September 13, 2017



Na Saleh Ally aliyekuwa London
UNAPOMZUNGUMZIA Thierry Daniel Henry katika suala la soka kunakuwa na mengi sana ambayo unaweza ukayakumbuka kama shabiki au mtu unayefuatilia mchezo wa soka.

Henry raia wa Ufaransa, hadi sasa anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora zaidi katika Klabu ya Arsenal akiwa amefunga mabao 228 tangu alipojiunga nayo mwaka 1999 hadi 2007 alipoamua kuondoka na kujiunga na FC Barcelona.

Henry ndiye mfungaji bora zaidi wa timu ya taifa ya Ufaransa baada ya kufanikiwa kuvunja rekodi ya gwiji, Michelle Platini pale alipofanikiwa kufikisha mabao 51 baada ya kuichezea Ufaransa mechi 123 za michuano mbalimbali ya kimataifa.

Arsenal wanaendelea kumkumbuka kwa mengi ikiwa ni pamoja na kuisaidia Arsenal kubeba makombe mawili ya Ligi Kuu England na matatu ya FA.

Kwa mashabiki na wapenda soka wataendelea kukumbuka kazi yake wakati akiwa mchezaji wakati sasa ameamua kuwa kocha baada ya kufundisha timu ya vijana ya Arsenal.

Kwa wachezaji wa Arsenal, kila anayeichezea timu hiyo hawezi kumsahau kutokana na kumbukumbu ya ubora wa Henry katika masuala kadhaa ya uamuzi.




Katika miaka yake nane aliyokaa Arsenal, miwili ya mwisho kabla ya kuondoka alikuwa ni nahodha wa timu hiyo, yaani msimu wa 2005-06 na 2006-2007 alipoamua kuondoka na baadaye Kocha Arsene Wenger akaamua kumvisha ‘kitambaa’, kinda Cesc Fabregas kutoka Hispania.

Wakati alipokabidhiwa unahodha, Henry aliingoza Arsenal katika mechi mbili tu kabla ya kubadilisha mambo na kuifanya Arsenal kuwa na utaratibu wake unaojitegemea hadi sasa.

Kawaida unapoingia katika vyumba vya kubadilishia nguo kwa asilimia 90 au 95, ukaaji hufuata namba. yaani kuanzia namba moja hadi inayokwisha.

Mfano, SALEHJEMBE ilitembelea Santiago Bernabeu unaomilikiwa na Real Madrid na ule wa Camp Nou mali ya FC Barcelona. Ndani ukaaji wake ni mpangilio kufuata namba bila ya kujali nani anakaa na nani.

Wakati SALEHJEMBE ilipotua kwenye Uwanja wa Emirates jijini London, mambo yalikuwa tofauti kwa kuwa suala la namba ndani ya vyumba hivyo halipo tena tangu mwaka 2005 baada ya Henry kuwa nahodha.

Unapoingia katika vyumba hivyo, utagundua kuna mpangilio wa namna zilizojichanganya bila ya kujali yupi anavaa namba gani na badala yake ukaaji unaanza na makipa, mabeki, viungo na baada ya hapo washambulizi halafu wanafuatia watu wa benchi.

Ukaaji huo unakwenda kama vile kikosi kinavyopangwa, yaani namba 1 hadi 11 halafu wanafuatia watu wa benchi. Kama utaangalia kwa kufuata jezi za mgongoni kama ilivyo kwa Barcelona, Real Madrid au hata Manchester United na timu nyingine utaona kuna tofauti kubwa kabisa.

“Hata hapa Emirates na kabla pale Highbury wachezaji walikuwa wakikaa kwa kufuata namba za mgongoni. Yaani inaanza namba moja na kuendelea na kila mtu jezi yake inawekwa kwenye sehemu kufuatana na namba ya mgongoni,” anasema James Harry mmoja wana historia wa Arsenal katika makao makuu ya klabu hiyo jijini London.



“Lakini sasa ni mambo tofauti na mfumo huu Arsenal ni kati ya timu chache sana duniani unazitumia. Unajua baada ya Henry kuchaguliwa unahodha, baada ya mechi mbili tu akaamua kuvunja utaratibu wa zamani.

“Alitoa wazo lake kwa Kocha Arsene (Wenger) na kumueleza aliona itakuwa vizuri kila kundi likakaa pamoja. Mfano, kipa namba moja na yule wa benchi wanaanza. Halafu mabeki, viungo na baadaye washambuliaji.

“Ndiyo maana mfano mzuri unaona Lacazette, Sanchez na Ozil au Walcott jezi ni tofauti lakini wanalazimika kukaa pamoja kutokana na mfumo huo wa Henry.

“Wenger alikubaliana nao baada ya kuona Henry ana hoja. Alisema kabla ya mechi, vizuri watu wakajadiliana vitu vinavyofanana. Mfano kipa na mabeki na viungo na viungo na washambulizi pia. Suala la kuunganisha litafanywa na nahodha au kocha.

“Henry aliamini kufuata namba si jambo baya kwa kuwa miaka yake yote ya soka alicheza akiwa katika mfumo huo, lakini aliona una makosa. Kwani wakati mwingine mchezaji aliye katika kikosi kinachoanza anakaa na aliye benchi, jambo ambalo halina faida sana kwa timu,” anasema na kuongeza:

“Pamoja na kubadilisha mfumo hivyo, Henry alichagua kubadili nafasi, kwa kuwa yeye ni nahodha akawa anakaa katikati ili inapofikia wakati wa kuzungumza, watu wanamsikiliza vizuri na kumuelewa.



“Kawaida wakati akizungumza alikuwa ni mtu makini na asiyetaka mchezo. Wote walimuelewa na asingejaribu kufanya utani kwa kuwa nahodha aliyepita kama Patrick (Vieira), hawakuwa watu wanaotaka utani hata kidogo.”



Kwa sasa Henry ni kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Ubelgiji chini ya Kocha Roberto Martinez na kazi yake imekuwa ikionekana ni nzuri kutokana na mwendo mzuri wa Ubelgiji ambayo tayari imefuzu kucheza Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic