August 11, 2017




Beki wa zamani wa Yanga na Taifa Stars ambaye ni mgombea wa nafasi ya urais katika Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ally Mayay Tembele, juzi Jumatano alizindua rasmi kampeni zake ambapo miongoni mwa mambo aliyoyabainisha ni namna gani ataitendea haki nafasi hiyo endapo atapata nafasi ya kuliongoza shirikisho hilo.

Mayay ambaye aliwahi kuwa mchezaji wa Yanga, ameamua kuwania nafasi hiyo huku akiwa na kauli mbiu ya ‘Turudishieni Mpira Wetu’, ambapo mbali na kumwaga sera zake, lakini pia amefafanua kwa nini ameamua kuingia na kauli mbiu hiyo.

Ameweka wazi vipaumbele vyake ambavyo ni kuanzisha mkakati wa maendeleo ya soka la Tanzania, urasimishaji wa soka, kujenga na kuboresha miundombinu ya mchezo huo, uendelezaji wa soka la wanawake na la ufukweni na mkakati wa maandalizi ya fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Vijana (U-17) mwaka 2019 hapa Tanzania.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Mayay alisema: “Kwa kutumia uzoefu wangu na uelewa wangu wa changamoto zilizopo katika soka, nitahakikisha nabadilisha kila kilichokuwa kibaya kuwa kizuri kwa lengo la kuwarudishia mpira wao Watanzania waliopoteza matumaini na viongozi wao wa soka.

“Nadhani mnajua kuwa mimi nina mapenzi ya dhati na mpira na maisha yangu ni kielelezo cha mapenzi hayo, hivyo nimeona sasa ni wakati muafaka wa kugombea nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu kwenye kuuinua mpira wa nchi hii ambao wengi tunaupenda.”


Aidha, Mayay alifafanua kauli mbiu yake kwa kusema: “Naamini kwa dhati kabisa kuwa Watanzania wapenzi wa soka wana mapenzi ya dhati kabisa na mchezo huu na wamekuwa na kiu ya muda mrefu ya kutaka mafanikio katika mchezo huu lakini bahati mbaya mafanikio hayo yamekuwa hayapatikani.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic