Baada ya kupona kwa mastraika wa Yanga, Donald Ngoma na kiungo Thabani Kamusoko, straika raia wa Burundi, Amissi Tambwe, ameibuka na kusema wapinzani wao Simba wasitarajie Yanga itapoteza mchezo wowote tena hadi wanachukua ubingwa.
Ngoma na Tambwe kwa nyakati tofauti walikuwa nje ya kikosi hicho kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya goti lakini kwa sasa wamepona na Jumamosi iliyopita Ngoma na Kamusoko, walidhihirisha hilo kwa kucheza katika mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya MC Alger ya Algeria.
Tambwe amesema kuwa uwepo wa nyota hao utawafanya wazidi kupambana na Simba kwenye mbio za ubingwa na hatimaye kuwapiku na kuwa mabingwa hata kwa tofauti ya mabao kama watalingana pointi.
Tambwe amesema tangu amewaona Kamusoko na Ngoma wameanza kucheza wikiendi iliyopita, hakika amepata nguvu ya kufanya vizuri zaidi ya hapo na kwamba kama hakitatokea kikwazo kingine basi Simba wao wajaribu kuelekeza nguvu mahali pengine tu kwani suala la ubingwa litakuwa gumu sana kwao.
“Najua wenzetu wapo mbele kwa tofauti ya pointi mbili baada ya kuifunga Mbao FC, juzi lakini naomba wajue tu kuwa kupona kwa Ngoma na mimi huku Kamusoko naye akiwa fiti, hii ni chachu kubwa ndani ya safu yetu ya ushambuliaji ambayo utaona kila mmoja atakuwa amepata nafasi kubwa ya kucheza na kufunga kwani sisi kila mmoja ana uwezo wa kumtafutia mwenzake na kufunga mwenyewe.
“Simba wasitegemee ubingwa kama sisi tupo hata kama wamekuwa na kasi nzuri, lakini wajue kuwa tutapambana hadi mwisho,” alisema Tambwe.
SOURCE: CHAMPIONI
Aache ujinga wake
ReplyDelete