June 3, 2017
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, amesema kamwe hawatakubali kuonewa tena na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na badala yake watakwenda Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kudai uhalali wa straika Mbaraka Yusuph kwani anaamini ni mchezaji wao.

Hans Poppe alitoa kauli hiyo katikati ya wiki hii alipokuwa akizungumza katika Kipindi cha Spoti Hausi cha Global TV Online kinachorushwa kila Alhamisi saa 10:00 jioni.

Chanzo cha Hans Poppe kusema wataenda Fifa ni tetesi kuzagaa kwamba Mbaraka aliyefunga mabao 12 kwenye msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, anatakiwa Yanga.

Mbaraka hivi karibuni alizua mvutano mkubwa juu ya usajili wake, Simba wenyewe wanadai ni mchezaji wao ila walimtoa kwa mkopo Kagera Sugar, huku klabu hiyo ya Kagera ikisisitiza straika huyo ni mali yao.

Hans Poppe alisema, Mbaraka bado ni mali yao na walimtoa kwa mkopo Kagera kwa ajili ya kukiendeleza kipaji chake baada ya kuona hana nafasi ya kucheza katika kikosi cha Simba, wanamrudisha.

Hans Poppe alisema, Mbaraka alisajiliwa Simba kwa mkataba wa miaka mitatu na aliyekuwa meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu lakini wanashangaa kupata taarifa za Mbaraka kusaini mkataba mpya wa kuichezea Kagera.

“Niseme ukweli hatutakubali tuone tunaonewa na TFF kwa kuchukuliwa wachezaji kirahisi, hivyo basi tutakuwa tayari kwenda Fifa kupeleka kesi nyingine kwa ajili ya kwenda kudai uhalali wa mchezaji Mbaraka.

“Mbaraka ni mchezaji mwenye mkataba na ikumbukwe kuwa mchezaji huyo tulimtoa kwa mkopo Kagera, na kinachofanyika ni utoto kati ya TFF na Kagera wenyewe wanafanya magumashi ili kujimilikisha mchezaji huyo.

“Wao walichokifanya ni Kagera kumbadilisha jina mchezaji huyo kwa kumuita Mbaraka Yusuph badala ya Mbaraka Abeid, jina alilokuwa analitumia akiwa anaichezea Simba.

“Walilibadilisha jina kwa lengo lisisome kwenye TMS wao Kagera kwa kushirikiana na TFF, hivyo tumegundua hayo ni magumashi wanayofanya, hivyo tumepanga kwenda Fifa kushtaki,” alisema Hans Poppe.

Kama ikienda Fifa, hii itakuwa mara ya pili kwa Simba kupeleka malalamiko yake kwa shirikisho hilo kwani hadi sasa inasubiri jibu la malalamiko yake ya kupokwa pointi tatu na TFF kwa kosa la Kagera Sugar kudaiwa kumchezesha Mohammed Fakhi mwenye kadi tatu za njano.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV