Na Saleh Ally, aliyekuwa Ujerumani
UKIMTAJA kiungo Jay Jay Okocha, itakuwa vigumu sana mtu kusema hukuwahi kusikia taarifa zake hata mara moja.
Jina lake halisi ni Augustine Azuka raia wa Nigeria aliyezaliwa Agosti 14, 1973 ambaye alikua akicheza soka mitaani hadi alipoibuka na kuwa shujaa wa Nigeria, shujaa wa Afrika na mmoja wa nyota wasiosahaulika katika Ligi Kuu ya Ujerumani, maarufu Bundesliga.
Okocha alianza kuibuka kisoka baada ya kuanza kucheza soka nchini Ujerumani akiwa na klabu ndogo ya Borussia Neunkirchen ambayo aliitumikia kwa mechi 35 baada ya kucheza misimu miwili na kufanikiwa kufunga mabao saba.
SALEHJEMBE yenye mfumo wa kutafuta kila habari inayoonekana ni nzuri kwa wasomaji wake na kuwafikishia kwa lengo la kujifunza na kujua zaidi kuhusiana na michezo.
Blogu hii ilifunga safari hadi Ujerumani kwa kushirikiana na StarTimes ambao wamekuwa wakionyesha Bundesliga kupitia king’amuzi chao.
Katika ziara hiyo, Okocha alikuwa sehemu ya nyota walioalikwa kufika katika mechi kadhaa za Bundesliga ikiwa ni pamoja na kuwapa nafasi wanahabari kutoka baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Tanzania, kuzungumza naye.
Okocha ni mtu mtulivu sana na unapopata nafasi ya kumuona utagundua muda wote anaonekana ni mwenye furaha na anayejiamini sana.
Kumekuwa na taarifa nyingi kuhusiana na maisha yake namna yalivyo baada ya kustaafu soka, wengine wakiamini kwamba aliingia katika maisha magumu sana baada ya kustaafu soka.
Lakini ukikutana naye, mambo ni tofauti kabisa na yeye anasimulia kwa kueleza kwamba maisha yake ni ya kawaida lakini si kweli kama wengi ambavyo wamekuwa wakifikiri.
SALEHJEMBE imepata nafasi ya kuzungumza naye ana kwa ana na zaidi kutaka kujua masuala mengi kuhusiana na soka na pia maisha yake baada ya kustaafu.
Unakumbuka kuhusiana na Ronaldinho ambaye alizua mjadala mkubwa kuhusiana na mkongwe huyo kwamba yupi ni mkali zaidi au yupi amekuwa akimuiga mwenzake?
Okocha pia ameeleza maisha yake akiwa PSG na baadaye England lakini Ujerumani alipoanzia katika Klabu ya Eintracht Frankfurt ambayo ni klabu iliyomuinua na kumtangaza katika ulimwengu wa soka.
SALEHJEMBE: Kwanza baada ya kustaafu, kuna taarifa unaishi maisha ya shida kama ambavyo tumesikia wastaafu wengine?
OKocha: Nafikiri ni maneno tu, nina maisha mazuri sana. Nimeamua kubaki nyumbani Lagos, naishi nikiwa na familia yangu na ninaendelea na biashara zangu vizuri kabisa. Si vibaya nikisema nina maisha mazuri.
SALEHJEMBE: Biashara ipi unayofanya?
OKocha: Ziko nyingi, majumba, vyakula na kadhalika. Niseme ninaishi maisha mazuri na endelevu.
SALEHJEMBE: Wachezaji wengi wamefeli na kuishi maisha magumu baada ya kustaafu, Nigeria inaweza kuwa mfano na wengine ulicheza nao. Wewe umeepuka vipi hili?
Okocha: Kweli, limetokea kwa wengi, si Nigeria tu, Afrika na kwingine Ulaya limekuwa tatizo lakini mimi nilijiandaa.
SALEHJEMBE: Ulijiandaa vipi?
Okocha: Nilijua ninacheza na baadaye nitastaafu maana wakati ninacheza wako waliokuwa wamestaafu na niliona. Hivyo nilianza kujipanga mapema kuanzisha biashara wakati nacheza na baada ya kustaafu miradi nimekuwa nikiiendeleza.
SALEHJEMBE: Turudi katika Bundesliga, unaikumbukaje?
Okocha: Kwangu Bundesliga ni shule, Ujerumani ndiyo sehemu nilipata mafunzo yangu ya maisha kisoka.
SALEHJEMBE: Labda fafanua zaidi…
Okocha: Nilikuja Ujerumani nikiwa mvulana, nikaondoka hapa nikiwa mwanamume hasa na utaona watu walikuwa wananikubali ndiyo maana nilienda Uturuki nikafanya vizuri na baadaye nikaenda Ufaransa na kuendelea kufanya vizuri.
SALEHJEMBE: Ulikwenda Fenerbahce halafu ukahamia PSG ambako ulikutana na Ronaldinho ambaye imekuwa ikielezwa umekuwa ukiiga uchezaji wake jambo ambalo limezua mjadala mkubwa. Unaweza kutueleza ilikuwaje?
Okocha: (kicheko), Ronaldinho na mimi imekuwa stori ndefu sana na kila mmoja akisema lake lakini ukweli naujua mimi. Ilikuwa hivi…
KESHO tutaendelea na makala hii na Okocha ataelezea namna alivyoishi na Ronaldinho wakiwa PSG na ukweli kuhusiana na nani ambaye amekuwa akicheza kwa kumuiga mwenzake kama ambavyo imekuwa ikizua mjadala. USIKOSE, ITAENDELEA KESHO JUMAMOSI.
Duh Broh Salehe Sasa umeamua kutuwekea makala katika mtindo wa Tamthilia......Sidhani kama hii inafaa zaidi.
ReplyDeleteThis comment has been removed by the author.
ReplyDelete