February 20, 2017

Na Saleh Ally
NIMEANDIKA mambo mengi sana kuhusiana na suala la mpira katika Mkoa wa Tanga, sidhani kama kuna ambacho nilisema na hakijawahi kujirudia au kudhihirika hadharani.

Kama umewahi kusoma miaka zaidi ya mitano iliyopita nilieleza namna ambavyo kuna nidhamu mbovu ya mashabiki na hata viongozi wa timu wakati huo nikiitolea mfano Coastal Union hasa kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Nilishangazwa na fujo karibu katika kila mechi kubwa, mashabiki kuamini kufanya vurugu ni ujanja. Wako wanaotaka kuonekana mbele ya wenzao ni watu wenye jazba sana. Nilieleza huo ni upuuzi ulionishangaza mara kadhaa.

Uliendelea kutokea, tumeona fujo mfululizo hadi vyombo vya michezo, kisheria na hata Jeshi la Polisi lilikemea kuhusiana na suala hilo.

Kama unakumbuka tumeona waamuzi wanapigwa kama wezi katika mechi ya Ligi Kuu Bara lakini mambo yanakwenda kama mechi za mchangani. Mashabiki wanaingia kumpiga mwamuzi na baadaye kuharibu vitendea kazi kama ubao wa kubadilishia wachezaji ambao Tanga upo mmoja tu! Ubao ulichezesha vibaya?

Nilieleza namna watu wa Tanga wasivyopendana hasa katika soka, wanayoishi kwa vikundi wenye umahiri wa majungu na nikasisitiza ni vigumu sana hata timu tatu walizokuwa nazo ligi kuu kudumu. Mwisho wa msimu, Coastal Union, African Sports ambazo ni kongwe na Mgambo iliyokuwa imekaa kwa muda katika ligi hiyo, zote zikaporomoka daraja hadi la kwanza.

Zikiwa daraja la kwanza, viongozi wa chama cha mkoa wakawa wanaeleza namna ambavyo wamejipanga kushirikiana kuzirejesha. Niliendelea kushangazwa kuwa vipi timu tatu hata moja haikubaki, sasa wanazungumzia kuzirudisha zote!

Nilieleza namna ambavyo itakuwa vigumu kwao hata kuirudisha timu moja tu. Kwa kuwa nimejifunza, watu wa Tanga mmoja akiwa hana nguvu angependa na wengine wasiwe nayo na kama kufeli, basi wafeli wote.

Juzi jioni, nimemsikia mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa Tanga (TRFA), akijisifia angalau kuzibakiza Coastal Union na Mgambo Shooting katika Ligi Daraja la Kwanza. Hii ni baada ya African Sports kuporomoka hadi daraja la pili. Haya ni maajabu na mshangao usiokuwa na mfano.

Tanga waliokuwa na timu kubwa, zilizowahi kubeba ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Muungano kisha zikawa vigogo. Vipi wanajisifia kubaki Ligi Daraja la Kwanza?

Waliahidi kuzirejesha zote, vipi wameshindwa hata moja na mbaya zaidi moja imeporomoka hadi daraja la pili. Watu wa Tanga bado hawajifunzi au wanaamini wakiambiwa wanaonewa au kusakamwa ndiyo maana wanashindwa kubadilika na kujisaidia?

Hawa watu wana laana ya kutokubali makosa yao, wanaendekeza majungu, kila mmoja anamsema mwenzake. Wengine ni maarufu kwa kujipendekeza, kazi yao kuwapiga majungu wengine wachukiwe na wengine wameunda makundi ya kuwakataa wengine na kuwatenga.

Coastal Union ni makundi, African Sports hali kadhalika na sasa wanaipa wakati mgumu hata Mgambo ambayo ilikuwa na heshima za kijeshi na kuifanya ibaki ligi kuu kwa muda mrefu.

Timu za Tanga ziliondoka Ligi Kuu Bara kwa zaidi ya miaka 10. Ziliporudi hazikukaa hata misimu mitano. Hii inaonyesha kuna tatizo na wao lazima wakubali kubadilika.

Hakuna mafanikio ya mmoja tu. Lazima muungane na kukubali kwamba mnakwenda na mawazo ya kizamani, nikiwa na maana yaleyale na mbaya zaidi, hamjui mnaiangamiza Tanga yenye vipaji lukuki.

Vijana wengi wanawategemea viongozi. Lakini wengi wenu si mfano, majungu yamesababisha makundi na hata walio na nia ya kusaidia kwao Tanga wamekuwa wakishindwa kwa hofu ya kuingia kwenye majungu kama mlivyo.


Badilikeni, kwa jinsi hali ilivyo na mnavyokwenda, hali inaonyesha dunia inawaacha na mwisho mtaanza kujisifia kwa kubakisha timu daraja la pili!

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV