September 13, 2017




Na Saleh Ally aliyekuwa Manchester
KIUNGO Park Ji-sung ameichezea nchi yake ya Korea Kusini mechi 100 na kufunga mabao 13. Hii inamfanya kuwa mmoja wa wachezaji wenye mafanikio zaidi katika kikosi cha timu hiyo ya taifa ya nchi yake.

Alianza kucheza soka la kulipwa mwaka 2000 katika timu ya Kyoto Purple Sanga na aliendelea kuhama timu moja baada ya nyingine hadi mwaka 2014, alipotangaza kustaafu akiwa amecheza jumla ya mechi 318.

Katika timu zote alizozichezea, Manchester United ndiyo iliyompa mafanikio zaidi baada ya kujiunga nayo mwaka 2005, akitokea PSV Eindhoven ya Uholanzi ambayo alikuwa ameichezea mechi 65 na kufunga mabao 13.

Manchester United chini ya Kocha Alex Ferguson, aliichezea mechi 134 na kufunga mabao 19 akiwa mmoja wa wachezaji walioonekana ni muhimu kabisa kwa kocha huyo raia Scotland.

Wakati anatangaza kustaafu alikuwa amefunga jumla mabao 45, ambayo ukiangalia unaweza kusema ni machache sana. Lakini alikuwa ni mchezaji ambaye alitumiwa kwa kazi maalum tu hasa Manchester United.



Wakati fulani mmoja wa viungo bora kabisa kuwahi kuonekana katika soka la ushindani ni Andrea Pirlo, aliwahi kusema ukitaka kuishinda Manchester United, basi mkamate Park Ji-sung.

Alipotakiwa kufafanua, Pirlo alisema Mkorea huyo ndiye injini ya Manchester United na Kocha Ferguson amemtumia mechi karibu zote ambazo aliamini ni ngumu katika hesabu zake.

Kiungo huyo Muitaliano alisisitiza kuwa Ji-sung ni mchezaji aliyekuwa na nguvu kubwa ya kutibua mifumo ya utembeaji wa mpira wa timu yoyote halafu akaingia katika mfumo wa ushambulizi wa timu yake.

Huyo ni Pirlo, lakini Muitaliano, Gennaro Gattuso aliwahi kumuita  Park kama “Mchezaji asiyeonekana”.

Gattuso alikuwa akimaanisha Ji-sung anaonekana ni mchezaji wa kawaida sana Manchester United inapocheza. Lakini anakuwa msaada mkubwa sana timu hiyo inapocheza uwanjani.



Gattuso alisisitiza, ukitaka kujua umuhimu wa mchezaji huyo. Basi cheza mechi ambayo naye yupo uwanjani wewe ukiwa mpinzani.

Kwa hesabu, inaonyesha alikuwa katika kundi la kwanza la wachezaji waliokuwa wakitegemewa na Kocha Alex Ferguson.

Championi kwa mara nyingine, kimekuwa chombo cha kwanza cha habari kufanya mahojiano mafupi na Park.

Mahojiano hayo mafupi kwenye Uwanja wa Old Trafford jijini Manchester, yalifanyika huku Park akiwa na binti yake pamoja na mkewe ambaye ni mwanamitindo wa Kikorea.

Park anasema ameamua kubaki Manchester na angependa familia yake iendelee kubaki katika jiji la Manchester kwa kuwa kwake sasa ni kama nyumbani.

“Kweli natokea Korea Kusini, lakini Manchester imekuwa ndiyo nyumbani. Familia inafurahia kuwa hapa na kama wao wanafurahi, mimi nafurahia zaidi.



“Nafikiri nitabaki hapa kwa kuwa ninaweza kuishi nikiwa na amani na watu walionizunguka ni waungwana na wanaonifanya niwe na furaha,” anasema.

Kuhusiana na masuala ya soka, Park anasema anapenda kujiendeleza zaidi. Anaweza kusoma mambo ya ukocha na angependa kuanza kwa kufundisha soka Ulaya na baadaye afanye kazi hiyo katika nchi nyingi za Asia ikiwemo kwao Korea Kusini.

“Naamini ukijifunza soka katika nchi za Ulaya kuna mafanikio makubwa zaidi ukifananisha na kwingineko.

“Napenda kujifunza zaidi na kama nitaendelea na kufanikiwa naweza kufundisha nje ya Ulaya kama sehemu ya kuleta mabadiliko kisoka katika nchi ambazo zinachipukia,” anasema.

Alipoulizwa kama ana kipi anachokifanya ili kusaidia michezo na hasa soka katika nchi aliyotokea, anasema:

“Si kwamba sitarudi Korea Kusini, ninakwenda na kule nyumbani, nina makazi. Hata kesho unaweza kusikia niko huko. Kuna mambo mengi nasaidia kwa ajili ya michezo kupitia taasisi yangu na zile ambazo ziko tayari kufanya kazi na mimi.”

Kuhusiana na namna Ferguson alivyokuwa akimtumia katika kikosi chake. Park anasema, alikuwa akivutiwa.

“Nilikuwa nacheza tofauti, Ferguson akataka nicheze tofauti. Mwanzo ilikuwa shida lakini baadaye ikawa nikawa napenda zaidi.

“Alikuwa na maelekezo ambayo ukiyafuata utaona tofauti kubwa sana. Niliimarika zaidi kwa kuwa niliufuata mfumo namna ulivyo.”


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic