June 2, 2017

HAMAD JUMA


Na Saleh Ally
UKIZUNGUMZIA mapenzi au upole inawezekana Watanzania tukawa tunaongoza kuliko raia wengi wa nchi nyingi za Afrika na ikiwezekana sehemu nyingine duniani.

Watanzania hatupendi bugudha na si watu tunaopenda kuona mambo yanakwenda katika mwendo wa tafrani. Tunapenda mambo laini na ikiwezekana yanayofurahisha au kuburudisha zaidi.

Kibaya zaidi katika mwenendo wa sisi wengi, unafiki umetawala sana na watu wasingependa kuambiana ukweli uso kwa uso. Lakini wanapokaa pembeni, wangependa kusema jambo fulani kuhusiana na mtu fulani ambaye wangeweza kuwa na nafasi ya kumueleza uso kwa uso.


Leo mimi nakwenda moja kwa moja kama nilivyozoea na kuamini ni sahihi na nitazungumzia mabeki wawili wa kulia wa Simba.


Mabeki hawa wawili, wote wametua Simba wakitokea timu tofauti. Mmoja ni raia wa Tanzania, huyu ni Hamad Juma na mwingine ni raia wa DR Congo, Janvier Besala Bukungu.

Bukungu ana miaka zaidi ya 33, amewahi kucheza timu kubwa kama TP Mazembe na kadhalika. Simba ilionekana kama amejiunga akienda kustaafu soka. Lakini kaonyesha uwezo na mchango mkubwa na kuwashangaza wengi.

Mwisho Katika Ligi Kuu Bara Simba imemaliza ikiwa sawa na Yanga ambao wamebeba ubingwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa baada ya kuwa na pointi 68 kila moja.

Simba wamebeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho baada ya kuifunga Mbao FC kwa mabao 2-1 katika mechi ya fainali. Mechi zote muhimu au nyingi za Ligi Kuu Bara zilizochezwa, alicheza Bukungu. Alipokuwa majeruhi au ana kadi, alilazimika kiungo Mghana, James Kotei kuziba nafasi yake.

Katika hali ya kawaida, mshindani wake ni Hamad ambaye alijiunga na Simba akitokea Coastal Union na akipewa nafasi ya kupambana na Hassan Kessy ambaye baadaye alijiunga Yanga. Sasa ikaonekana ni Hamad atatamba, wapi, kaingia Bukungu naye kachukua namba.



Hamad amekuwa akituhumiwa na tabia za ulevi kupindukia. Wakati fulani alianguka, uongozi wa Simba ukasema alianguka bafuni. Baadaye siri ikafichuka, tuhuma zikasema alianguka kwenye ngazi akiwa “bwii”.

Jana wakati wa mahojiano ya kipindi cha Spoti Hausi kinachorushwa na Global TV Online. Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, aliamua kufunguka kwamba kweli Hamad aliwashinda kutokana na ulevi na kushindwa kuonyesha mwendo sahihi wa ushindani.

Hakuna ubishi, Hamad anaonekana hana nafasi Simba na huenda kitakachofuatia ni kusema “amepigwa misumari” ili mambo yake yasiende vizuri na inafikia wakati najiuliza, vipi alifanya juhudi akacheza vizuri Coastal Union na Simba imemshinda.

Je, ni mshahara mzuri au posho kubwa ya Simba kuliko ile ya Coastal Union? Ni akili matope au ulimbukeni wa mjini? Ni mtu asiyependa ushauri au anaamini anajua kila kitu?

Wako wengi wameanguka kama Hamad na huenda walikuwa wabishi kuelezwa au kuamini wanajua kila kitu. Wako walishindwa kama yeye lakini wakaona wameonewa, wamesakamwa au walibaniwa na wakati mwingine kuamini hisia za kishirikina wakati “Shiriki” wanaitengeza wao kwa matendo yao!

Anawezaje Bukungu kufanya vizuri zaidi na Hamad akashindwa? Jibu ni kwamba Bukungu anajitambua na anajua maana ya kutafuta maisha au kupambana na kitu ili kupata anachohitaji.

Huyu Hamad uongozi wa Simba uliona sahihi kumfichia siri. Hans Poppe alisema walifanya hivyo wakiamini atajirekebisha. Lakini mwisho wameona amewashinda.

Sasa jiulize, Hamad ana kipaji, akiachwa Simba akasajiliwa timu nyingine ndogo yenye mshahara na posho kidogo ndiyo ataanza kujituma tena! Akisajiliwa tena katika timu kubwa, atakuwa kama alivyo Simba tena?

Iko haja ya Hamad kujitambua na kubadilika. Wachezaji wa Kitanzania utafikiri mba laana. Amsheni masikio yenu, fungueni macho mtazame mbele. Mmekuwa nyuma mar azote na visingizio lukuki lakini nyie ni sehemu ya mpira wan chi yetu kufeli.

Hamad, hao hawataki kukueleza ukweli. Ndiyo maana unahisi uko sahihi. Brother, unaharibu, jichambue upya.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic