September 23, 2017






Na Saleh Ally aliyekuwa London
KOCHA Mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger ndiye mtu anayezungumzwa zaidi na mashabiki wa klabu hiyo maarufu duniani.

Kuna wanaoona ni wakati angeondoka, kuna wale wanaoona anatakiwa kubaki. Kuna mengi yanayoendelea kuhusiana na Wenger na Arsenal inaendelea.


Kama utapata nafasi ya kufika jijini London na kuitembelea Klabu ya Arsenal, unaweza kushangazwa kwamba pamoja na kuwa kocha, Wenger ni mtaalamu wa masuala ya uchumi aliyechangia Arsenal kupata mambo mengi
sana.

SALEH ALLY "JEMBE" AKIWA NDANI YA OFISI YA WENGER

Arsenal hufanya mazoezi katika Uwanja wa Colney London, umbali kwa takribani Kilomita 41 kutoka London katikati. Huko kuna ofisi nzuri ya Wenger kama ilivyo kwa makocha wengine.


Ofisi hiyo, si rahisi kuigusa labda upate mwaliko kutoka kwa kocha huyo kwa ajili ya masuala ya kikazi. Kwani hata anapokuwa sehemu hiyo, kama ni mwandishi basi nafasi yako kukutana naye ni katika chumba maalum kwa ajili ya mahojiano na waandishi wa habari.


Ofisi ya Colney inaelezwa kuwa binafsi zaidi na sehemu ambayo angependa kutulia na kufanya kazi zake kwa utulivu mkubwa.


Ukiachana na ofisi hiyo kwenye viwanja vya mazoezi, kuna ofisi nyingine ya Wenger ambayo iko katika Uwanja wa Emirates katika eneo la Isilington ambayo mara nyingi anaitumia wakati wa mechi.

SEHEMU YA WAANDISHI WA HABARI

Wenger anaitumia ofisi hiyo pale tu Arsenal inapokuwa ina mechi na 
mara chache kama kuna wageni ambao wanamtembelea pale Emirates.


Ofisi hiyo sasa inaingiza fedha nyingi kwa Klabu ya Arsenal kwa kuwa watu wengi ambao wanataka kujua kuhusiana na historia ya Arsenal, wangependa kufika ndani ya ofisi hiyo.


Kutokana na uhitaji huo mkubwa, Arsenal wameamua kutoa nafasi kwa wapenda soka kuitembelea ofisi hiyo na wamekuwa wakilipa kiingilio.





Mtaalamu wa historia wa Arsenal ambaye yuko katika uwanja huo anasema kwa wale wanaotembelea uwanja huo kutoka sehemu mbalimbali duniani, wamekuwa wakivutiwa na vitu vitatu vikubwa.


Kwa sasa, ofisi ya Wenger ndiyo inashika namba moja kwa vitu hivyo vitatu kwa kuwa kila mmoja anataka kuiona ofisi ya kocha huyo mkongwe.




Pili ni vyumba vya kubadilishia nguo, wapenda mpira wakiwemo mashabiki wa Arsenal, wangependa kuingia na kupiga picha sehemu ambayo wachezaji hukaa na tatu na mwisho ni sehemu ya katikati ya uwanja.


Mashabiki wanaotokea nje ya England au London, wangependa kutokea upande wa ndani ya uwanja ambako waone mazingira na mwonekano.

Kila anayeingia hulipa pauni 14 (Sh 42,000) na kwa siku kama mambo ni mazuri, watu hadi 2,500 hutembelea na kunapokuwa na watu wachache basi hadi watu 150 inategemea kuhusiana na hali ilivyo.


Ndani ya ofisi ya Wenger kuna mambo mazuri unaweza kujifunza. Kuna makochi tu na sehemu ya yeye kutundika makoti yake, upande wa pili kuna runinga iliyo ukutani na anaweza kuona kinachoendelea.


Chumba chake ndani kina maliwato inayojitegemea na sehemu maalum kwa ajili ya chakula kama ataamua kupata chakula laini.




Kitaalamu iko hivi; chumba cha Wenger kimetengenezwa kikiwa kinaingiliana na chumba cha kubadilishia nguo cha wachezaji. Hivyo wote wanaingia kwenye lango moja, wanapita sehemu ya mabafu ya bwawa dogo la kuogelea la wachezaji, chumba cha madaktari halafu wanaingia
katika chumba cha wachezaji. Baada ya hapo, Wenger anaingia chumbani kwake.

Kawaida, Wenger anapofika uwanjani na kushuka kwenye basi akiongozana na wachezaji naye anapitiliza chumbani kwake. Wao huendelea na taratibu zao ikiwa ni pamoja na kutoka nje kwenda kupasha misuli.


Wanaporejea, yeye hutoka chumbani kwake na kuzungumza nao kwa takribani dakika tano halafu anarudi chumbani akisubiri wao watoke naye anafuatia.




Wakati wa mapumziko, utaona yeye anawahi, kawaida hupitiliza katika ubao ulio katika chumba cha wachezaji karibu na mlango wa kuingia ofisini kwake na kuanza kuchora anachotaka kufundisha. Wachezaji wanapofika wanaendelea na mambo yao kwa dakika tatu hadi tano, halafu anaanza kutoa somo na dakika tatu hadi tano za mwisho anawaacha washauriane kabla ya kurejea uwanjani.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic