May 8, 2017



Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe, amemfunika kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya kwa kukaa muda mrefu bila ya kufunga bao kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara.

Tambwe mwenye mabao kumi kwenye orodha ya wafungaji msimu huu, juzi Jumamosi alifunga bao dhidi ya Prisons zikiwa zimepita takribani siku 129 bila ya kufunga kwenye Ligi Kuu Bara. Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Kabla ya bao hilo la juzi, mara ya mwisho Tambwe kufunga bao kwenye ligi ilikuwa ni Desemba 28, mwaka jana dhidi ya Ndanda katika ushindi walioupata Yanga wa mabao 4-0. Mchezo huo pia ulipigwa katika Uwanja wa Taifa.

Huku Tambwe akikaa muda huo bila ya kufunga, awali Kichuya mwenye mabao 11, aliweza kukaa kwa takriban siku 115 akisaka bao katika ligi kuu na kuja kufanikiwa kufunga dhidi ya Yanga kwenye ushindi wa timu yake wa mabao 2-1, Februari 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Kichuya kabla ya bao hilo dhidi ya Yanga, mara ya mwisho kwake kufunga bao ilikuwa ni Novemba 2, mwaka jana wakati timu yake ilipoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stand United katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

“Majeraha ndiyo yaliyokuwa yakinifanya nisicheze kwa kiwango changu na kushindwa kufunga mabao, lakini namshukuru Mungu nimerejea kuendelea kuipigania timu yangu,” alisema Tambwe.


Kwa upande wa Kichuya, alisema: “Kufunga mabao inakuja tu na wala huwezi kupanga, ninapopata nafasi huwa nafunga, lakini kikubwa napenda kuona naisaidia zaidi timu yangu kupata matokeo mazuri bila ya kujali kama nimefunga au la.”

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic