June 10, 2017Fainali ya michuano ya SportPesa Super Cup inatarajiwa kuchezwa kesho Jumapili kwa Gor Mahia na AFC Leopards zote za Kenya ambazo zikikutana mechi yao huitwa Mashemeji Derby.

Timu hizo zimetinga fainali baada ya Gor Mahia kuitoa Nakuru All Stars ya Kenya kwa mabao 2-0 katika nusu fainali huku AFC Leopards ikiitoa Yanga kwa penalti 4-2 katika hatua hiyo juzi Alhamisi kwenye Uwanja wa Uhuru.

Fainali ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha ya SportPesa, inatarajiwa kuanza saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Bingwa wa michuano hii iliyoanza Juni 5, mwaka huu atapewa zawadi ya dola 30,000 (Sh milioni 66.9) na nafasi ya kucheza dhidi ya Everton ya England Julai 13, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Leopards, Denis Kitambi raia wa Tanzania alisema, hiyo ni fainali ngumu kwa pande zote kutokana na kuzikutanisha timu zinazofahamia aina ya uchezaji na mbinu zao.

“Mechi ni ngumu kwetu kiukweli na ninaamini siyo peke yetu hata kwa wapinzani wetu kwa sababu hizi ni timu pinzani nchini Kenya, lakini kwa maandalizi niliyoyafanya nina matarajio ya kuchukua kombe hili,” alisema Kitambi aliyeipandisha daraja Ndanda FC.

Kwa upande wa Kocha wa Gor Mahia, Zedekiah Otieno alisema: “Kikosi changu nilikiandaa kwa ajili ya kukutana na timu yoyote kwenye fainali, hivyo kukutana na Leopards hakukunishitua.

“Nitaendelea kuwapa mbinu wachezaji wangu ili tushinde mechi hii ya fainali.”


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV