November 6, 2017




NA SALEH ALLY
NINA kumbukumbu nyingi sana kuhusiana na mchezo wa ngumi, iwe ni zile za ridhaa au za kulipwa na mara nyingi nililazimika kutembea umbali mrefu kuhakikisha nafika eneo ambalo mapambano ya ngumi yanachezwa.

Nililazimika kutembea kwa miguu kwa kuwa sikuwa na nauli ya kufika eneo husika lakini ukweli nilitaka kutimiza ndoto ya kufanikisha kuandika kuhusiana na mchezo huo ambao sasa naweza kusema si kupoteza mwelekeo tu badala yake unakwenda shimoni kabisa.

Mwanzoni mwa miaka ya 2000, hasa 2001, mabondia hawakuwa wakilipwa fedha nyingi sana na ilikuwa inashangaza kusikia bondia kapewa Sh milioni moja kwa pambano moja.

Kipindi cha familia ya akina Matumla wakiongozwa na kaka yao Ali Matumla na baadaye Rashid Matumla, ilikuwa raha sana. Walikwenda kwa kipindi kirefu wakiuchangamsha mchezo huo huku wakiendelea kuitangaza Tanzania kila kona kwa kushinda mataji mbalimbali hata nje ya Tanzania.

Rashid Matumla alishinda mataji ya dunia mara mbili nje ya Tanzania, akiwatwanga wazungu na kuwaonyesha Tanzania ilivyo na vipaji vya mchezo huo. Alifanya hivyo tena hapa nyumbani, siku moja yeye alipomchakaza mzungu na mdogo wake Mbwana Matumla akafanya hivyo.

Ndani ya Tanzania, ushindani ulikuwa mkubwa kati ya Rashid Matumla dhidi ya Joseph Marwa, mwanajeshi aliyekuwa anapigana kisomi, mambo yake yalikuwa taratibu lakini kwa uhakika. Baadaye ushindani huo ukahamia kwa Maneno Oswald, wakati huo akiwa maarufu kama Mtambo wa Gongo.

Matumla na Maneno wote ni watoto wa Keko, ushindani wao ulianzia katika kitongoji hicho, ukapaa hadi Dar es Salaam yote na baadaye nchi nzima. Hakuna aliyekuwa anakataa kuwa mchezo wa ngumi ulichukua namba mbili iliyokuwa ikishikiliwa na mchezo wa kikapu.

Angalia baadaye ushindani wa ngumi ulipohamia kati ya Keko na Kinondoni, kambi ambazo zilishindana kwa muda mrefu kabla ya ushindani huo kuwa wa mkoa, yaani Dar es Salaam dhidi ya Morogoro hasa baada ya kuibuka kwa Francis Cheka.

Hayo yamepita, sasa ngumi unazishindanisha nani na nani, kitongoji kipi na kipi au mkoa upi na upi? Kila kitu sasa badala ya kuwa mikononi na ulingoni kimehamia midomoni na mapromota wa ngumi wamekuwa chanzo kikubwa kwa kuwa wamekuwa bora midomoni badala ya utendaji.

Mara nyingi nimewasikia mapromota wakilalamika kutowekewa mazingira mazuri katika suala la uandaaji mapambano, jambo ambalo wanadai linawasababishia hasara na wao ni watu muhimu, jambo ambalo nakubaliana nalo kwamba wanatakiwa kuwekewa mazingira mazuri.

Kama watawekewa mazingira mazuri ili waweze kufanya kazi yao vizuri, nani atawasaidia wao kubadilika na kuwa watu wenye malengo ya kufanya jambo au kuandaa mapambano kwa kufuata weledi?

Suala la kufuata weledi au kuangalia pambano moja linaweza kutengeneza pambano jingine bora au kuendeleza mchezo wa ngumi za kulipwa ndiyo bora zaidi na mapromota wanapaswa kulipa kipaumbele.

Ajabu ninachokiona, kila promota hataki kuona promota mwingine anafanikiwa. Kila mmoja hataki kuona mwenzake anaingiza fedha na hili jambo limewafanya kuwa watu wasio na mwelekeo na mwisho lawama zao wanaziangusha kwa watu wengine vikiwemo vyombo vya habari kwamba vinapendelea tu mchezo wa soka.

Kuna kipi kizuri cha kuripoti katika ngumu kama majungu na utovu wa nidhamu ndiyo vimegeuka kuwa michezo. Kila mmoja anajua kuzungumza kuliko mwingine, promota na promota hawapendani sababu ya wivu utafikiri mchezo huo ni wa mapenzi!

Shirikisho moja nalo halipendi jingine lifanye vizuri na promota huyu anaelewana na viongozi wa shirikisho hili na hawapendi wa shirikisho hili. Basi ni chuki tu ndiyo imetawala na kuongoza maisha ya watu wa ngumi jambo ambalo ni uzuzu na ulimbukeni wa kupindukia.

Mabondia wana vipaji, wanapaswa kupata mameneja bora wenye malengo na wao wawasikilize. Mapromota nao wanapaswa kuwa watu wanaolenga kuingiza kipato lakini wajue kuuendeleza mchezo huo ndiyo jambo bora zaidi.


Chuki za kipuuzi kila kukicha, kila promota akitamba kwa ubora wa maneno kuliko kazi? Nani kati yao amefanikiwa zaidi ya kuuzorotesha mchezo wa ngumi za kulipwa na sasa lawama wanaziangushia kwa wengine? Hovyo kabisa na huu ndiyo wakati wa kubadilika.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic