January 25, 2017Beki tegemeo wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani amepata nafuu ya majeraha ya uvimbe wa kidole chake na juzi Jumatatu alianza mazoezi mepesi pamoja na Nadir Haroub 'Cannavaro'.

Yondani aliukosa mchezo wa Kombe la FA wakati timu hiyo ilipovaana na Ashanti United kutokana na majeraha aliyoyapata wakati Yanga ilipocheza na Majimaji ya Songea na kushinda bao 1-0, likifungwa na Deus Kaseke.

Kukosekana kwa beki huyo, Kocha Mkuu wa Yanga Mzambia, George Lwandamina alilazimika kumtumia beki wa pembeni, Oscar Joshua kucheza nafasi hiyo ya Yondani.Daktari Edward Bavu amesema beki huyo anaendelea vizuri baada ya kupata matibabu ya haraka kuhakikisha anakuwepo uwanjani mechi ijayo ya ligi kuu dhidi ya Mwadui.


Bavu alisema, beki huyo ameanza mazoezi mepesi ya binafsi tangu juzi (Jumatatu) jioni na jana asubuhi alifanya mazoezi magumu pamoja na wenzake.


"Katika kikosi changu, mchezaji ambaye bado majeruhi ni Ngoma (Donald), pekee ambaye yeye anaendelea na program maalum chini ya uangalizi wangu na daktari anayemtibia goti lake.

"Lakini hao wachezaji wengine kama akina Chirwa (Obrey), Zulu (Justine) wamepona na wameanza mazoezi pamoja na Yondani,"alisema Bavu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV