December 1, 2017





NA SALEH ALLY
KUMEKUWA na maandalizi makubwa kuhusiana na michuano ya Cecafa ambayo imepangwa kufanyika nchini Kenya.

Michuano hiyo inaanza Jumapili katika makundi mawili na inaonekana Zanzibar na Tanzania Bara wamejiandaa vilivyo kuhakikisha wanafanya vizuri.

Ukitulia utasikia kuhusiana na michuano hiyo, kila upande ukizungumzia maandalizi na kujigamba kufanya vizuri ndani ya michuano hiyo.

Michuano hiyo kwangu huiona kama haina maana sana na iko kwa ajili ya watu wachache na si mpira wa Afrika Mashariki na Kati.

Kati ya watu ambao nawaona ni chanzo kikubwa cha kudorora michuano hiyo ni Nicholas Musonye ambaye ameamua kuwa kiongozi wa maisha wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

Musonye amejiwekea ukuta, ameamua kubaki kama mmiliki wa Cecafa na kuendelea kufanya anavyotaka yeye na si kuangalia maendeleo ya mchezo huo katika ukanda.

Napinga sana hasa kwa viongozi wa mashirikisho ya soka katika ukanda huu ambao nao wanaona mambo yamekuwa ni kawaida tu na wanaonekana pia huenda wanaunga mkono hilo.

Kama wangekuwa hawaliungi mkono, basi wangelifanyia kazi. Cecafa inahitaji mawazo mapya ili kufanya mambo kulingana na wakati tulionao. Ninaamini wanaweza kulitafakari tena jambo hilo kwa kulifanyia kazi.



Jamhuri ya Muungano ya Tanzania inapeleka timu mbili katika michuano hiyo. Tanzania Bara na ndugu zao Zanzibar ambao ni wapinzani wakubwa wanapokutana.

Tanzania Bara itarusha karata yake kwa kuivaa Libya kama timu mwalikwa katika michuano hiyo. Hakika niwe wazi bila ya kupindisha mambo kwamba napinga kabisa kuiona Libya ikiwa katika michuano hiyo.

Huu ulikuwa wakati wa kuonyesha msimamo wa Kiafrika na kuwaonyesha Walibya kwamba wameshindwa kuonyesha uanadamu kwa kitendo walichowafanyia wahamiaji mbalimbali.

Wahamiaji kutoka nchi mbalimbali za Afrika wamekuwa wakiuzwa kama watumwa nchini humo. Tayari baadhi ya nchi mbalimbali na hasa za Ulaya zimekuwa zikilaani kuhusiana na tukio hilo. Kwetu Tanzania inawezekana halijatugusa sana, lakini si suala la kuliacha lipite kirahisi hivi.

Libya watakaocheza dhidi ya Kilimanjaro Stars hiyo ya Jumapili wanatokea nchini Libya ambako Waafrika kutoka Afrika Magharibi walikuwa wakiuzwa kama nyanya na Waafrika wenzao kutoka Afrika Kaskazini.

Kuna ‘mentality’ imejengeka kwa watu wengi wanaoishi Afrika Kaskazini kwamba wao wako Ulaya. Wakati fulani tukiwa Cape Verde na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, tuliimbiwa nyimbo zikieleza kwamba wanatuogopa tutawaambukiza ugonjwa wa Malaria.

Nimeona nikiwa Misri, pia Tunisia. Huenda hata hao watu wa Libya walifanya unyama na upuuzi huo wakiamini wao si Waafrika na huenda wanatokea Ulaya.

Kitu kizuri cha kuthibitisha wao ni Waafrika, wanacheza michuano chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na sasa wamealikwa Afrika Mashariki na Kati na wala si upande wa Bara la Asia au Ulaya. Kwao, linaweza kuwa funzo namba moja kama kigezo cha kuiheshimu Afrika na Waafrika.

Hii inaweza isitoshe, nasisitiza, ungekuwa uwezo wangu wangeondolewa mashindanoni ili wafikishe ujumbe kwa wale wapuuzi wa nyumbani kwao walioamua kuwauza ndugu zetu kama vitunguu au maembe sokoni.

Najua Cecafa ni wafanyabiashara, hawawezi kuingia katika jambo hilo hadi lingekuwa na faida kwao kama sasa kupeleka mashindano Nairobi ili kuonyesha Kenya kuna amani ya kutosha na wao itakuwa faida kubwa kwao ukizingatia Musonye ni Mkenya.

Ajabu ni kushindwa kuona ubaya wa Libya, kushindwa angalau kukemea na ikiwezekana kuchukua hatua. Kwa kuwa Libya wanashiriki, basi iko sababu ya ujumbe wa Waafrika kufikishwa kupitia kwao ikiwezekana kwa kuwaonyesha upendo kuliko wanavyotarajia au kuwatuma kwa maneno kwenda kuwaeleza wale wajinga wa nyumbani kwao kwamba, ni lazima kuuheshimu utu wa mwanadamu na Afrika zaidi ni upendo na si upuuzi wanaofanya.



3 COMMENTS:

  1. Heko,kwa ujumbe huu.No mambo matatu nayaona kwenye ujumbe wako.1. Mosyoke kuimiliki cecafa kwa grocery yake.Ni kweli Musyoke anamaguvu mengi sana kwenye shirika hili.tuseme ni lake.
    2.Ule ukimya Wa Afrika kukemea uovu unaotendeka Libya.In unyama.Wakati wazungu wapo mbali wanakemea,cc kimyaaaaa,!!!
    3.utumiaji Wa cecafa kisiasa.hili in jambo LA miaka mingi.vyama vya mipira huko wanaendesha kwa mfumo unaoangalia upepo Wa kisiasa.na hii in nguvu ya rushwa tu.
    Asante umeliona hili.linauma maana hats cc tunfeweza kuomba kujitoa kwenye michuano hiyo ili kuobyesha hatuungi mkono ukatili unaoendelea Libya

    ReplyDelete
  2. SALEIH maoni yako ni mazuri lakini kwa Libya ya sasa mtu mwenye akili zake timamu anakwenda kufanya nini kule? Nasikia wengi wa wahamiaji wanatoka Nigeria? Kweli utajiri waliojaaliwa wanaejeria wakwenda kukimbilia Libya?hata kama ni mlango wa kupitia kwenda ulaya kwani huko ulaya zile nchi zimeshushiwa hali nzuri za maisha kutoka mbinguni? Akufukuzae kabla ya kukwambia toka utaona dalili. Ni ukweli kabisa warabu wa Africa hawajinasibu kuwa ni wa Africa hiyo inajulikana na si kitu kingine isipokuwa ni upuuzi uliowajaa. Mimi siwezi kuwachukia walibya kwa vitendo vinavyodaiwa kuwafanyia wa Africa wenzao. Nazilaumu na nazichukia serikali za nchi za kiafrica na tawala zake kwani licha ya kujaaliwa utajiri mkubwa wa rasilimali lakini wameshindwa kuwatengenezea watu wao mazingira mazuri ya kuishi. Kwani hata wale wahamiaji ambao wengi wao ni vijana ni rasilimali hadimu ni nguvu kazi inawachwa ikiteketea. Lazima sisi wa Africa ifike pahala tuseme enough is enough katika kujitengenezea mazingira mazuri yetu wenyewe ya kuishi kabla ya kufikiria kukimbilia kwa wenzetu. Na kwa heshima kubwa kabisa nachukuwa nafasi hii kumpongeza raisi wa watanzania John Pombe Magufuli kwa kuwa na maono ya mbali ya kuwatengenezea watanzania mazingira mazuri ya kuishi. Siku zote kizuri hakiji bila ya gharama kuna mambo watanzania hasa wale wenye maono finyu wanaweza kukwazika na hatua zinazochukuliwa na serikali ya Magufuli lakini hakika juhudi hizo ni muarubaini wa kuja kutujengea heshima kutoka kwa mataifa yenye kejeli juu ya hali zetu duni za maisha? Tena nimefurahi sana kwa Magufuli kuita hatua anazochukua kurekebisha uchumi ni VITA. Unapoamua kuingia kwenye vita ni hatua ya mwisho kutafuta ufumbuzi wa tatizo hata ikiwa kwa kupoteza maisha,Hongera sana Magufuli. Na Kunako usimamizi mzuri wa rasilimali zetu basi kipindi si kirefu itakuja wakati ukisimama ukisema wewe ni Mtanzania mtu hatofikiria tena kuambukizwa maleria bali atakuwa anafikiria atafikaje Tanzania? Kwa kiasi kikubwa majanga tunayokumbana nayo wa Africa juu ya hali duni ya maisha ni uzembe wetu wenyewe.

    ReplyDelete
  3. Wakati unaitaka cecafa kuiondoa Libya kwenye mashindano, ungeishauri Tanzania kuondoa timu zao kwa sababu Libya inashiriki ili kuonesha kutounga mkono kinachoendelea Huko. Nadhani hiyo ndio njia bora kwa sababu umesema Cecafa haiwezi kuiondoa Libya kwa sababu za kimaslahi. Shauri watu wako wa karibu kwani hata hayo makala yako yanaweza kutoonwa na hao cecafa. Au kuonesha msimamo wenu kuanzia blogu yako na magazeti yenu msiripoti michuano hiyo kuonesha hamkubalini na yanayoendelea Libya. Kinyume na hapo ni unafiki tu wa kutaka kuwalaumu wengine wakati wewe mwenyewe huwezi kuchukua hatua. Ntaendelea kufuatilia blogu yako na magazeti yenu nione mnaripoti michuano hiyo au la, ilinijue ulichoandika kinatoka moyoni au ni katika kusogeza mkono upate kwenda mdomoni.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic