June 3, 2017Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema timu yake imechoshwa na kauli zisizoeleweka za wachezaji Jonas Mkude, Abdi Banda na Ibrahim Ajibu kuhusu usajili mpya, hivyo kamaa wanataka kuondoka ruksa.

Hans Poppe ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache tangu Banda awaage mashabiki wa timu hiyo akitangaza kuondoka Msimbazi kupitia ukurasa wa akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram.

Mikataba ya wachezaji hao tayari imemalizika mwishoni mwa msimu uliopita na sasa wanatajwa kuondoka kwenda kwenye moja za klabu za hapa nchini.

Akizungumza katika Kipindi cha Spoti Hausi kilichorushwa juzi Alhamisi na GLOBAL TV Online, Hans Poppe amesema wachezaji hao wote watatu wamefanya nao mazungumzo lakini anashangaa wanaposema wanavyozungumza tofauti mitandaoni na kwenye vyombo vya habari.

Hans Poppe alisema: “Tulikubaliana nao kila kitu na kilichobaki ilikuwa ni kuwakamilishia mahitaji yao ikiwemo dau la usajili na vitu vingine.

"Banda alivyofanya siyo sawa, tumezungumza naye pamoja na Ajibu na Mkude, lakini wanavyosema hatujaongea nao si sawa na kama wanabadilika hivi niseme tu waende zao.

"Inashangaza mtu unazungumza naye anakubali kila kitu halafu baadaye anaongea vitu vingine, hata kama wanataka kuondoka waage vizuri haya ni maisha ya soka watakuja kujuta baadaye.”

Banda anatajwa kupata timu Afrika Kusini iitwayo Polokwane City FC wakati Ajibu nan Mkude wanatajwa kuwaniwa na Yanga na Singida United.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV