December 6, 2017




Na Saleh Ally, aliyekuwa Ujerumani
JUZI Jumamosi, Jay Jay Okocha wakati akifanya mahojiano ya ana kwa ana na Gazeti la Championi, alieleza mambo mengi kuhusiana na kiungo nyota wa Brazil, Ronaldinho ambaye alicheza naye soka wote wakiwa PSG.

Kumekuwa na mijadala mingi kuhusiana na nyota hao wawili ambao walikuwa na uchezaji uliofanana kwa kiasi fulani na watu wamekuwa wakiamini mmoja alimuiga mwingine na mwingine ndiye aliyeanzisha.

Lakini Okocha alielezea namna Ronaldinho alivyotua PSG ya Ufaransa wakati huo akiwa kinda kabisa na yeye alikuwa kati ya watu waliompokea. 

Pamoja na maelezo hayo, Okocha aliulizwa swali kuhusiana na uraia wake wa Uturuki na kuanza kufafanua kuhusiana na uamuzi huo wa kuwa raia wa nchi hiyo wakati akicheza soka katika moja ya klabu kubwa ya Fenernahce.



SALEHJEMBE: Kuna taarifa una uraia wa Uturuki na jina lako ni Muhamet Yavuz, hii imekaaje?
Okocha: (kicheko) Kweli nina uraia wa Uturuki, nimekuwa nao kwa muda mrefu hadi sasa nimeendelea kuwa raia wa Uturuki. Pasi yao ya kusafiria huwa siitumii na niliendelea kubaki na ile pasi ya kusafiria ya Nigeria ambayo nimekuwa nikiitumia.


SALEHJEMBE: Sababu ipi imefanya usiitumie wakati uliichukua?
Okocha: Hakuna maelezo mengi sana, mimi najivunia kuwa Mwafrika. Ila hawa jamaa wakati nacheza Fenerbahce walikuwa wakinipenda sana. Unajua Waturuki wanapenda sana mpira na kama ukifanya kazi yako vizuri, mapenzi yao kwako hayana hata kificho. Hivyo ikafikia ili kurahisisha mambo kadhaa yasiwe na maswali mengi kwangu kama raia basi nichukue uraia, nikafanya hivyo.

SALEHJEMBE: Sasa vipi, ulikuwa ukitumia jina Muhamet Yavuz na wewe ni Austine Okocha?
Okocha: Kawaida kuwa Mturuki lazima uwe na jina la Kituruki, huo ni utaratibu na mimi nilifanya hivyo. Kwa sasa siitumii kama nilivyokueleza lakini ni sehemu ambayo naweza kusema ina kumbukumbu nyingi sana katika maisha yangu ya kisoka.


SALEHJEMBE: Ulimshawishi Iwobi kuchezea Nigeria badala ya England. Kawaida kila mtu angependa acheze England, labda ulifanyaje kumshawishi?
Okocha: Ilikuwa kazi ngumu sana hasa mwanzoni kumshawishi Iwobi akubali kuichezea Nigeria badala ya England kwa kuwa alikuwa na nafasi ya kucheza England. Lakini kwake kwa kuwa alikuwa na mtu ambaye angetamani kuwa kama yeye, kidogo ikasaidia.

SALEHJEMBE: Nini kilikufanya umshawishi acheze Nigeria badala ya England? Utaifa wa Nigeria?
Okocha: Suala la utaifa linaweza kuwepo lakini halikuwa namba moja kama nilivyoangalia mafanikio ya Iwobi mwenyewe. Kitu cha kwanza niliangalia wachezaji walionao England hasa kwa umri wake yeye, kidogo nilijua kutakuwa na ugumu kwake na mimi nilitaka apate nafasi ya kucheza Kombe la Dunia akiwa bado kinda.



SALEHJEMBE:Uliwahi kusema, mwishoni haikuwa vigumu tena kumshawishi, kidogo inachanganya?
Okocha: Mwishoni hasa baada ya kuzungumza naye na utaona hata yeye alianza kuona nilichomueleza kinaeleweka. Hivyo akawa na mawazo yaleyale kama yangu na urahisi ukaongezeka kwa yeye kuamua kuchezea Nigeria badala ya England.


SALEHJEMBE: Ukiachana na timu ya taifa, ilionekana vizuri ungemchukua Iwobi acheze Bundesliga badala ya EPL maana wewe umekulia Bundesliga na kupata mafanikio makubwa?
Okocha: Ningeweza kufikiri hivyo, lakini unaona katika umri mdogo tayari kocha (Arsene Wenger), anamuamini na anampa nafasi jambo ambalo sikulitegemea. Ninaamini mambo yataenda vizuri zaidi na zaidi. Angalia sasa anacheza hadi timu ya taifa ya Nigeria, kucheza Afrika ni vigumu zaidi ya Ulaya na anafanikiwa.
Championi: Haujawahi kusikika angalau unakwenda kuwa kocha?
Okocha: Nafikiri si rahisi kila mmoja wetu anaweza kuwa kocha, hili ni vizuri kulijua. Nilitamani zaidi siku moja lakini pia nimekuwa na hofu sana kuhusiana na masuala ya viongozi, wengi si wakweli au waaminifu au wanaotaka kusaidia na wamekuwa wakiwakwamisha makocha na kuwaangushia mzigo.

SALEHJEMBE: Mpira wa Ulaya uko tofauti sana na mpira wa Afrika na utaona hata viwanja vyake viko karibu na mashabiki na wamekuwa wakitoa lugha chafu hasa kwa wachezaji wenye asili ya Afrika, ulipambanaje na hili?
Okocha: Kuna ugumu sana, kweli mashabiki wanatoa maneno machafu na mengine ni ya kudhalilisha. Lakini kama mchezaji unakuwa unaelewa kwamba hawa wamekuja hapa kwa ajili ya kuangalia mechi na wamelipia. 
Wanaokuchanganya wangefurahi iwe hivyo, ninachofanya ni kutowapa hiyo nafasi na badala yake naendelea na malengo yangu.


SALEHJEMBE: Katika ligi ulizocheza, ipi ilikupa ugumu sana wakati ukicheza?
Okocha: Hakuna ligi rahisi, kila moja ina aina yake na utaratibu wake lakini ushindani upo kila sehemu, ugumu na raha upande mwingine na ndivyo ilivyokuwa.


SALEHJEMBE: Ile ‘clip’ yako ukimnyanyasa Roy Keane wa Manchester United ambaye nusura akuvunje mguu, unaikumbuka na labda umewahi kuiangalia hivi karibuni?
Okocha: Roy Keane (kicheko)….


ITAENDELEA…

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic