February 20, 2017



Na Saleh Ally
HAKUNA timu wanayolaumiana sasa kama Arsenal, hii ni bila ya kujali ni England, Tanzania au kwingineko.

Kila mmoja anataka Kocha Mkuu, Arsene Wenger atupiwe virago au afunge mwenyewe na kuondoka zake!

Kila shabiki wa Arsenal sasa analaumu na hii inaonekana imeamshwa na kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa Bayern Munich katika mechi ya kwanza ya hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hakuna anayeamini Arsenal inaweza kupindua mambo na kuiangusha Bayern kwa kuichapa mabao 4-0, halafu isonge mbele. Kiwango cha machungu kwa mashabiki wa Arsenal, kiko juu.


Kunaweza kuwa na mambo mengi sana ndani ya kikosi cha Arsenal na Wenger ambaye imeelezwa amekubali kuondoka mwishoni mwa msimu akawa ni sehemu tu lakini tatizo likawa kubwa zaidi.

Moja ya sababu zinazoonekana kuisumbua Arsenal ni uongozi wa ndani ya uwanja. Si timu tena yenye watu ambao wakati mwingine kwa misemo ya wapendo soka huitwa “Baba Mwenye Nyumba.” Mfano mzuri kama ukirudisha hapa nyumbani, kama unamkumbuka Juma Kaseja wakati akiwa Simba.

England kuna mifano miwili mzuri ya kuikumbushia. Wakati Arsenal nahodha akiwa Patrick Vieira, Manchester United alikuwa Roy Keane.

 Bado timu hizo zilikuwa na watu wa shoka kila upande ambao walirithishwa. Thierry Henry akarithi kwa Vieira na urithi wa Keane ukasogea taratibu kutoka juu, ikafika hadi kwa Gary Neville na baadaye Rio Ferdinand na mambo yakaendelea kwa mafanikio.



Katika kikosi cha sasa cha Man United, angalia hamasa imerejea. Kuna mtu ndani ya uwanja anaweza kutoa uamuzi, akaamrisha, akasisitiza na hata kufoka na watu wakamsikiliza.

Zlatan Ibrahimovic si nahodha, lakini jiulize mchezaji gani wa Man United sasa anaweza kubisha atakachosema? Kila mara ukimuangalia utafikiri ni “Mkubwa na wanawe”.

Zlatan ni mtu wa makombe, amechukua makombe pia ubingwa wa ligi kuu maarufu kama Eredivisie alipotua Ajax ya Uholanzi akitokea kwao Sweden. Alipohamia Italia, timu zote tatu, Juventus, Inter Milan na baadaye AC Milan, zote amebeba nazo ubingwa wa Serie A. Alipotua Ufaransa, misimu minne akachukua ubingwa wa League 1.

Zlatan ni mtu wa makombe, anayetaka kushinda na hajawahi kushiriki ligi ya nchi bila makombe. Miaka 35 sasa, lakini ana hamu ya mafanikio kama ana miaka 20 tu.

Kocha anapokuwa nje ya uwanja, wakati mwingine hawezi kufikisha kila kitu haraka kama ambavyo mchezaji anayeaminika au kuheshimiwa katikati ya uwanja.

Zlatan ana uwezo wa kumkataza Anthony Martial kufanya utoto, ana uwezo wa kumpongeza na kumuongezea jambo la haraka kuliko inavyokuwa kwa kocha.

Arsenal hawana Zlatan wao, si kikosi ambacho kuna mchezaji anayehofiwa na wenzake hadi ikafikia wakamheshimu na kumsikiliza nini anaagiza.

Wachezaji wa Arsenal kwa sasa, kila mmoja ni mkubwa na hata wale nyota wanazidiwa nguvu na wazawa. Mfano, Mesut Ozil au Alexis Sanchez hawezi kuwa na sauti ya juu dhidi ya Theo Walcott.

Mkumbuke nahodha Tony Adams na ndani yake alikuwepo Martin Keown ambaye hakuwa nahodha lakini asingeruhusu utani.

Chelsea imekwenda inatoboa tu, ndani yake unaona John Terry akiwa hataki utani hata kidogo. Sasa yuko nje kwa kuwa hachezi mechi nyingi, bado anaendelea kuwa msaada na kuwarithisha watu jambo.

Kumbuka AC Milan na Paul Maldini ndani kukiwa na Genaro Gatuso lakini Juventus chini ya Alesandro Del Piero au Barcelona yenye Xavi Hernandez, naamini utanielewa.

Wenger kuna sehemu anakosea, lakini msaada wa kiongozi sahihi ndani ya uwanja ungeweza kuipatia Arsenal ahueni kuliko ilivyo sasa.

Unaona wanapofungwa, wanachanganyikiwa zaidi. Hakuna wa kusema wengine wakamfuata hata neno “tulieni”, endeleeni kupambana.


Kila mmoja ana sauti, kila mmoja anamlaumu mwenzake na kila mwingine si kosa lake. Kamwe hakuwezi kuwa na mwendo sahihi na Arsenal kama watamuondoa Wenger, basi wasisahau kutafuta kiongozi wa uwanjani aina ya Zlatan.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic