NA SALEH ALLY
NAFIKIRI itakuwa ni mara ya nne sasa nimeelezwa kuwa Kocha wa Makipa wa Yanga, Juma Pondamali amekuwa ananisaka kila kona akiwa ameahidi kuwa anataka “kunitoa shoo.”
Pondamali ananitafuta kutokana na kukerwa kwa kiasi kikubwa na mimi kuzungumzia suala la kutaka makocha wa makipa nao kujiongezea ujuzi zaidi ili kuendana na mwenendo sahihi katika kipindi husika.
Wiki mbili zimepita sasa Tangu nilipoandika makala inayohusiana na msisitizo wa kuwaona makocha wa makipa nao wanaimarika zaidi kulingana na mbinu mpya za kisasa.
Katika makala yangu hiyo, niligusia mambo mbalimbali lakini yote yakiwa yanahusiana na makocha wa makipa hapa nchini.
Kwanza ilikuwa ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuwatafutia kozi maalum fupifupi kwa kuwasiliana na mashirikisho mbalimbali kama Caf na Fifa na kadhalika.
Nikasisitiza, TFF ina nafasi kubwa ya kupata kozi hizo kwa kuwa ina uhusiano mzuri na mashirikisho mengine makubwa yanayoweza kutoa msaada.
Wakati nikisisitiza kwamba makocha wa makipa nao wanatakiwa kufundishwa mbinu mpya nilieleza namba ambavyo kuna kila mbinu mpya wanaofundishwa washambulizi na viungo ili kuwashinda makipa.
Nilisema halikuwa jambo sahihi upande mmoja unafundishwa na mwingine ukiwa kimya. Nikatoa mfano wa makocha wa makipa ambao ninaona wamejifunza siku nyingi na walitakiwa kujiimarisha zaidi badala ya kutumia uzoefu au kipaji kama sasa.
Nilimtaja Pondamali kwamba hawezi kuendelea kufundisha na mwaka 1947, huku nikiwataka makocha wengine kama Mwarami Mohammed wa Simba na wengineo.
Ajabu, nimekuwa nikisikia moja ya mambo yanayofanya Pondamali anitafute ni kwa kuwa nimefananisha na Mwarami ambaye ni mwanafunzi wake kwa kuwa alimfundisha katika kikosi cha Taifa Stars wakati alipoteuliwa na kama unakumbuka wakati Taifa Stars ikichapwa na Brazil mabao 5-1, yeye alikuwa langoni.
Jambo la pili ambalo Pondamali amelalamika, ni kwamba nimesema hana vyeti. Hivyo alikuwa akizunguka na rundo la vyeti na alinitafuta huku akitishia atanishitaki mahakamani.
Awali, nilitaka kumpigia simu, lakini nilitaka kujitofautisha naye na kubaki nikimsubiri ili nijue malalamiko yake kwa kuwa niliyoelezwa niliona hayana msingi na huenda wafikishaji hawakuwa sahihi.
Mmoja wa wajumbe aliowatuma, walinifikishia ujumbe kwa sauti jambo ambalo lilinisikitisha kuona Pondamali akisoma nilichoandika halafu hakuelewa hata kitu kimoja na anaonekana kaelewa tofauti utafikiri nilitumia lugha ya Kirumi.
Mara ya mwisho nakumbuka kulikuwa na kozi ya makipa kupitia akademi ya Ivo Mapunda ambaye aliomba msaada na mtaalamu kutoka Keepers Foundations nchini Poland ndiye alikuja nchini kufundisha akisaidia na kocha wa makipa wa zamani wa Simba, Iddi Salim raia wa Kenya ambaye ana leseni ya Uefa katika kazi hiyo.
Mafunzo hayo ya Julai 14, 2017 yaliyofanyika pale Karume, yaliegemea mafunzo na umuhimu wa uwepo wa kocha wa makipa, maandalizi ya msingi kwa makipa mazoezini na kutumia mbinu mwafaka katika wakati mwafaka hasa katika kipindi hiki kiitwacho “new era”, si vibaya ukasema kizazi kipya. Sikumbuki kama Pondamali alishiriki.
Huenda Ivo Mapunda amesaidiwa pia na kufanya kazi nje ndiyo maana aliona haraka jambo hilo akaomba wataalamu kutoka Poland na Kenya na ninaamini walioshiriki walifaidika.
Sasa wakati ninaomba makocha wa makipa wasaidiwe, mmoja wao analalamika kufananishwa na wengine akilia kupitia mifano na mbaya zaidi anaangalia ukongwe badala ya ubora.
Nafikiri kuna haja ya kujifunza na kuachana na kuamini visivyowezekana. Wakati mwingine ni bora kusikiliza kuliko kusema na wakati wa kusoma vizuri kuyakubali maandishi yafike kwenye ubongo kupitia machoni badala machoni kupafanya ndiyo kutuo cha maamuzi.
Naweka msisitizo, makocha wa makipa watafutiwe mafunzo ya kisasa nao pia wajiendeleze hata kupitia mitandao. Naendelea kumsubiri Pondamali.
We nae unalialia kama mtoto
ReplyDelete