Beki wa kati wa Simba, Method Mwanjale ameshusha presha katika kikosi cha timu yake kwani leo Jumamosi anatarajiwa kuanza mazoezi mepesi kwa ajili ya kujiandaa na mechi dhidi ya Yanga.
Simba na Yanga zinatarajiwa kuvaana Jumamosi ijayo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Beki huyo ambaye ameikosa mechi ya Kombe la FA dhidi ya African Lyon, anaanza mazoezi hayo baada ya kupona majeraha ya enka aliyoyapata kwenye mechi iliyopita ya ligi kuu dhidi ya Prisons ambapo Simba ilishinda mabao 3-0.
Akizungumza jijini Dar, Daktari wa Simba, Yassin Gembe alisema beki huyo ataanza mazoezi baada ya kupona majeraha hayo yaliyomuweka nje ya uwanja kwa wiki moja.
Gembe alisema, beki huyo kabla ya kuanza mazoezi hayo, alikuwa ana program maalum ya gym huku akiendelea na matibabu hayo ili kuhakikisha anapona kwa haraka kwa ajili ya kurejea uwanjani.
“Habari njema kwa mashabiki wa Simba ni kuwa Mwanjale amepona majeraha ya enka yaliyokuwa yamemuweka nje ya uwanja kwa muda wa wiki moja sasa.
“Hivyo, Jumamosi (leo) ataanza mazoezi mepesi binafsi tukiwa kambini Zanzibar tutakapokwenda kuweka kambi ya kujiandaa na mechi dhidi ya Yanga.
“Uwezekano wa kucheza au kutocheza bado haijajulikana kwani ndiyo kwanza atakuwa anaanza mazoezi, hivyo tusubirie kwanza kwani majeraha aliyoyapata siyo makubwa sana,” alisema Gembe.
0 COMMENTS:
Post a Comment