July 14, 2017
Na Saleh Ally
HIVI karibuni, kipa mkongwe wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Manyika Peter alieleza namna alivyoamua kuchukua uamuzi mgumu kwa mwanaye kipa, Peter Manyika.

Mzazi huyo ambaye ni mmoja wa wachezaji wachache wa Tanzania waliowahi kucheza nje ya Tanzania, alieleza jinsi ambavyo hafurahishwi na mwanaye kutopata nafasi katika klabu yake ya Simba.

Manyika aliwahi kucheza Shelisheli, Iran pia lakini amewahi kuwa kocha wa makipa katika timu ya Ligi Kuu nchini Oman ya Seeb.

Wakati akielezea uamuzi wa kumshawishi mwanaye aachane na Simba, Manyika alielezea namna ambavyo amekuwa hapati nafasi ya kucheza na kusisitiza umefika wakati wa kuangalia nafasi ya kucheza kuliko fedha au mshahara mkubwa.

Anaamini kwa umri alionao mwanaye ni jambo gumu kuendelea kukaa benchi huku akipata fedha. Anaona hivyo si kuujali mpira na mapenzi yake au kutoangalia maendeleo na mwisho anaona bora acheze timu ndogo inayompa nafasi ya kucheza kuliko kupokea mshahara mkubwa huku akiwa benchi Simba.
Kwa wanaofuatilia makala zangu, watakuwa wanakumbuka niliwahi kusema kuhusiana na wakati mwafaka wa Manyika kuondoka Simba ili apate nafasi ya kucheza.

Aliendelea kubaki msimu mmoja tena ambao hajacheza hata zaidi ya mechi tano ukijumlisha zile za ligi na zile za kirafiki. Badala yake Simba ilikuwa ikipambana kusajili makipa wapya bila kujali ana uwezo pia.

Katika mechi za kirafiki pia, nafasi kubwa mwanzo ilikuwa kwa kipa Vincent Angban na baadaye wakamsajili Daniel Agyei ambaye alicheza hadi mechi za kirafiki tena mikoani ambazo ingekuwa nafasi kubwa kwa kipa kama Manyika kujenga hali ya kujiamini.

Wakati Manyika anaamua kumuondoa mwanaye, naona kama kuna kosa jingine limefanyika ambalo linataka kulingana na hilo alilolifanya Manyika.

Nakukumbusha hivi, mmoja wa wachezaji waliofanya vizuri msimu uliopita alikuwa ni kipa kinda Ramadhani Kabwili ambaye hakika alistahili kucheza timu ya ligi kuu.

Kabwili alionyesha cheche zake hasa katika kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys.
Nakumbuka Kabwili ni kati ya wachezaji makinda ambao walikuwa katika timu ya vijana ya Azam FC na alikuwa akionyesha kuwa baadaye atakuwa bora.

Sijajua aliondoka vipi Azam FC, lakini baadaye nilianza kumuona akionyesha cheche zake akiwa na Serengeti Boys na mwisho hakuna anayeweza kupinga kwamba alionyesha uwezo mkubwa na alikuwa msaada.

Kabwili ambaye ameisaidia Serengeti kucheza Kombe la Mataifa Afrika, anakuwa hana tofauti na Manyika ambaye alifanya vizuri katika kikosi hicho cha vijana hadi kuivutia Simba.

Kabwili kaivutia Yanga ambayo tayari ina makipa wawili, mmoja ni mpya ambaye ni Rostand Youthe, raia wa Cameroon lakini kuna Beno Kakolanya. Hakuna uhakika hadi sasa kama Deogratius Munishi ‘Dida’ ameishaondoka au Mustapha Ally ‘Barthez’.

Kipa huyo anakwenda Yanga, unaweza ukasema si kosa kama utaangalia uwezo. Hakuna ubishi nafasi yake itakuwa ndogo kucheza kama ukiangalia uzoefu.

Kama Yanga itaamua kubaki na makipa wanne, basi atakuwa kipa namba nne. Ikibaki na watatu atakuwa kipa namba tatu na ukumbuke pamoja na kuwa na michuano mingi, ina michuano ya kimataifa.

Kocha kawaida huangalia zaidi mchezaji anayefanya vizuri sana na asingependa kumuweka benchi na kujaribu mwingine kwa lengo la kufanya “naye acheze”.

Kama kipa amefanya vizuri katika michuano ya kimataifa, kocha atamuweka katika mechi za ligi kwa kuwa anajua zitampa nafasi ya kucheza vizuri michuano ya kimataifa. Na mfano mzuri wa hili ni kipindi cha Juma Kaseja, wengi walilaumu lakini Kaseja hakuwa akijipanga.

Sasa Kabwili anaweza kupata fedha nyingi lakini akaendelea kuwa kipa wa mazoezini na benchi. Mwisho kiwango kitashuka na kupoteza nafasi ya timu ya taifa kwa kuwa wako wengi wenye ushindani katika nafasi yake.

Kama angejiunga na Ruvu Shooting, Majimaji na kadhalika. Timu zisizokuwa na presha kubwa ingekuwa nafasi yake ya kuonyesha uwezo.

Kama angecheza msimu wa kwanza hata mechi 15, msimu unaofuata angepata nafasi zaidi na mwisho angekuwa na uwezo wa kujiunga na timu kubwa saizi ya kati au zile kubwa kabisa zenye presha.

Kuna bahati inaweza kumtokea Kabwili, labda waumie makipa wote ili acheze. Ninampa moyo anaweza, lakini naona uamuzi wake haukuwa sahihi na alipaswa kujiunga na timu ambayo angepata nafasi ya kucheza kuepuka yale ya Manyika.

Vizuri kwenda kwenye kikosi kikubwa ukiwa na uzoefu angalau kidogo. Mara nyingi wanaoanzia timu kubwa, inapendeza wale waliokulia kisoka katika timu za vijana za timu husika na wanakwenda wanapanda taratibu.


0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV