March 27, 2017Na Saleh Ally
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ameanza kazi moja kwa moja akiingia katika kamati ya Saidia Serengeti Boys ambalo linaonekana ni jambo zuri kabisa.

Kamati hiyo inataka hali ya uharakishaji wa mambo kwa kuwa siku zinasonga mbele kwa haraka na timu hiyo inataka maandalizi ya kutosha kabla ya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika huko Gabon, Mei, mwaka huu.

Moja ya kitu kikubwa kabisa kwa Serengeti Boys ni kucheza Kombe la Dunia. Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alianzisha kamati hiyo akijua umuhimu katika hilo na Dk Mwakyembe ameingia na mara moja ameonyesha si mtu wa kusubiri.

Dk Mwakyembe ndiye kiongozi wetu tunayepaswa kumuunga mkono na itakuwa vizuri sana kukumbuka maneno ya Nape kwa Tanzania ni kubwa sana na tunapaswa kumpa sapoti Dk Mwakyembe katika majukumu yake. Hili ni muhimu sana.

Kwa upande wa Championi tumeonyesha mfano mkubwa ikiwa ni pamoja na kutoa matangazo yanayohimiza kuichangia Serengeti Boys ili kufanikisha lengo.

Lazima tukumbuke, pamoja na kulenga kuiona inafanya vizuri katika michuano ya Gabon, kama ikiingia nusu fainali basi itajihakikishia kucheza Kombe la Dunia, hili si jambo dogo.

Kumuunga mkono Dk Mwakyembe, itakuwa ni msaada kwa ajili ya Serengeti Boys ambayo ikifanya vizuri ni basi ni faida zaidi ya maradufu kwa taifa letu.

Haya ni mambo ya kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ingawa ningependa kumkumbusha Dk Mwakyembe kwamba huku kuna Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambao hapaswi kuamini ni watu bora au wasafi sana.

Kwa kuwa wakati Dk Mwakyembe anaingia moja kwa moja amepitiliza na kuanza na kazi na kamati ya Serengeti Boys, watu wa kwanza kabisa kushirikiana nao wanakuwa ni TFF kwa kuwa ndiyo wasimamizi wa timu zetu za taifa.

TFF wamekuwa na madudu mengi ambayo yamesababisha leo hii hata hiyo timu ya taifa inalazimika kuchangiwa kwa kuwa wadhamini hawana imani na kuingiza fedha zao ndani ya shirikisho hilo.

Hata wale waliowahi kuingiza fedha zao, wengi wamezitoa na wachache wamebaki. Walioondoka ni kutokana na kuona mambo hayaendi kwa utaratibu sahihi na wako waliolalamika kuhusiana na matumizi ya hovyo.

Tunajua ubovu wa uendeshaji wa ligi uliojaa uswahiba, ushabiki na kutofuata weledi ambayo yamesababisha mpira wa Tanzania kudorora kupita kiasi na sasa kuwa chini ya 150 katika viwango vya  Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) lenye wanachama 205.

Tanzania iko kwenye anga za Djibouti, Eritrea na Somalia au Shelisheli karibu na walipo akina Comoro. Nchi kama Uganda na Kenya, ziko mbali kwa zaidi ya namba 50 au zaidi tulipo sisi.

Ukiangalia TFF chini ya Jamal Malinzi ndiyo iliyotuporomosha zaidi na ikaanza kuchangamka mwishoni kwa kuwa uchaguzi wa TFF unakaribia. Utaona zilianzishwa ligi za wanawake na watoto ili kuziingiza kwenye rekodi, lakini mambo yake yalikuwa zimamoto na wagonjwa wakabebwa kwenye gari la faya. Mwisho tulimpoteza kijana mmoja wa Mbao FC, Mwenyezi Mungu amrehemu.

Dk Mwakyembe, TFF nalo ni jibu, hivyo ukaribu wa kamati wasikusahaulishe kushughulikia mambo muhimu yatakayosaidia kuikwamua Tanzania ilipo sasa.

Yako mazuri machache waliyoyafanya, ninaamini wanapaswa kuungwa mkono kwa kuwa ukweli haujifichi. Mfano, leo wanaungwa mkono katika hilo la Serengeti Boys ambalo pekee wanaweza kujivunia kwa kuwa walikubali kumrudisha Kim Poulsen ambaye walimlipa mamilioni kumuondoa kwa kuwa aliletwa na Leodegar Tenga.

Karibu sana Dk Mwakyembe, lakini usisite wala kulainika, madudu ya TFF yametukwamisha sana, tafadhali, usiyasahau.
0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV