May 31, 2017


Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog raia wa Cameroon, amepanga kuitumia michuano ya Kombe la Sportpesa kwa ajili ya kukijenga zaidi kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao.
Simba ambayo imemaliza msimu huu ikinyakua Kombe la FA huku ikilikosa Kombe la Ligi Kuu Bara lililotua kwa watani zao wa jadi, Yanga, inatarajiwa kuwa na mapumziko ya takribani siku tano kabla ya kuanza kujiandaa na michuano hiyo.

Michuano hiyo itakayozishirikisha timu nane ambazo ni Simba, Yanga, Singida United na Jang’ombe Boys kutoka Tanzania na Tusker, Gor Mahia, Nakuru All Stars na AFC Leopards za Kenya, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 5, mpaka 11, mwaka huu.

Omog amesema kuwa: “Tunashukuru tumemaliza msimu salama licha ya kuukosa ubingwa wa ligi kuu, lakini kitendo cha kuchukua Kombe la FA ni faraja kubwa kwetu hali ambayo itatufanya msimu ujao tujipange zaidi.


“Baada ya ligi kumalizika, kinafuata kipindi cha usajili ambapo hatutakiwa kufanya makosa kwa hilo na hii michuano midogo ambayo tunakwenda kushiriki, inaweza kutusaidia kuangalia wapi tunatakiwa kujiweka imara zaidi kabla ya kuanza kwa msimu ujao, lakini pia wale wachezaji waliokuwa wanakosa nafasi ya kucheza mara kwa mara, wataanza kuonekana.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV