August 7, 2017
Na Saleh Ally
ZILE hadithi za nani anataka kumsajili nani au yupi anataka kufanya usajili wa kutisha, zimefikia kikomo na huu ndiyo muda mwafaka wa kupata majibu ya kile ambacho kilizungumzwa kwa muda mrefu.

Usajili wa Ligi Kuu Bara umefungwa usiku wa kuamkia leo na kila timu itakuwa imejitosheleza kama ambavyo ilitaka kufanya hadi mwisho wa ligi na malengo kwa timu zinazojiamini huwa ni kubeba ubingwa na si kingine.

Wakati wa usajili kumekuwa na mambo mengi sana yanayojitokeza. Mfano utasikia mchezaji huyu anakwenda huku na baadaye ikawezekana au kushindikana.

Ni kawaida kabisa kusikia mchezaji amemalizana na uongozi wa Yanga, kesho ukasikia yuko Azam FC au vinginevyo. Ni kipindi kigumu ambacho huwachanganya viongozi, wachezaji wenyewe, mashabiki na wakati mwingine hata waandishi na vyombo vya habari.

Unajaribu kuangalia nani anaweza kuwa amefanya usajili bora zaidi. Lakini bado kila mmoja atakuwa na maoni yake akiamini huyu na mwingine ataamini yule, basi ilimradi kila mmoja anaamini anavyoona mwenyewe.

Kuna wanaoweza kupatia kwa kukuambia kwamba kikosi fulani kimefanya usajili mzuri na kuna wanaoweza kuwa wamekosea. Lakini sasa ndiyo wakati mwafaka wa kupata majibu sahihi yasiyo ya kubashiri tena.

Kipindi hiki kila aliyefanya usajili ana nafasi ya kujua jibu ya kile ambacho alikifanya. Kwa mashabiki watapata jibu pia kwamba yupi hasa alifanya usajili mzuri au unaoweza kuwa na matunda.

Ligi ina mambo mengi sana na kila jambo lake ni hatua na hapo utaona kila upande ukipita katika milima na mabonde na mwisho subira au uvumilivu wa mambo, kuamini kujifunza na ubunifu wa mambo unaweza kuusaidia usajili bora kufanya vizuri zaidi au kuuinua usajili usio bora sana kuanza kufanya vema.

Lakini kutokuwa na subira, kuharakisha mambo kunaweza kusababisha waliokuwa na usajili bora wakajichanganya na kufanya mambo yaende kwa hofu kuu na mwisho kuishia kufeli kwa kuwa wahusika wanaweza wasiwe na subira kwa kuwa waliamini walisajili vizuri sana.

Hii itakuwa ni sehemu ya kudhihirisha kwamba usajili bora pekee hauwezi kutosha badala yake kuna mambo mengi ya kufanya.

Lakini wachezaji nao ndiyo wakati wa kuonyesha thamani yao kwamba walistahili kusajili kwa kiwango ambacho huenda kilikuwa kikubwa sana.
Hata wale waliosajiliwa kwa fedha ambayo wanaona ilikuwa ni kiwango cha chini, sasa wauonyeshe umma kwamba walistahili juu zaidi.

Mashabiki nao ni sehemu ya kufanya mambo yaende vizuri au yaharibike. Inawezekana timu iliyotegemewa kufanya vizuri ikafanya vibaya mwanzoni halafu ikawa na nafasi ya kujirekebisha hapo baadaye.

Lakini kama kutakuwa na presha kubwa kupindukia kutoka kwa mashabiki wake, halafu ikasababisha wachezaji kufanya vibaya zaidi, maana yake inaweza kusababisha mwendo wa timu husika kuendelea kuwa mbaya zaidi na mwisho kuishia katika nafasi mbaya zaidi bila ya kutegemewa.

Waamuzi wanaweza kuwa watu wengine wenye nafasi ya kufanya usajili wa timu zote upate majibu sahihi au majibu ya kubabaisha.

Majibu sahihi ni kama waamuzi watakuwa makini na kufuata mkondo wa haki kupitia sheria 17 kwa usahihi kabisa. 
Waamuzi kama watakuwa ni wale wanaoingia uwanjani na matokeo mfukoni, watachangia kuvuruga mambo na kusababisha matokeo kuwa yasiyo ya haki na hapa usajili bora hautakuwa na nguvu kabisa.

Maana yangu kwa yote ni kwamba, usajili bora pekee kwa timu fulani hauwezi kuwa kila kitu. Badala yake maandalizi bora, uendeshaji sahihi wa timu wakati wa ligi halafu uingie kwa viongozi kwenda na mwendo sahihi, makocha kufanya mambo kwa ufundi na ubunifu, wachezaji kujituma na mashabiki kuonyesha ushirikiano ndiyo unaweza kusaidia ubora wa kikosi kuthibitisha usajili sahihi au kuuinua hata ambao haukuwa sahihi kwa kiwango cha juu.
0 COMMENTS:

Post a Comment

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV