September 26, 2017



Kocha Mkuu wa timu za vijana Tanzania, Kim Paulsen, amevutiwa na uwezo wa vijana wanaoibuka kila mwaka katika soka nchini na kusema tuna hazina ya wachezaji wenye uwezo wa kucheza mahala popote duniani.

Poulsen amewaambia waandishi wa habari leo Jumanne Septemba 26, 2017 jijini Dar es Salaam kwamba wamefanikiwa kuona uwezo wa vijana kwa wakati wote, lakini umahiri umekuwa ukiongezeka kwa kila timu mpya inapoitwa.

Kwa takribani mwezi mmoja, Kocha Poulsen akishirikiana na Oscar Mirambo walikuwa kwenye programu ya kuinoa Serengeti Boys mpya.

“Hii Serengeti mpya inayokuja, nayo ni bora kama ilivyo kwa wale waliopita. Bado naona kuna vipaji vikubwa sana. Ni kulea tu hawa vijana kazi ambayo tutaendelea nayo.”

Poulsen - Raia wa Denmark amesema kambi ya vijana 57 walioripoti na kufundishwa na makocha hao, wameonesha uwezo mkubwa, lakini kiufundi wamepunguza hadi hadi kubaki 27.

Amesema hao waliobaki watapangiwa kambi nyingine itakayoanza Novemba 19, 2017 na itafikia mwisho Desemba 19, mwaka huu  baada ya kuivunja kambi ya muda jana Septemba 25, mwaka huu.

Katika programu ya kambi hiyo mpya ya Novemba na Desemba, Kocha Kim ametaka angalau mechi moja ya kirafiki ya kimataifa huku akisisitiza apate timu ya nchi iliyowekeza hasa katika soka la vijana: “Ikiwezekana hata mbili.”

Akizungumzia kuhusu ujio mpya wa timu ya taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 - Ngorongoro Heroes, Kocha Kim amesema itaitwa kambini wakati wowote kuanzia Oktoba mwanzoni kwa kambi ya wiki tatu.

“Timu ya Serengeti Boys iliyopita ilifanya vizuri sana. Ni matarajio yetu hata hii itafanya vizuri, lakini hapa nataka nizungumzie ile iliyoshiriki fainali za AFCON u17 nchini Gabon…

“…kwa hiyo kambi itakayoitwa ya Ngorongoro Heroes, tutaita wale wote waliounda Serengeti Boys iliyopita. Hata wale ambao hawakubahatika kwenda Gabon tutawajumuisha kwa ajili ya kambi ya wiki tatu mwezi Oktoba,” amesema Poulsen.


Amesema kwamba sababu za kuita nyota wale wa Serengeti Boys katika Ngorongoro Heroes ni kuwapa nafasi ya kwanza wao kuonekana kama wangali na uwezo wa kupambana kama ilivyokuwa zamani na kwa wale wenye uwezo tu, ndio watakaochukuliwa,” amesisitiza.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic