October 20, 2017



NA SALEH ALLY
SIKU chache zimepita tangu Kampuni ya GF Truck and Equipment Ltd kuamua kutoa basi kwa Mbao FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mbao FC ni timu iliyoanzishwa mjini Mwanza miaka michache iliyopita chini ya wafanyabiashara wakubwa na wale wadogowadogo wa Mbao jijini Mwanza. Wao walifanya kama burudani kwao baada ya uchovu wa kazi zao lakini imefikia sasa kuwa timu ya Ligi Kuu Bara.

Tangu Mbao FC ipande Ligi Kuu imekuwa ni moja ya timu zinazofanya mambo yake kwa mpangilio mkubwa na sasa ni gumzo kwa kuwa imeaminika na kujipambanua kuwa moja ya timu zinazotengeneza vipaji.
Kama ulivyoona msimu uliopita, Mbao FC imeuza wachezaji katika timu mbalimbali zikiwemo Azam FC, Simba na baada ya hapo kukawa na hofu kwamba huenda ikashindwa kurejea katika kiwango chake msimu huu.

Hadi baada ya mechi sita tayari Mbao FC imekusanya pointi sita ukiwa wastani wa pointi moja kila mechi na iko katika nafasi ya tisa. 

Hauwezi kusema iko katika nafasi mbaya sana lakini inatakiwa kujitutumua zaidi na imeonyesha pamoja na kuondokewa na wachezaji wengi, bado ina nafasi ya kufanya vizuri kwa imecheza na Simba ambayo inaonekana ina kikosi bora kabisa, imewatoa jasho na matokeo yamekuwa sare ya mabao 2-2.

Kumbukumbu zinaonyesha timu nyingi zilishindwa kufanya vizuri kutokana na kukosa nauli na wadhamini wengi walikimbilia katika timu kubwa pekee kama Yanga na Simba au Azam FC na Mtibwa Sugar au Kagera ambazo tayari zilikuwa na uhakika wa udhamini.



Sasa mambo yameanza kubadilika tangu misimu miwili iliyopita na inaonekana mambo yanazidi kuwa mazuri kwa kuwa imani ya baadhi ya wadhamini inazidi kusogea chini na wanaendelea kuingia kutoa fedha na kuzidhamini hata klabu ambazo zilikuwa zinaonekana ni ndogo.

Unakumbuka Cowbell wameidhamini Ruvu Shooting ambayo awali ilionekana ni timu ya jeshi hivyo hakukuwa na haja ya kuwa na mdhamini. Udhamini wao ulikuwa ni sehemu ya mapinduzi makubwa katika mpira ingawa wengi tumeuchukulia kama kawaida.

Unakumbuka kampuni ya Bin Slum ilipozidhamini timu Mbeya City, Stand United na Ndanda FC kwa wakati mmoja.

Sasa tumeona kampuni kubwa ya ubashiri kama SportPesa imeingia kuzidhamini Yanga na Simba na Singida United ambayo ni maarufu. 

Angalia timu kama Majimaji, nayo imepata udhamini wa Sokabet, kampuni nyingine ya ubashiri pia ambalo ni jambo zuri kwa kuwa linazidi kuonyesha thamani ya mchezo wa soka.

Usisahau, Benki ya NMB iliingia kuwadhamini Azam FC na hadi sasa wao ndiyo wadhamini wakuu wa klabu hiyo. Wameingia kudhamini wakiwa wanajua kwamba timu hiyo ingeweza kudhaminiwa na bidhaa nyingi za Bakhresa ambaye ni mmiliki wa klabu hiyo.

 Lazima tukubali kwamba wadhamini wameonyesha wanauthamini mchezo wa soka ndiyo maana unaona kampuni kama GF Truck and Equipment Ltd wanaamua kutoa basi kwa timu kama Mbao FC wakati zamani mabasi walipewa Yanga na Simba au ungewaona nalo Azam FC au timu za majeshi.

Kuna jambo la kujifunza zaidi kwamba, kama wadhamini wanakubali kughalimia timu za mpira au kujiingiza katika soka, maana yake wameona jambo au wameona kuna faida.

Sasa hao wanaoonekana ni wenye faida au watengenezaji wa faida wanalitambua au kujitambua?

Hapa kuna mambo mengi ya kufanya kuhakikisha wanazidi kuongeza thamani yao na kutengeneza ushawishi wa wadhamini kujitokeza zaidi ambao watawaingizia kipato zaidi na wao waweze kupunguza ukali wa gharama za uendeshaji.


Hali kadhalika, lazima kuwe na mfumo mzuri wa kufanya mambo kiuweledi ili kuwaridhisha wadhamini badala ya kuwakasirisha na kuona kama fedha wanazotoa ni msaada. Lazima mjue wao wanafanya biashara, basi biashara ifanyike.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic