MACHAKU |
Kocha Mkuu wa Lipuli FC, Selemani Matola, ameeleza kuwa, yupo mbioni kuachana na mchezaji wake, Salum Machaku kutokana na utovu wa nidhamu anaoufanya.
Awali, uongozi wa Lipuli uliwasimamisha wachezaji Malimi Busungu na Machaku kutokana na utovu wa nidhamu waliokuwa wakiuonyesha katika klabu hiyo.
Akizungumzia suala hilo; Matola amesema kuwa, katika ripoti yake aliyoiwasilisha kwa uongozi, kuna majina kadhaa ya wachezaji ambao amependekeza kuachana nao akiwemo Machaku.
“Nimewasilisha jina la Machaku kwa uongozi kuweza kuachana naye, simtaki aendelee katika timu kwa kuwa ni mtovu wa nidhamu na hastahili kuwepo kwenye timu.
“Awali alikuwa yeye na Busungu, lakini mwenzie ameonekana kujirekebisha hivyo nimeamua kumuacha aendelee, lakini kwa upande wa Machaku hana nafasi tena ya kuendelea katika kikosi chetu.
“Nadhani akiendelea kukaa katika timu atawaharibu wachezaji wengine kwani nidhamu yake ni mbovu, hivyo sihitaji kuendelea kubaki naye, kwa sasa nipo katika mchakato wa kutafuta wachezaji wengine kwa lengo la kuimarisha kikosi ambapo nimepanga kusajili wachezaji watano katika usajili wa dirisha dogo,” alisema Matola.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment