September 22, 2017





Na Saleh Ally aliyekuwa Manchester
KATI ya mabeki bora kabisa Brazil wamewahi kuwapata ni Jose Edmilson Gomes de Moraes. Beki huyo hakuwa na utani uwanjani lakini maisha yake yamekuwa kimyakimya sana.


Edmilson amekuwa ni mmoja wa watu wepesi kusahaulika kabisa. Hii inatokana na ukimya wake na kuwa mtu asiyependa mambo mengi. Lakini kwa historia, yeye ni kati ya mabeki bora kabisa waliowahi kupata mafanikio makubwa.

Edmilson alipata mafanikio akiwa nchini Brazil, akafanya hivyo Ufaransa na pia Hispania ambako aliichezea FC Barcelona akiwa mmoja wa wachezaji waliofanya vizuri katika kikosi cha Kocha Frank Rijkaard.

Kama unakumbuka, kikosi hicho kilikuwa na nyota kama Ronaldinho, Samuel Eto’o, Deco, Cares Puyol na wengine wengi ambao waliifanya Barcelona kuwa gumzo na sasa hilo linaendelezwa.



SALEHJEMBE imefanikiwa kufanya mahojiano na Edmilson kuhusiana na masuala mbalimbali hasa baada ya kuwa amestaafu kucheza soka.

Edmilson aliyekuwa jijini Manchester, England ameiambia SALEHJEMBE kuwa pamoja na kuwa na umri wa miaka 41, furaha yake ya maisha bado imeendelea kubaki kuwa ni soka.

“Unaona leo ninakuwa na wachezaji mbalimbali wa soka ambao tulicheza nao miaka nenda rudi. Wakati mwingine ninaweza kuwa na wachezaji wa Barcelona. Lakini unaweza kuniona niko na wachezaji wa Lyon au Santos.

“Pia unaweza kuniona nikiwa na wachezaji wa timu nyingine pinzani. Furaha inayokuwepo ni kwa kuwa tunaheshimiana na kupendana na tunaishi maisha yanayokumbusha mengi ya zamani. Nafikiri nitabaki hivi katika maisha ya soka hadi mwisho wangu,” anasema.

Kuhusiana na wachezaji mbalimbali aliocheza nao, SALEHJEMBE ilitaka kujua Edmilson alikuwa akivutiwa na yupi kati ya Ronaldo na Ronaldinho kwa kuwa wote amecheza nao katika timu tofauti au timu moja.


EDMILSON AKIWA NA SALEH ALLY

“Hawa wawili ni kati ya wachezaji bora kabisa niliowahi kucheza nao. Wote ni bora na kila mmoja ana lake. Ronaldinho nilicheza naye Brazil na timu ya taifa ya Brazil, yeye nasisitiza ni bora na ilikuwa ni vigumu sana kumzuia asikupite.

“Mara nyingi nilipenda kuwa upande tofauti na Ronaldinho hasa tunapokuwa mazoezini. Hii ilikuwa inanisaidia kuwa vizuri zaidi kama ukilinganisha na nilivyokuwa. Kulikuwa na kazi ngumu sana kumkaba kwa kuwa ana ujuzi halafu ni mchezaji ambaye hauwezi kujua anatuliza mpira, anapiga au anaendelea,” anasema.

Alipoulizwa kuhusiana na Ronaldo ambaye alikuwa mshambuliaji wa zamani wa FC Barcelona na baadaye Real Madrid akiwa nyota, anasema;

“Ronaldo alikuwa wa aina yake, ni mchezaji ambaye hakuwa msumbufu sana kama Ronaldinho lakini ungeweza kumzuia Ronaldinho kufunga ila si yeye. 

“Ronaldo akiamua kufunga anafunga kweli, hakuwa akijua ubora wa beki badala yake alijua ubora wake yeye.

“Tulipokutana Barcelona na Madrid, nilipata shida sana. Lakini niliapa asingepiga mpira hata mmoja wa kichwa. Nilijua kama ni mipira ya chini sikuwa na uwezo pia wa kumzuia kupita kwa asilimia mia. Nilifanikiwa katika mipira ya kichwa.

AKIWA NA KIKOSI CHA BARCELONA


“Lakini mwisho alifunga. Hata mwisho wa mchezo nilimpongeza kuwa nimeshindwa kutimiza nilichotaka. Naye akanipongeza akisema, nilicheza vizuri na nilizuia mbinu zake nyingi ukiwemo mpango wa kufunga mabao ya kichwa.”


Kwa muonekano, Edmilson ni mchezaji kama mdhaifu hivi, lakini anaaminika kuwa mmoja wa mabeki wenye nguvu nyingi na imara katika mipira ya juu, yaani vichwa.

Ndiyo maana unaona alifanikiwa kubeba makombe makubwa akiwa na Sao Paulo ya kwao Brazil, alitwaa Copa CONMEBOL mwaka 1994 na 1996 akachukua Copa Master de CONMEBOL.

Kuonyesha ni beki imara zaidi, akatua Ufaransa ambako akiwa Lyon alichukua ubingwa wa League 1 mara tatu pia makombe mengine.

Alipojiunga na Barcelona mwaka 2004 hadi anaondoka mwaka 2008 alikuwa amebeba ubingwa wa La Liga mara mbili, Super Cup ya Hispania mara moja na Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa msimu wa 2005-06.

AKIWA NA KIKOSI CHA BARCELONA LEGENDS PAMOJA NA GUILY NA RONALDINHO.

Edmilson ni kati ya wachezaji waliobeba ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2002 wakati Brazil ilipoishinda Ujerumani kwa mabao 2-0 katika fainali, yote yakifungwa na Ronaldo de Lima.


Kwa sasa, Edmilson anaendelea na maisha yake nchini Brazil lakini muda mwingi amekuwa barani Ulaya hasa Hispania na Ufaransa akifanya biashara zake ingawa hakueleza hasa ni zipi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic