September 22, 2017




Na Saleh Ally
NISINGEPENDA kumuona kiungo mkabaji wa Simba, Jonas Mkude akibaki nje kwa kuwa nina mambo kadhaa nilikuwa ninategemea kutoka kwake.

Mimi ni Mtanzania, ningependa kuwaona vijana wa Kitanzania wakifanya vizuri katika mpira na kuugeuza ajira na sehemu ya kuanza kufaidika nao ni hapa nyumbani.

Lakini ningefurahi kuona vijana wa Kitanzania wakifanikiwa kwa kuwa kama mchezaji kama Mkude anafanikiwa kufanya vizuri maana yake vijana wengine watahamasika kufuata nyayo zake na ikiwezekana nao wakafanikiwa.

Sasa kama Mkude akiwa benchi, hawezi kufanikiwa kama ambavyo ninatamani. Lakini kama atakaa benchi pia hawezi kuwahamasisha vijana wengine ambao wanatamani kufanikiwa au kupitia yeye wangeweza kuyatamani mafanikio.

Hivi karibuni kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusiana na Mkude, kwamba baada ya kuvuliwa unahodha, inaonekana kwamba amekuwa hapati nafasi ya kucheza na badala yake Simba inamtumia zaidi James Kotei raia wa Ghana.

Najua watu wanaweza kubanwa na ushabiki kuliko hata utaifa. Kwangu kidogo naweza kulidhibiti hilo, kama ni chaguo wakati wa utaifa basi ningekuambia kwamba Mkude anastahili kucheza kuliko Kotei.

Nitafanya hivyo kutokana na kutaka kuona Mkude anafanikiwa kama nilivyoeleza mwanzo lakini pia awe msaada kwa taifa letu hasa kama ataweza kuwa na kiwango cha juu. Usisahau ataisadia timu ya taifa lakini pia anaweza kupata nafasi ya kwenda kucheza nje ya nchi yetu na kuwa mmoja wa Watanzania wanaorudisha mafanikio na changamoto za matamanio ya mafanikio.

Lakini ukirudi katika uhalisia, ukamuweka pale Mkude na huku Kotei, jibu unajua utakalolipata. Kwamba Mghana huyo anaonekana ni zaidi ya Mkude hata kama itakuwa ni kidogo.

Huenda huu ndiyo wakati wa kuiheshimu ile kidogo ya Kotei kwa Mkude. Kile tunachoamini ni kidogo ndicho tunapaswa kukiheshimu pale Kocha Joseph Omog anapoamua kumtumia Kotei badala ya Mkude.

Lakini Mkude mwenyewe pia anapaswa kuiheshimu hiyo kidogo na kufanya kila linawezekana kwa maana ya  juhudi, kumsikiliza mwalimu ili kufanikiwa kuongeza kile anachokiona kimepungua. Akiongeze ili kuwa vizuri aweze kujisaidia na ikiwezekana kupata namba.

Wengi wamelalamika Mkude haanzi, wengi wameshauri angalau kuwe na uchezaji wa zamu. Lakini mimi nawakumbusha hizi ni mechi tatu na jana ilikuwa ya nne, kocha yupi anaweza kufanya hivyo dunia hii?

Mechi tatu, unaanza mzunguko? Tena unaanza mzunguko kwa mchezaji unayeona amecheza vizuri mechi mbili au tatu zote kwa zaidi ya asilimia 80. Ni jambo ambalo haliwezekani.

Lakini kinachovutia zaidi, baada ya zile mechi tatu za Simba (kabla ya jana dhidi ya Mbao). Mkude anaonekana amekua kisoka hata kama itakuwa ni kwa kiasi kidogo.

Anaonyesha ni mtu anayejitambua ambaye anaweza kufanya jambo fulani kwa ufasaha zaidi. Kwani alipoulizwa suala la kutocheza linavyomuumiza, akasema anajitahidi kupambana kupata namba.

Mkude amenifurahisha zaidi aliposema mambo mawili ndiyo yanamfanya asipate nafasi. Kwanza ni ushindani mkubwa wa namba wa kuwa na viungo wa ukabaji na mabeki.

Lakini ni suala la chaguo la mwalimu anataka nini kwa kipindi gani. Lakini yeye anaendelea kupigania namba kwa kuongeza juhudi ilikumshawishi mwalimu ampange.

Ukiangalia katika mazoezi ya Simba, kweli Mkude amekuwa akifanya mambo kwa juhudi kubwa na unaona ni mtu anayejielewa kwa kuwa hajatanguliza lawama badala yake anataka kubadili mambo kwa kupita katika njia sahihi.

Kama Mkude angefuata wanachokizungumza mashabiki, angeishapotea. Kama angeendelea kusikiliza wanacholalamika watu, huenda tayari angekuwa ameanza kusigana na Joseph Omog.

Lakini kama anajitambua, maana yake anapambana kupata kile kinachoonekana ni kidogo amezidiwa na Kotei.

Simba sasa ina kikosi kipana. Kuwa na kikosi kipana, maana yake ni kuwa na wachezaji bora, kuanzia 11 walio uwanjani hadi wale walio katika benchi. Sio kutoa SMG halafu uingize gobore, unatoa kitu, unaingiza kitu zaidi na hii ndiyo maana ya kikosi kipana. 

Hivyo ndani ya kikosi kipana, mafanikio si malalamiko badala yake juhudi na maarifa na Mkude anaonekana anajitambua.

Vizuri nasi tukajifunza kwamba, Mkude anajitambua nasi tunalalamika bila kuangalia uhalisia. Pia, uhalisia uwe ule ulio sahihi, kama Mkude hachezi sababu ya kuzidiwa kidogo na Kotei, siku anapoonekana kafanya vizuri, basi vizuri apewe hiyo nafasi kwa kuwa kwa Simba hata kama wana mipango yao lakini Mkude ni hazina ya taifa letu na itakuwa vema ikatumika. 


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic