sweden, anaweza kwenda Ubelgiji au kwingineko. Kikubwa nawaomba mvute subira na mambo yakikamilika, mtaelezwa,” alisema.

Taarifa nyingine kutoka Sweden zinaeleza, bilionea wa Kirusi aitwaye Alex anayeimiliki klabu hiyo ambaye ndiye alimuuza Ulimwengu TP Mazembe, ameahidi dau nono kwa mshambuliaji huyo tegemeo katika timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Kabla, Ulimwengu alikataa kuongeza mkataba na TP Mazembe baada ya kuisaidia kubeba ubingwa wa Afrika na kucheza Kombe la Dunia la klabu nchini Japan na Real Madrid ndiyo waliokuwa mabingwa.

Baada ya kusikia hajasajili TP Mazembe, klabu kubwa za Afrika zilianza kumsaka zikiwemo Orlando Pirates ya Afrika Kusini na Zamalek ya Misri. Hata hivyo, msimamo wake ulikuwa ni kwenda Ulaya.

Pia, Oostende na KRC Genk anayochezea Mbwana Samatta nazo zilionyesha nia ya kutaka kumpata ingawa mwishoni zilionekana kusuasua hadi AFC ilipojitokeza na kutaka kumaliza dili.

Ulimwengu alitua AFC baada ya mipango ya wakala wa kuuza wachezajia anayetambuliwa na Fifa wakati huo, Damas Ndumbaro kukamilika na kuishawishi klabu hiyo kumnunua.

Baadaye AFC ilimpeleka Hamburg ya Ujerumani kufanya majaribio, lakini hakufanikiwa na kurejea Sweden kabla ya kuamua kumuuza TP Mazembe ya nchini DR Congo.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV