September 7, 2017



Na Saleh Ally, Manchester
JUNI 2015 wakati Manchester United ikiivaa Southampton katika mechi ngumu ya Premier League alikatisha panya uwanjani. Hii ilisababisha malalamiko makubwa kwa mashabiki kwa kuwa lilionekana ni kama jambo la aibu kwa klabu.

Januari 2016, Kocha Louis van Gaal alilalamika kwamba utengenezaji wa uwanja sehemu ya kuchezea yaani pitch ulikuwa unachelewa licha ya klabu kutoa pauni 800,000 (Zaidi ya Sh bilioni 2.3). Wakati mwingine wanalazimika kuchelewa kufanya mazoezi kwa kuwa kunakuwa na mambo ya matengenezo.



Suala la uwanja huo wa kuchezea kuonekana una matatizo lilionekana kuukerea uongozi na Bodi ya Manchester United ambayo kikubwa inachotaka ni kulinda heshima ya klabu hiyo maarufu kuliko zote England na moja ya klabu tatu kubwa zaidi duniani, nyingine mbili zikiwa ni Real Madrid na Barcelona zote za Hispania.

Baada ya hapo, aliyepewa fedha kwa ajili ya kazi hiyo akahimizwa na yeye akafanya kweli na awali, ilionekana ulitakiwa kuwa kama ule wa Wembley ambao ni mali ya Serikali ya Uingereza lakini safari hii, pitch ya Old Trafford inaonekana ndiyo bora zaidi England na ikiwezekana Ulaya na inawezekana kufananishwa na ile iliyo katika Uwanja wa Emirates pekee.

Emirates unamilikiwa na wapinzani wakubwa wa Man United. Hawa ni Arsenal walio katika Jiji la London.
Nikisema ni kati ya watu wachache ambao si wachezaji waliofanikiwa kufika kwenye uwanja huo  katika pitch ni mimi. Huenda hii ni bahati kubwa na imenisaidia kujifunza ambacho nachangia nanyi wasomaji ili tujifunze wote.



Kilichonivutia ni baada ya kuwa pale katika pitch na wachezaji wakongwe wa Barcelona na wale wa Man United. Wale wa Barcelona walianza kushangazwa na namna ubora wa pitch ulivyo na mwisho nilimsogelea Eric Abidal na kumuuliza kama ile ya Nou Camp haifanani na hiyo?

 Abidal aliyekuwa tegemeo la FC Barcelona na sasa ni mmoja wa magwiji wa klabu hiyo aliniambia;
 “Huu ni uwanja wa aina yake, haufanani hata kidogo na ule wa Camp Nou. Unajua, Camp Nou wana uwanja bora wa kuchezea, lakini huu ni bora zaidi. Hata wa kule Madrid pia si kama huu.”

Hii ikanifanya nivutiwe zaidi na hasa kwa kuwa niliona utaratibu wa maandalizi siku moja kabla ya mechi namna majani yalivyokuwa yanakatwa lakini wakati wa mapumziko. Waliingia vijana takribani 18 haraka na kuanza kufanya marekebisho wakirudishia nyasi sehemu zilipong’oka. 



Mwisho niliwaona wakirudi mara tu baada ya mechi kwisha na kuanza kuzikata nyasi na mashine nane zilizokuwepo tena wakienda kwa utaratibu maridadi kabisa. Yaani kwa msitari na kila mmoja alijua anatakiwa kukata kona kushoto au kulia.

Lakini kabla mechi haijaisha, nilianza kumtafuta msimamizi mkuu wa uwanja aliyejitambulisha kwa jina la Allah Smith ambaye alinithibitishia kuwa pitch yao ndiyo bora zaidi duniani kwa kipindi hiki kutokana na teknolojia mpya.

Akasema hata kwa huduma inakuwa tofauti kwa kuwa Manchester United na Arsenal ndiyo timu zilizoanza kutumia teknolojia mpya ya majani ya kawaida au asili wenyewe wanasema natural kuchanganywa na yale ya bandia.

Unajua kuna viwanja vya asili kama Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na ule wa bandia kama ulivyo wa Uhuru lakini nyasi za Old Trafford ni asili asilimia 97 na asilimia 3 ni bandia na hii ni kuyafanya majani kuwa imara zaidi na mfumo mpya unaowafanya wachezaji kuwa salama zaidi.

Lakini kama hiyo haitoshi, uwanja huo kwa chini una mabomba maalum yenye uwezo wa kutengeneza joto kunapokuwa kipindi cha baridi au kuwa ya baridi sana kunapokuwa kipindi cha joto kali ili kuufanya uwanja kuwa na hali ya hewa isiyowapa tabu wachezaji.

Katikati uwanja umeinuliwa kwa inchi nane ili maji ya mvua yamwagike pembeni kutowasumbua wachezaji wakati wa mechi au kipindi cha mvua kubwa.

Mabomba ya plastiki yaliyozungushwa chini ya uwanja huo yana urefu wa Kilomita 37 kama yatanyooshwa moja kwa moja. Ukubwa wa pitch ya Old Trafford goli hadi goli ni mita 105 na upana ni mita 68.

 Mara ya kwanza uwanja huo wa kuchezea wa Old Trafford kufanyiwa marekebisho ilikuwa ni mwaka 1999 baada ya Man Unted kushinda makombe matatu likiwemo la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kocha Sir Alex Ferguson akataka ufanyiwe marekebisho makubwa ili kuwapa nafasi ya wachezaji kupambana vema wakiwa nyumbani.

Klabu ikamwaga pauni 250,000  (zaidi ya Sh milioni 716) na ukarabati mkubwa ukafanyika na kuanzia hapo haukufanyika tena hadi msimu huo wa 2012-13.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic