NA SALEH ALLY
NILIWAONA mashabiki wengi wa soka waliojitokeza kwenye Uwanja wa Boko Veterani nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam wakiwa na shauku kubwa ya kuwaona nyota waliotokea nje ya Tanzania.
Mashabiki hao walijitokeza kuhudhuria mazoezi ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambayo inajiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Malawi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, kesho.
Hakika mashabiki walijitokeza kwa wingi na hamu kuu ya kutaka kuiona timu yao ya taifa inafanya mazoezi na bahati yao nzuri kwa kuwa hakuna uwanja ambao wangeweza kujificha sehemu na kuendelea na mazoezi hivyo walikuwa katika eneo linalifikika na wao wangeweza kuwaona.
Wakati wanaendelea na mazoezi, mashabiki wengi waliojitokeza walionekana na hamu kuu ya kuwafikia au kuwakaribia wachezaji wawili zaidi ambao ni Saimon Msuva na Mbwana Samatta.
Lakini wako ambao walionyesha shauku yao pia kwa beki Abdi Banda anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Baroka FC ya nchini Afrika Kusini.
Samatta anaitumikia KRC Genk ya Ubelgiji na Msuva anaichezea Difaa Al Jadid ya Morocco na wote wameonyesha mafanikio makubwa ambayo huenda Watanzania wengi wasingetarajia.
Wakati Samatta anakwenda msimu wa pili akiwa Ubelgiji ambako sasa ni tegemeo la ushambulizi katika kikosi cha KRC Genk, Msuva naye ameonekana kuwa tegemeo na chanzo au mfungaji wa mabao ya Al Jadid huko Morocco.
Hali hiyo na kwa kuwa ni washambulizi, ndiyo imewafanya mashabiki kuwa na hamu kubwa ya kuwasogelea na ikiwezekana kupiga nao picha kwa ule mtindo wa “selfie”.
Ilikuwa raha zaidi kwa kuwa Samatta na Msuva nao walitoa nafasi kwa mashabiki wao hao kuhusiana na ombi la kutaka wapige nao picha.
Baada ya Samatta na Msuva kutoa nafasi hiyo baada ya mashabiki hao kuwaomba, kwa kiasi fulani mashabiki walikuwa kama wamechanganyikiwa kutokana na furaha waliyokuwa nayo.
Mimi nilisikia faraja kwa kuwa niliwaona Watanzania hao namna ambavyo wanasikia raha kupata nafasi ya kupiga picha na nyota kutoka nyumbani kwao Tanzania lakini wanapambana kusaka maisha nje ya nyumbani.
Hii ilinifanya niendelee kuamini zile hisia zangu za miaka nenda rudi kwamba siku moja inawezekana na sisi tukawa na timu ya taifa, kuanzia namba moja hadi 11 na benchi wote wanatokea ughaibuni. Mwisho wa mechi, mashabiki wanachagua wa kupiga naye picha kutoka FC Barceloma, Real Madrid, Manchester United, Arsenal, PSG, Bayern na kadhalika.
Najua inawezekana kabisa na ndiyo maana naamini selfie ya Samatta na ile ya Msuva, bado hazitoshi na Watanzania wapenda soka wanastahili kupata nyingine hata kama ziko nyingine chache za kina Banda na Farid Mussa anayecheza Tenerife ya Hispania.
Inawezekana wengine wakawepo tena wengi lakini si jambo rahisi la kuibuka tu kama uyoga. Badala yake wachezaji walioko kwa sasa hapa nyumbani, wanatakiwa kujituma na kuonyesha nia ya kutaka kutoka kimafanikio na mambo yanawezekana hata inapokuwa nje ya Tanzania.
Wanaokwenda nje ya Tanzania, wanakutaka na ushindani tofauti usiofanana na tulionao kutokana na utamaduni na mazingira lakini wanakuwa na nafasi zaidi ya kujiendeleza kimafanikio.
Kama ambavyo Samatta ameonyesha kufurahishwa na idadi ya Watanzania wanaocheza nje ya Tanzania kuongezeka na ameeleza kuwa kikosi chenye changamoto ya wanaocheza nje kwa wingi kitaongeza mabadiliko.
Anaweza akawa hajaanika kila kitu lakini Samatta anaelewa tofauti ya nyumbani na huko anakofanya kazi. Jitumeni, achaneni na kuamini kuwa Simba, Yanga na Azam FC ndiyo mwisho wa mafanikio.
0 COMMENTS:
Post a Comment