Simba Sports Club
D'salaam, Tanzania
22/4/2017.
TAARIFA KWA UMMA
Klabu Ya Simba SC inapenda kuwajulisha wanachama na wapenzi wake kuwa imesitisha maandamano iliyopanga kuyafanya Jumanne wiki ijayo 25.04.2017 , baada ya nia na dhamira njema ya serikali kutaka kushughulikia sintofahamu inayoendelea baina ya klabu na Shirikisho la Soka nchi (TFF).
Ikumbukwe jana klabu yetu , ililiandikia barua Jeshi la Polisi nchini ikiomba kibali cha maandamano ya amani, yaliyopangwa kuhudhuriwa na viongozi,wanachama na washabiki wa klabu yetu kwenda Wizara inayosimamia Michezo nchini, yakiwa na lengo la kupeleleka kilio chetu juu ya namna TFF inavyoshughulikia malalamiko ya muda mrefu na ya sasa ya klabu hii kubwa nchini.
Katika barua iliyoandikwa na katibu Mkuu wa Baraza la michezo nchini (BMT) Mohammed Kiganja kwa niaba ya Serikali, imetutaka Shirikisho na Klabu kutafuta namna sahihi na iliyo na weledi katika kushughulikia changamoto hizi zinazoweza kuvuruga amani ya nchi.
Serikali kupitia barua hiyo,imeahidi pia kutukutanisha pande zote haraka iwezekanavyo,ili kwa pamoja tumalize sintofahamu hii kwa maslahi ya mchezo wa mpira wa miguu Tanzania.
Klabu ya Simba inachukua nafasi hii ya kipekee kuishukuru serekali kupitia baraza la michezo la taifa ( BMT) kwa hatua mahsusi na za haraka katika kutafuta suluhisho la kudumu la jambo hili.
Tunawaomba wanachama na washabiki wetu watulie na sote tuache majibizano yoyote ili kutoa fursa kwa Serikali kusimamia kikamilifu jambo hili.
Klabu ya Simba inafanya mawasiliano na Jeshi la Polisi nchini kuwajulisha kusudio letu la kusitisha maandamano hayo.
IMETOLEWA NA...
Haji S Manara
Mkuu wa Habari wa Simba Sc
Simba nguvu moja
0 COMMENTS:
Post a Comment