February 24, 2017Na Saleh Ally
HIVI karibuni nililizungumzia suala la vita ya madawa ya kulevya ambayo inaongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.


Nilieleza namna ambavyo ninaiunga mkono vita hiyo kwa kuwa ni ukweli Watanzania wengi wanaathirika na inaathiri nguvu kazi ya taifa letu kwa kuwa wanaoathirika wengi ni vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa.


Pamoja na kuiunga mkono vita hiyo, nilieleza kiasi gani ninapishana na Makonda kwa namna alivyokuwa akitumia njia ya kuwataja watuhumiwa hadharani ambalo halikuwa jambo sahihi kwa haki za wanadamu ambao wana familia zao pia watu wao.


Nilieleza haikuwa sahihi na siku chache baadaye, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwaagiza wakuu wa wilaya na mikoa kutowatangaza watu kabla ya uchunguzi wa kutosha kufanyika. Leo nasisitiza tena, haikuwa sahihi na wala si sahihi hata kidogo.


Vita dhidi ya madawa ya kulevya, haizuii kufuatwa kwa sheria za nchi wala haimpi nafasi mtu kuwa juu ya sheria.


Leo ninataka kuzungumzia ule ubao wa matangazo ulio ndani ya Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambao mara nyingi umekuwa hautumiki na inaonekana hauna faida kubwa kama kweli wahusika wangekuwa wakiutumia hasa.


Mimi ninaamini kama nilivyoeleza siku chache zilizopita kuwa vita ya madawa ya kulevya haiwezi kumalizwa na nguvu pekee badala yake kuna sehemu zinahitaji ufundi, au utaalamu wa kisaikolojia.


Kuutumia ubao huo mbele ya mashabiki takribani 60,000 wanaojitokeza kushuhudia mechi ya watani Simba na Yanga. Si kazi lahisi kuikusanya idadi kubwa ya watu kama hiyo kwa wakati mmoja.


Hata kama watapungua na kuwa 45,000 bado wanaweza kuwa wajumbe wazuri kama kutakuwa na picha kabla ya mechi kuanza, mapumziko na ikiwezekana mara tu baada ya kwisha.


Wanachotakiwa ni kuelezwa mambo mbalimbali kama madhara ya madawa ya kulevya kwa vijana, wanavyoumia, yanavyosababisha ushoga, yanavyosababisha umasikini na kadhalika.


Hata kama kutakuwa na mtaalamu atakayezungumza kwa dakika tano au 10, au mtu aliyewahi kuathirika na madawa akapewa nafasi hiyo kwa kurekodiwa na kuonyeshwa kwenye runinga hiyo ya uwanjani. Ujumbe utakuwa umefika sehemu kubwa.


Nyota wa soka au wasanii pia wanaweza kutumika kuwafikishia ujumbe watu walio uwanjani hapo kiutalaamu bila ya kuwabugudhi na wao wakitoka pale, hata kama watu 20,000 watakuwa wamekubali kuwa mabalozi wazuri wa kusambaza ujumbe kuhusiana na ubaya wa madawa ya kulevya, utakuwa ni msaada mkubwa sana.


Sehemu nzuri ya kufikisha ujumbe ni sehemu yenye mikusanyiko ya watu hasa wanapokuwa pamoja kwa idadi kubwa. Mchezo wa soka una uwezo wa kukutanisha watu wengi kwa wakati mmoja.


Uzuri wa bango hilo, hata wakati wa runinga inayorusha moja kwa moja. Pia inaweza kulionyesha nini kinaendelea nab ado ikawa ni sehemu nzuri ya usambazaji wa ujumbe ambao unakuwa faida kwa taifa.


Lazima ubao huo uwe unatumika. Hata kama mtu hajahutubia, basi kuwa na matangazo kutoka serikali kuhusiana na madawa ya kulevya, kupinga uhalifu, kukata mambo yasiyofaa na kadhalika.


Najua umekuwa ukitumika kuwatahadharisha watu kuepuka masuala kadhaa yaliyo na tija kwa taifa letu.


Mchezo wa soka una mashabiki wanaopatikana katika Nyanja zote za jamii yetu. Ni jambo zuri sana kupata mabadliko waliopo katika kila shemeu kwa maana ya watu wa kawaida, wafanyabishara, madaktari, askari polisi, waandishi na kadhalika.

Ninaamini itafikia siku ombi langu litafanyiwa kazi kwa lengo la kulisaidia taifa letu.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV