January 21, 2017



Kikosi cha Yanga jana Ijumaa kilifanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar kabla ya leo hakijavaana na Ashanti United, lakini kimeonekana kushituka baada ya kufanya mazoezi maalum ya upigaji penalti ambazo zimekuwa kama ugonjwa kwao.

Leo Jumamosi kwenye uwanja huo, Yanga itapambana na Ashanti kwenye mchezo wa Kombe la FA raundi ya tano ambapo dakika tisini zikimalizika kwa sare, basi mshindi ataamuliwa kwa mikwaju ya penalti.

Kwa muda mrefu, Yanga imekuwa ikishindwa kila ikifika kwenye hatua ya penalti kwani hata hivi karibuni iliondoshwa katika michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kufungwa penalti 4-2 na Simba.

Katika mazoezi hayo, Kocha mkuu wa Yanga, George Lwandamina alikuwa kiwapa vijana wake zoezi hilo maalum ikiwa ni kama tahadhari ya mchezo wa leo kwani lolote linaweza kutokea.

Mbali na hilo, leo Yanga inatarajiwa kukosa huduma ya nyota wake watano ambao wana udhuru mbalimbali. Nyota hao ni Kelvin Yondani anayesumbuliwa na uvimbe kidoleni, Haruna Niyonzima (ana msiba), Hassan Kessy (anaumwa typhoid), Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (anaumwa malaria) na Deogratius Munish ‘Dida’ aliyepewa ruhusa maalum.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi akizugumzia mchezo huo alisema; “Ni ngumu ndani ya kipindi kifupi hiki kuandaa timu vizuri, ratiba imetoka jana (juzi) kwa mechi ya kesho (leo), kwa kweli hatujapata muda wa kuwasoma wapinzani wetu.

“Lakini tutaingiza timu na kucheza kama mamlaka zinavyotaka ila utaratibu uliotumika haukuwa sawa, kuhusu majeruhi ni kweli wapo wengi lakini tuna kikosi kipana kitakachoweza kupambana.”


Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuwa; Beno Kakolanya, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Oscar Joshua, Andrew Vincent ‘Dante’, Said Makapu, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Juma Mahadhi, Amissi Tambwe na Deus Kaseke.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic