April 23, 2017Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limetangaza kuipoka Simba pointi tatu na mabao matatu ambazo ilipewa kutokana na mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar.

Wiki mbili zilizopita Simba ilipoteza mchezo dhidi ya Kagera kwa kufungwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera katika Ligi Kuu ya Bara lakini baadaye ilikata rufaa ikipinga Kagera kumtumia mchezaji Mohamed Fakhi ikidai alikuwa na kadi tatu za njano, ndipo ikapewa ushindi huo kupitia Kamati ya Saa 71.

Mara baada ya kamati hiyo kuipa Simba pointi Kagera ikaomba kupitiwa upya kwa suala hilo na ndipo TFF ikatangaza kuwa suala hilo sasa litakuwa chini ya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF ambayo ndiyo imetoa maamuzi hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari juu ya uamuzi huo, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa amesema kuwa kuna sababu kadhaa zimechangia kuchukuliwa kwa maamuzi hayo ambapo alizitaja kuwa ni:

“Malalamiko ya Simba hayakuwasilishwa kwa wakati muafaka tangu mchezo ulipochezwa, malalamiko yao hayakuwa katika njia ya maandishi, rufaa ya Simba haikulipiwa ada, kikao cha Kamati ya Saa 72 kilikosa uhalali kutokana na kuwashirikisha watu ambao hawana uhalali wa kuwa kwenye kikao.

“Kutokana na sababu hizo kamati imeamua kutengua maamuzi yaliyochukuliwa na Kamati ya Saa 72 na kurejesha matokeo kama yalivyokuwa, pia kamati imemuagiza katibu mkuu wa TFF kuwapeleka baadhi ya wajumbe wa bodi ya ligi katika Kamati ya Maadili ya TFF kwa kosa la kwenda kinyume na kazi zao,” alisema Mwesigwa.

2 COMMENTS:

 1. Soka la bongo kweli ni kizungumkuti, sasa ikiwa sababu ni kama zilizovyorodheshwa kwamba malalamiko ya simba dhidi ya Kagera hayakuwasilishwa kwa wakati muwafak tangu mchezo ulipochezwa,malalamiko yao hayakuwa katika njia ya maandishi n.k

  Ikiwa hizi ndio miongoni mwa sababu sasa kulikuwa na haja gani kuwasumbua watu kuja kutoa ushahidi kama mchezaji ana kadi tatu au hana?

  Kulikuwa na haja gani ya kupoteza muda juu ya kutoa maamuzi takriban wiki mbili sasa watu wanasubir maamuzi

  Hapa katika hili kuna figisu figisu za Usimba na Uyanga.

  ReplyDelete
 2. Aaaaaah basi bwana bora Simba wajipange wachukue ubingwa wa Uwanjani wa mezani ni mgumu sana.

  ReplyDelete

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV