November 10, 2017



Na Saleh Ally
KUNA ile methali “Lililopo ndiyo lisemwalo”. Maana yake kwamba linalozungumzwa kwa wakati husika linastahili kuzungumzwa kwa kuwa ndilo lililopo wakati huo.

Wakati wa kuchagua lililopo, kila mmoja anaweza kuona ni tofauti lakini hata kama unaweza kuwa unaona tofauti, mimi naweza kukumbusha ulilolisahau na tukalizungumzia sote na ukaona lilistahili kuzungumziwa sasa.

Kama unakumbuka, beki Mwinyi Haji wakati anajiunga na Yanga akitokea Zanzibar, Yanga ilikuwa ikimtegemea beki Oscar Joshua katika beki ya pembeni kushoto.

Mashabiki kadhaa wa Yanga walikuwa hawamkubali kabisa Joshua kutokana na anavyocheza. Mara nyingi hakuhusika na makosa kutokana na uchezaji wake wa kibabe lakini alikuwa makini sana.

Alipotua Mwinyi, alionyesha ni mtu mwenye hamu kubwa ya kutaka mafanikio na kweli aliitaka hasa namba ya Joshua. Baada ya muda, Mwinyi aliichukua namba hiyo na gumzo likawa yeye kutokana na namna alivyokuwa akicheza.

Kama unakumbuka, misimu miwili iliyopita, Yanga ilichukua ubingwa ikiwa na uhakika na mabeki wawili wa pembeni, Juma Abdul kulia na Mwinyi kushoto waliifanya Yanga kuwa hatari na isiyokamatika.

Mwinyi alitamba hata kimataifa kwa kuwa Yanga ilifanya vizuri zaidi hadi kuingia katika hatua ya makundi, Kombe la Shirikisho Afrika huku ikiwa imechukua ubingwa wa Tanzania Bara na ule wa Kombe la Shirikisho.

Baada ya hapo, kukaanza kuzuka taarifa mbalimbali zikiwemo zile Mwinyi amejiingiza kwenye ulevi lakini yeye akaibuka na kuzipinga na mwisho ilionekana kama vile kuna watu tu walikuwa hawamtakii mema.

Kilichonishangaza ni benchi la ufundi la Yanga kuamua kutafuta nguvu nyingine katika beki ya kushoto. Uamuzi wa kufanya hivyo maana yake kocha hakuwa akiridhika na hali ilivyo. Huduma aliyokuwa akipata haikuwa ikijitosheleza, hilo ndiyo jibu sahihi bila ya kuzunguka.

Nilianza kujiuliza hivi; kama ni hivyo, vipi yale maneno, yalikuwa na ukweli watu wakayafukia au ilikuwaje? Lakini kama si kweli vipi inaonekana Yanga haikupata huduma ya kutosha hadi kutaka mtu wa kufanya kazi hiyo ya ziada.

Kuingia kwa Gadiel Michael, moja kwa moja kukamng’oa Joshua. Ukawa ndiyo mwisho wake Yanga na akabaki Mwinyi na mgeni huyo ambaye si mchezaji wa kigeni, ametokea Azam FC tu pale Chamazi na mara kadhaa amekutana na Yanga akiwa na timu yake hiyo ya zamani.

Hakuna haja ya kuzungumza maneno kwa sasa Mwinyi ni mchezaji wa benchi. Nafasi yake ndani ya kikosi cha Yanga analazimika kuigombea tena kama ambavyo Joshua alivyokutwa naye na baadaye akaanza kuipigania tena.

Kilichomtokea Joshua, sasa kinamtokea Mwinyi na unapaswa kujiuliza kama nafasi alikuwa nayo mkononi, kwa nini leo analazimika kupigania? Au kama alikuwa nayo, vipi Yanga ililazimika kumtafuta Gadiel na si kumuacha yeye aendelee kuitumikia na benchi la ufundi liangalie nafasi nyingine? Hata kama atakataa, tatizo namba moja ni yeye kwa kuwa Yanga haikuridhika na huduma yake.

Sasa analazimika kugombea nafasi aliyokuwa nayo mkononi mwake na akashindwa kuilinda. Kama ni kupokezana, inaonekana kazi ya Gadiel imekuwa bora zaidi ya kwake na kwa kuwa Mwinyi aliachia tundu la Gadiel kuingia mwisho amechukua ufalme.

Kinaweza kuwa ni kipindi kigumu kwa Mwinyi lakini anaweza pia kujaribu kuonyesha kwamba hakuna lolote baya na maisha yanaendelea vizuri. Ukweli ni mtu mwenye hofu ambaye anapambana kurudi katika nafasi ambayo aliichezea.

Kilichomtokea Mwinyi kimewatokea wachezaji wengi na ubaya wengi wamekuwa wakishindwa kujipima hata baada ya tatizo na badala yake huishia kuangusha lawama kwa wengine au wale wanaowaongoza kwa mambo mengi kwamba hawawapendi na kadhalika.

Kilichomtokea Mwinyi kimewatokea watu hata katika maisha ya kawaida ya kila siku. Wamekuwa wakijisahau kila baada ya mambo kuwaendea vizuri na wakaona nafasi walizonazo watakuwa nazo milele bila ya kuonyesha wanastahili kuzilinda.


Maana yangu kilichomtokea Mwinyi, hata wewe kinaweza kukutokea wakati wowote ule. Hivyo ni vizuri kukijali ulichonacho, onyesha ubora kadiri ya uwezo wako na pambana uweze kufanya bora na zaidi ya bora kila mara badala ya kusubiri ulichonacho kikuponyoke halafu uanze kulaumu.

1 COMMENTS:

  1. Asante sana nimekuelewa vizuri sana, MUNGU akubariki mno.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic