Na Saleh Ally
NATAKA niendelee kuwa mkweli kwa kuwaambia hakuna jambo la kipuuzi linaloendelea mbele yetu kama hili la kadi tatu za beki Mohammed Fakhi.
Wote tumeliacha liendelee, ushabiki umetuzidi nguvu na kila mmoja anazungumza kama shabiki. Hata walioamua kuwa wakweli, wanavishwa ushabiki kwa kuwa wasikilizaji wanayapokea mambo kishabiki.
Angalia namna suala la uhakika wa beki Fakhi kama alikuwa na kadi tatu za njano au la linavyokuwa na mzunguko mkubwa.
Kawaida kunakuwa na wakusanya ripoti za kila mchezo, hawa ni waamuzi na makamishna. Halafu wanazipeleka kwa wahifadhi rekodi ambao ni Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Sasa ni ajabu kabisa kama utasikia hata Bodi ya Ligi haina uhakika na kadi za mchezaji, TFF pia haina uhakika.
Ajabu kabisa, waamuzi nao wanatumia udhaifu huo kupitia ushabiki wao kuingia kwenye mzozo, mmoja akisema kulikuwa na kadi na mwingine anasema hakukuwa na kadi.
Hapa suala linakuwa si kadi tena, badala yake ni kuwachanganya Watanzania na kuonyesha hakika tumefeli kwa kuwa hata wanaotuongoza na tunaowategemea wapambane kuukuza mpira wamefeli.
Kumekuwa na taarifa za chinichini kwamba ripoti zilichezewa na inawezekana kadi haikuwepo. Kama ni kweli, ripoti haziwezi kuchezewa bila wahusika kwenye bodi. Kama ni hivyo, watajwe, wafikishwe kwenye vyombo vya sheria na hili lifanyiwe kazi kisheria.
TFF na bodi ya ligi lazima watakuwa wanahusika katika kadi, iwe ilikuwepo au la. Mkanganyiko huu ungemalizwa na wao lakini kwa kuwa hawakuwa na mpangilio katika mambo yao kwa ufasaha, shida inaanzia hapo.
Kumbukumbu zao ndiyo maana waliopo wanakuwa na uwezo wa uamuzi wa kuzichezea. Mfano walio na kadi kusema hawakuwanayo au wasiokuwanayo kusema ipo. Huu mwanya unatokana na uzembe wa TFF, ndiyo maana nafasi kwa wanaotaka kuharibu inakuwepo.
Lakini yote, angalia kuhusiana na Mwenyekiti wa Soka Mkoa wa Kagera, Jamal Malinzi ambaye timu anayoiongoza kutoka mkoani mwaka inapambana na Simba “mezani” kurejesha pointi zake.
Kagera ambayo mwamuzi wa akiba alitokea Kagera, alikwenda kuitetea kuhusiana na kadi hiyo lakini Malinzi ni kiongozi wa soka mkoani Kagera ambaye bila shaka angefurahi kuona timu ya mkoani kwake inashinda kama ambavyo alifurahia kuona nyasi bandia zinabandikwa Bukoba na si kwingine.
Ana haki ya kuitetea timu kutoka mkoani mwake kwa kuwa yeye ni mwenyekiti na ndiye msimamizi wa maendeleo na haki kwa soka mkoani kwake.
Yeye ndiye aliyeteua zile kamati ambazo zinaamua kutoa au kuchukua pointi au kutoa adhabu kwa timu au kwa mchezaji. Kamati ambazo zikikaa wajumbe wanapata posho zao safi na nyingi kabisa.
Malinzi huyohuyo, ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo sasa, ndani yake na walalamikaji wengine Simba wapo.
Hawa hawatokei mkoani mwake, wanatokea Dar es Salaam ambako yako makao makuu ya TFF. Malinzi ni binadamu, hili lazima tukubali.
Ndiyo maana, wakati fulani mimi nilipinga Malinzi kuwa mwenyekiti wa Kagera na pia ya Rais wa TFF. Nilieleza linavyoweza kuleta mkanganyiko siku moja.
Utaona kunakusuasua hapa. Maana kuna taarifa Simba wamepokonywa pointi walizozipata kutoka kwa Kagera. TFF inatafuta “timing” kama ile ya kumvizia kobe ili kutangaza.
Tena imeelezwa kwamba wanataka kutangaza kupitia kamati kwa kuwa hawataki kuonekana wanahusika. Jambo ambalo ni baya kabisa. Wana sababu gani ya kukimbia, maana yake wanajua kuna tatizo na sasa Malinzi atakuwa akiliona tatizo nililowahi kumueleza na kusisitiza ni kosa yeye kuwa mwenyekiti wa Kagera na Rais wa TFF.
Inawezekana kabisa haki ni ya Simba, lakini Malinzi na watu wake watakuwa hawajiamini kwa kuwa wanaona hawawatendei haki watu wa Kagera kwa kuwa yeye ndiye mwenyekiti wa soka na anapaswa kuwatetea.
Kumbuka Kagera nao wanahitaji nafasi ya nne ambayo ina nafasi kwenye Ligi Kuu Bara na ukweli haufichiki kuwa walishinda uwanjani ambalo ni jambo zuri, lakini kanuni ndiyo zinazowabana kama kweli kadi tatu za njano zipo tatu.
Pia inawezekana kabisa haki ikawa ni ya Kagera, inawezekana hakukuwa na hizo kadi. Bado Malinzi atakuwa hana uhakika au hatatulia kwa hofu ya kuonekana hajatenda haki na Simba wengi hawataamini tu. Hii si sawa, ndiyo maana nasisitiza kuwa mwenyekiti wa mkoa na rais wa shirikisho ni kituko.
Kuna taarifa nyingi lakini safari hii lazima tuone kama kuna ukweli watu wafikishwe kwenye vyombo vya sheria. Maana inaelezwa kuna rekodi zilichezewa, kama hilo ni kweli basi TFF ya Malinzi na bodi ya ligi wanapaswa kuwajibika.
Hata kama anataka kura wakati wa uchaguzi kwa kuwa ataweza kujipigia, bado Malinzi anapaswa kubadilika na kuwa mtu anayejifunza kwamba anakosea kung’ang’ania madaraka na haitakuwa sawa kwa maendeleo ya mpira na hili tatizo la kadi tatu za Fakhi, liwe shule kubwa kwake.
Kuhusu rekodi kwamba zilichezewa, kama hili nalo lipo kweli, basi TFF iwajibike moja kwa moja kwa kuwa bodi ya ligi, waamuzi ndiyo watu wao.
Baada ya hapo kuna haja ya kuzuia mijadala ya pointi za mezani na hii ya kama kadi ipo au haipo kwa kuwa na kitengo bora na sahihi cha ukusanyaji wa takwimu.
TFF na bodi ya ligi watafute wataalamu ili timu ziache kutafutana kwenye makosa. Kuwe na taarifa ya kadi za wachezaji kila wakati wa “pre match meeting” ambavyo ni vikao hufanyika kabla ya mechi.
Kukiwa na utaalamu wa uhakika, hivi habari za nani ana kadi tatu kacheza hazitakuwepo na mpira wetu utakuwa umepiga hatua. Hivi mwisho itakuwa vilio vinavyozidisha kutoaminiana na kama hamuaminiani, ni vigumu kuungana na kusukuma maendeleo mbele.
Najua wengi mnafaidika na migogoro ya mpira lakini ukweli, imetuchosha na sasa tunataka maendeleo. Hamuwezi, muondoke na kuwaachia wenye nia njema.
ww umeshajiandaa kuchukua fomu ya kugombea urais TFF? kama unaujua ukweli uweke wazi na kukosoa uongo. manneno mengi hayana tija, wewe sema kuwa Fakh alikuwa na kadi tatu na toa ushahidi ili tatizo liishe.
ReplyDeleteMwandishi ni mnazi wa simba,hivi malinzi kuwa kiongozi wa fa ya kagera na kuwa kiongozi wa shirikisho LA mpira Tanzania ni ajabu? Franz Anton Beckenbauer amewahi kuongoza shirikisho LA soka german na timu yake bayern Munich At the same time,kina Kassim dewji ,kaburu,hassanoo ni viongozi wa shirikisho kupitia mikoa yao na wako simba pia,mwandishi badilika,unajiabisha Sana kwenye hili,jiongeze,kuwa fair ,kuwa mkweli
ReplyDelete