September 27, 2017






Na Saleh Ally, aliyekuwa Manchester
WAKATI fulani, kiungo nyota wa Yanga mwanzoni mwa miaka ya 2000, Waziri Mahadhi, alibandikwa jina la Gaizka Mendieta. Hii ilitokana na umahiri wake na ufanyaji mambo kwa uhakika katika safu ya kiungo.

Mahadhi, alibandikwa jina hilo kutokana na umahiri wa kiungo nyota wa Valencia wakati huo. Huyo ni Gaizka Mendieta Zabala ambaye alikuwa akiichezea Valencia.

Mendieta alikuwa bora hasa na si mtu wa kubahatisha, kwani aliichezea Valencia mechi 230 na kufunga mabao 44. Wakati huo, Valencia ndiyo ilikuwa kiboko ya vigogo kama Real Madrid na Barcelona.



Baadaye Mendieta alijiunga na Lazio mwaka 2001 ambako alidumu kwa msimu mmoja akicheza mechi 20 na wao wakaamua kumtoa kwa mkopo FC Barcelona ambako alicheza mechi 33 na kufunga mabao manne.

Akiwa Hispania, sehemu aliyopata mafanikio makubwa ni wakati yuko na kikosi cha Valencia ambako alizoa makombe lukuki.

Alibeba Copa del Rey, Super Cup ya Hispania, Uefa Intertoto, na Uefa Champions League mara mbili akaingia fainali ingawa mara zote hakufanikiwa kubeba ubingwa.

Alipokwenda England alijiunga na Middlesbrough ambako alifanikiwa kubeba Kombe la Ligi, yeye ndiye akiwa kiungo mchezeshaji tegemeo.



Mendieta ni mchezaji mkubwa ambaye hata katika kikosi cha Hispania ambacho si kazi rahisi kupata namba na hasa katika nafasi ya kiungo, Mendieta alipata nafasi ya kucheza mechi 40 na kufunga mabao nane. Hii pekee inatosha kumtambusha kama mmoja wa wachezaji wa kiwango cha juu duniani.

Mendieta ni jina linaloheshimika katika soka la Hispania, lakini heshima yake iko juu duniani kote kutokana na heshima aliyoipata wakati anacheza.

Kwa sasa amestaafu na ukitaka kumuona ni wakati anaichezea timu ya wakongwe wa Barcelona kama ambavyo wiki chache zilizopita alipopiga chenga na kufunga bao la pili na kufanya mechi yao dhidi ya Manchester United kwisha kwa sare ya mabao 2-2.

Pamoja na heshima kubwa katika mpira, Mendieta sasa anafanya mambo mawili tu, kwanza ni biashara na pili ni kazi.

Kazi anayofanya ni kazi ya muziki. Sasa yeye ni Disco Joker, maarufu kama DJ au mchezesha muziki. Kazi ambayo amekuwa akiwashagaza wengi kwa kuwa sasa ni DJ wa kimataifa.



Amekuwa ni DJ wa kimataifa kwa kuwa anaalikwa katika matamasha mbalimbali makubwa ili kuchezesha muziki na sasa amekuwa mmoja wa MaDJ wanaolipwa vizuri zaidi duniani.

Udj imekuwa ni kazi anayoifanya kwa ufasaha mkubwa na sasa heshima yake imepanda kwa kuwa anaalikwa mara kadhaa katika matamasha makubwa ambayo hualikwa wale wanaoaminika au wazoefu hasa.

Mendieta anasema, kazi hiyo si rahisi na wakati anaanza wengi walidhani atakata tamaa.



“Niliipenda sana hii kazi tangu nikiwa mwanasoka na kazi yangu muda wote na wengi walidhani natania lakini nilijua sitaacha.

“Kwangu Udj imekuwa kama soka tu, maana ni kazi yangu, pia ni burudani yangu. Hivyo nafanya kazi hii huku nikiwa naifurahia maana inaniburudisha hata kabla ya kipato.

“Kweli soka ni namba moja wakati huo, sasa muziki ni namba moja kwangu maana ni burudani na kazi na ninaendelea kujifunza vizuri vingi ingawa wengine wananiita ni wa kimataifa. Lakini nitaendelea kujifunza zaidi,” anasema.

Pamoja na kazi hiyo ya muziki, Mendieta ameamua kuwa mfanyabiashara na vitu vingi vinasimamiwa na mkewe ambaye ni “mwanamke wa chuma.”

Mara nyingine, Mendieta anakuwa na mkewe na wanafanya kazi ya kuendesha migahawa mbalimbali ya kisasa katika maeneo mbalimbali ya Ulaya.

Sehemu mojawapo ambayo wanamiliki mgahawa wa kisasa ni jijini London, England. Lakini wanayo migahawa kwenye nchi nyingine kadhaa na imekuwa ikiwaingizia fedha za kutosha kuendesha maisha yao pamoja na familia yao.



Kuonyesha kweli yuko makini na kazi zake, pamoja na kufanikiwa kufungua migahawa zaidi ya minne, Mendieta ameonekana ni mwenye juhudi kubwa anayetaka mafanikio zaidi ya hayo.

“Mimi umri unakwenda, lazima nihudumie familia yangu. Kwanza nataka kuachana na dhana kuwa mchezaji akistaafu basi au mchezaji anatakiwa ategemee mambo ya soka tu,” anasema.

Tayari Mendieta ni fundi wa kulicharaza gitaa la besi na anataka kujifunza zaidi aina nyingine za magitaa ili kuujua muziki zaidi kwa kuwa hatanii.

“Niko makini na hili, nafanya ninachokipenda lakini naona ni sehemu itakayonibadilisha kabisa.”

Mendieta ni kati ya watu wataratibu kabisa kama utakutana naye. Hapendi kuzungumza sana lakini pia ni mtu anayependa kujumuika na watu hasa rafiki zake wa zamani.

Anasema mara nyingi asingependa sana kukumbuka mambo ya zamani yanayohusiana na mpira na hasa kipindi ambacho anaamini mambo yalikuwa magumu.

“Nilifanikiwa kweli, kulikuwa na changamoto nyingi lakini mpira umenifunza kuwa imara na ninayetaka kupambana kama ilivyo leo.

“Lakini sipendi kuuzungumzia mpira kila mara na wakati mwingine ningependa kuzungumzia kazi yangu ya sasa na kujifunza zaidi.

“Timu nilizopita mfano Valencia, mimi na wenzangu tulifanya vizuri kweli. FC Barcelona, Lazio na Middlesbrough. Kila sehemu ina jambo ambalo sitalisahau katika maisha yangu na kila moja limetofautiana.”




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic