April 24, 2017



Na Saleh Ally
KAMA kuna mtu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wangepewa nafasi ya kumfungia, basi ninaamini mimi ningekuwa wa kwanza kabisa hata kabla ya Rais wao, Jamal Malinzi hajafikisha hata siku mbili madarakani.

TFF ni shirikisho la aina yake hasa katika kipindi cha Malinzi. Ndiyo shirikisho ambalo limejaza watu wengi wenye uwezo mdogo wa utendaji na ambao wamekuwa na tabia ya “kujilinda” kutokana na kuwa wakali sana hasa pale wanapokosea.

Tunajua mengi sana kuhusiana na TFF ambayo hivi karibuni maofisa wake walifikishwa mahakamani na kushinda kesi ya tuhuma ya upangaji wa matokeo kutokana na mambo ya kisheria.

Lakini kawaida, huku tunajua nini kinaendelea na ndiyo maana hatujawahi kuacha kukosoa kwa nia nzuri ya mchezo wa mpira ambao si wa Malinzi pekee au rafiki zake ambao wamekuwa wakipambana kuuporomosha kwa maslahi yao binafsi.

Najua kwa kipindi hiki, kila mtu aliye TFF, rafiki wa Malinzi au anayefaidika naye atakuwa anafurahia sana kuona kinachofanyika huku akijua si kitu kizuri au hakina msaada wowote kwenye mpira wa Tanzania.

TFF inataka watu wanaosifia madudu yao, mfano kwa kipindi hiki kila mmoja wetu anapigania kuona Serengeti Boys inafanikiwa. Tumekuwa tukifanya michango ya hali na mali huku tukitangaza kwa juhudi zote kuona inafanikiwa.

Lakini najua Serengeti Boys sasa ndiyo inatumika kama kivuli cha kuonyesha eti TFF imefanikiwa sana na kibaya zaidi ndiyo nguzo ya kampeni ya Team Malinzi bila ya kujali kuwa wamefeli vitu 1000 na kufanikiwa kimoja!

Mara kadhaa, nimezungumzia ubabe wa TFF wa kuwafungia kila wale wanaoonekana kuikosoa bila ya kuogopa na watu wote wakakaa kimya bila ya kutetea.

Huenda ushabiki pia umekuwa tatizo. Msomi, Dk Damas Ndumbaro alifungiwa kutokana na kuzitetea klabu za Ligi Kuu Bara baada ya kuonekana TFF inataka kuzipoka haki yao. Ajabu ikatangazwa kufungiwa miaka mitano.

Miaka mitano kwa kuwa ni kipindi ambacho Malinzi atakuwa amegombea kwa mara nyingine kwa kuwa Dk Ndumbaro alionekana ni mtu makini na kama angeamua kugombea, basi mara moja Malinzi ambaye ameonekana kufeli katika mengi, angeanguka.

Ingawa Dk Ndumbaro hakuwa ameonyesha nia ya kugombea, ule uamuzi wa kuzitetea klabu, ikawa amejenga hofu kwa Malinzi. Hakuna aliyelalama na kitu kibaya zaidi ushabiki ukaingia ikaonekana kuwa Dk Ndumbaro ni Simba kwa kuwa alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba, mkakaa kimya.

Mimi niliendelea kukumbusha kwamba si jambo la kuliacha, maana baadaye litaendelea kama Malinzi ataona kila anachoamua hata kama ni cha hovyo, kisichofuata kanuni na kulipua mambo kinaenda tu, mkakaa kimya tu.

Baada ya hapo, TFF ikaenda ikamfungia Msemaji wa Yanga, Jerry Muro kwa madai ametoa maneno makali. Hakukuwa na onyo wala vinginevyo zaidi ya kumfungia ili kumnyamazisha kutokana na namna alivyokuwa akiwaanika.

Muro ni Yanga, wadau wa Simba wakanyamaza na kuona lilikuwa ni jambo jema. Huenda hapa naweza kumpongeza mdau mmoja tu, Haji Manara ambaye ni msemaji wa Simba.

Huyu aliamua kufungua mdomo na kuiomba TFF imsamehe Muro kwamba ni kosa ambalo linasameheka. Nyie mliendelea kukaa kimya na hasa Wanasimba wakiona ni sawa kwa kuwa ni mpinzani na huenda wakati mwingine aliwatoa jasho.

Sasa sakata limehamia kwa Manara, amefikishwa kwenye kamati ya nidhamu ambayo imetangaza kumfungia miezi 12!

Kama hauungi mkono madudu ya TFF, hauna nafasi ya kuchangia au kushiriki katika mchezo wa soka. Jiulize kwa nini kipindi cha Malinzi wadau wanafungiwa tu? Tena mambo yanayowakera TFF yanashughulikiwa ndani ya siku chache tu. Ndani ya wiki, Manara kafungiwa?

Kumbuka rufaa ngapi hadi leo kamati hazijakaa? Wachezaji wamepiga wachezaji wenzao, hadi leo kimya. Kinachomuudhi “mtukufu” Malinzi, ndiyo kinachoshughulikiwa ndani ya siku mbili tu.

Hii si sawa, hii si haki na nyie endeleeni kugawanyika kishabiki, nawaambia mtakwisha wote na itabaki TFF inayoweza kufanya inavyotaka.


Vizuri TFF ikaonyesha ukomavu, wakati mzuri wa kuwa inajibu hoja zinazotolewa na si kufungia tu kwa lengo la kutimiza malengo au matakwa yake. Hii inatia kinyaa kwenye mchezo wa soka na inaonyesha wanaouongoza, hawako kwa maslahi ya mpira wenyewe. Maana ni fungia, juu ya fungia kwa kuwa hakuna majibu juu ya maswali.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic