June 5, 2017




Na Saleh Ally
MICHUANO ya SportPesa Super Cup inaanza leo jijini Dar es Salaam lengo likiwa ni kutafuta nafasi ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi moja ya timu maarufu za nchini England, Everton.

Mechi ya kirafiki kati ya Everton na bingwa wa SportPesa Super Cup itapigwa Julai 13, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Timu zitakazoshiriki michuano hiyo kutoka Tanzania ni Simba, Yanga, Singida United na Jang’ombe Boys na Kenya ni Gor Mahia, AFC Leopards na Nakuru All Stars.

Michuano hiyo si ya ligi kuu au mshindi atakayepatikana atakwenda kucheza michuano ya kimataifa chini ya Shirikisho la Soka la Afrika (Caf).

Lakini ni michuano ambayo itatoa nafasi kwa timu ya Ukanda wa Afrika Mashariki kucheza mechi ya kirafiki na timu kubwa ya Everton, hakuna ubishi kutakuwa na sehemu ya kujifunza.

Wakati michuano hiyo inaanza leo, bado inaonekana msisimko si mkubwa sana na kama vile baada ya ligi kuu, wenye “nchi” Yanga na Simba wana mipango yao.

Simba na Yanga wanaona wamecheza mechi nyingi baada ya ligi kuu na Kombe la Shirikisho. Hivyo huenda wakawatumia wachezaji wengi sana ambao ni wageni machoni mwa wengi.

Baadhi ya viongozi wa klabu hizo wameshasema wanataka kuitumia michuano hiyo kuwajaribu wachezaji wao wapya ambao watakuwa wamejiunga na timu zao au wana mpango wa kuwasajili.

Si vibaya kwa mpango wa maandalizi kwa ajili ya msimu mpya, lakini nilitaka kuwakumbusha, bado suala la heshima ya timu au klabu hujengwa na kufanya vizuri katika michuano.

Michuano ya SportPesa Super Cup haina tofauti na ile ya Emirates Cup ambayo timu kama za Arsenal au Real Madrid hushiriki licha ya kwamba zenyewe zina michuano migumu zaidi.

Timu inapofanya vizuri katika michuano yoyote iliyoamua kuingia ni heshima. Itakuwa ajabu sana kama klabu inakubali kushiriki michuano ambayo inaona ni midogo.

Kama ingekuwa midogo au haitakiwi kupewa hadhi basi moja kwa moja isingeshiriki. Si sahihi klabu inayojitambua kujaribu mambo, badala yake inatakiwa kuyafanya kwa uhakika kabisa.

Kwa wachezaji ambao watapewa nafasi kwa kuwa wanataka kusajiliwa, nao wana kila sababu ya kuonyesha thamani ya michuano na timu wanazotaka kuzichezea.

Wote tunajua, Tanzania imekuwa na michuano michache sana na wachezaji wa Tanzania wamekuwa wakicheza mechi chache sana kwa msimu huku wengine wakiambulia kulamba benchi kwa msimu mzima na mwisho wanaishia kucheza mechi za mchangani ambazo haziwapi hatua sahihi kimaendeleo.

Michuano kama ya Kombe la Shirikisho ya Azam Sports imeleta mwamko mpya na unaona namna ambavyo mambo yamekuwa na ushindani na wachezaji wanafaidika.

Sasa kuna SportPesa Super Cup, kama wachezaji wataonyesha ushindani na kulenga kufanya vizuri, maana yake watayainua na kuyafanya yawe makubwa na yenye msisimko.

Kama watafanya vizuri, hata wadhamini wa michuano hiyo, Kampuni ya SportPesa itashawishika kuongeza dau au udhamini na mwisho wanaofaidika zaidi ni wachezaji wenyewe.

Lazima wachezaji wakubali kwamba kweli wanatafuta lakini wajue na heshima wanayopewa wanavyopaswa kuitumia ipasavyo.

Wale ambao tayari wana nafasi katika timu, basi wajifunze kuwepo kwa michuano zaidi ya miwili, kunawaongezea faida kadhaa kama kupata nafasi ya kucheza zaidi na kujiimarisha lakini hata kimaslahi kwa kuwa posho zinaongezeka na wakishinda wanafaidika zaidi kupitia ongezeko la kipato.


Kwa viongozi, hawana ujanja. Lazima wajue kuwa wadhamini kama SportPesa wameingiza fedha na wao wangependa kuona mafanikio katika wanachokidhamini, hivyo wanapaswa kukithamini na kuonyesha weledi ili msimu ujao hata kama inafanyika Kenya, basi kuwe na uboreshwaji wa maslahi na mambo mengine.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic